Yanga hesabu zimekataa! Yashindwa kutinga robo fainali CAFCL

HESABU zimekaa. Ndicho kilichotokea jana kwa wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya CAF baada ya Yanga jana usiku kupata ushindi wa mabao 3-0 nyumbani mbele ya JS Kabylie ya Algeria, lakini ikajikuta ikiaga Ligi ya Mabingwa Afrika ikiungana na Simba, Azam FC na Singida BS zilizoaga mapema.

Yanga ilikuwa ikisikiliza matokeo ya jijini Cairo wakati kinara wa Kundi B, Al Ahly ya Misri ilipokuwa ikimalizana na AS FAR Rabat ya Morocco na kwa bahati timu hizo zilishindwa kutambiana kwa kutoka sare zilizozivusha zote kwenda robo fainali ya michuano hiyo.

Yanga imekamilisha mechi sita kwa kuvuna pointi nane kama ilivyokuwa msimu uliopita, baada ya kushinda mbili, sare mbili na kupoteza pia mbili, huku Al Ahly ikimaliza kileleni mwa kundi ikiwa na pointi 11 na AS FAR ikivuna tisa, ikikamilisha timu nane zilizopenya robo fainali.

Kung’oka kwa Yanga kumeifanya Tanzania kumaliza msimu kwa aibu, licha ya awali kuanza kwa heshima ya kuingiza timu nne hatua ya makundi ikiwa sambamba na Misri, Morocco na Algeria.

Hata hivyo, ni Misri na Morocco pekee zilizoingiza timu zote nne robo kwa sasa katika michuano ya CAF, huku Algeria ikipenyeza mbili zote zikiwa katika Kombe la Shirikisho.

hatua ya robo fainali mechi zake za awali zinatarajiwa kupigwa kati ya Machi 13-14 na zile za marudiano zitachezwa Machi 20-21 kupata timu nne za kila michuano kwenda nusu fainali na droo ya mechi zote hizo hadi ile ya fainali ikitarajiwa kufanyika kesho Jumanne.

Katika mechi ya jana, Yanga licha ya kusaka ushindi kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, lakini ilikuwa ikisikilizia matokeo ya Cairo, ili kuona kama ingetoboa mbele ya maafande wa As Far Rabat iliyokuwa inachuana nao kukamilisha nafasi moja ya kwenda robo kwa timu za Kundi B.

Lakini hesabu ziligoma baada ya Waarabu kushindwa kutambiana kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo na kumtibulia kocha Pedro Goncalves na jeshi hilo la Jangwani na sasa inarudi nyumbani kujipanga upya kutetea mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho michuano inayotoa tiketi za CAF.

Katika mechi ya leo, kocha Pedro alianza na washambuliaji wawili, Depu na Prince Dube, huku akiwaanzisha benchini Bakar Mwamnyeto na Chadrack Boka aliyeingiza kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Allan Okello na timu kwenda mapumziko ikiongoza kwa bao 1-0.

Bao hilo lilitokana na penalti iliyoweka kimiani na Depu baada ya Pacome Zouzoua kufanyiwa madhambi na kipa wa JS Kabylie, Seif Benrabah wakati alipokuwa akitaka kufunga na mwamuzi Jean Jacques Ndala kutoka DR Congo kuamuru pigo hilo na Depu kukwamiza wavuni kiufundi dakika ya 36.

Hata hivyo, Yanga ilipata pigo baada ya Pacome kushindwa kuendelea na mechi hiyo dakika nne baadaye kutokana na kutolewa uwanjani, nafasi yake ikichukuliwa na Mudathir Yahya.

Kipindi cha pili Yanga ilirudi na moto na kuandika bao la pili dakika ya 63 kupitia kwa Depu tena akimalizia pasi murua ya Okello na kuufanya uwanja wa Amaan utapike kwa shangwe.

Dakika mbili baadae Pedro alimtoa Okello na kumuingiza Boka aliyetumia sekunde 40 tu uwanjani kabla ya kufunga bao la tatu la Yanga akimalizia pasi ya Dube na kufanya mashabiki kupagawa, wakionekana kuchungulia kila mara simu zao wakifuatilia matokeo ya mechi ya Al Ahly na As FAR.

Sio kwa mashabiki tu, hata viongozi wa klabu hiyo akiwamo Rais Injinia Hersi Said na Makamu wake, Arafat Haji walionekana wakishughulika na simu zaidi, wakati mwingine wakionekana wakipiga kabisa kama watu wanaoulizia matokeo kutokana na netiweki uwanjani hapo kusumbua kwa muda mrefu.

Matokeo ya usiku wa leo imeifanya Yanga kumaliza mechi ikikusanya pointi nane na mabao matano ya kufungwa na yenyewe kufungwa matatu na kuaga michuano, ikirejea tukio la mwaka leo ilipokwama mbele ya timu ya kutoka Algeria, MC Alger japo hii imetokana na matokeo ya Cairo.

YANGA: Diarra, Mwenda, Tshabalala, Job, Bacca, Abuya, Okello, Maxi, Dube, Depu na Pacome.

Benrabah, Boulkaboul, Bellaouel, Belaid, Hamid, Bott, Bada, Sarr, Akhrib, Messaoudi na Malki.