Arusha. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitaka mamlaka hiyo kuongeza wigo wa utoaji huduma wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha.
Rais Samia alitoa maagizo hayo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2025 akisema ndani ya siku 100 za utawala wake ataongeza wigo wa huduma za kodi.
Jana Jumamosi, Februari 14, 2026, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alifanya ziara Karatu ambapo alizungumza na walipa kodi pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Lameck Karanga.
Mwenda alisema katika hatua za awali za utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo waendeshaji wa shughuli za utalii, kabla ya kufanya uamuzi wa aidha kuanzisha mkoa wa kodi au kupanua huduma.
Amesema TRA itaendelea kuwapatia huduma bora walipakodi kote nchini wakiwemo wa Wilaya Karatu na kuwa itaendelea kuwasikiliza na kutatua changamoto zao.
“Napenda kuwahakikishia walipakodi wote kwamba tutaendelea kuwezesha biashara zenu na kuwapa huduma bora huku tukitumia zaidi mifumo ya kidijitali ikiwemo IDRAS,” amesema Mwenda.
Amesema TRA itaendelea kutoa elimu ya kodi mara kwa mara kwa walipakodi
Kwa upande wake, Dk Karanga amesema wamefurahishwa na ujio wa Kamishna Mkuu kwenye eneo lao akieleza kuwa wilaya anayoiongoza ina uchumi mkubwa ambao unaotokana na shughuli za utalii.
Amesema wamekuwa wakishirikiana na TRA katika masuala mbalimbali ya kodi hali iliyowezesha kuvuka malengo ya makusanyo kwa miezi yote.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Shughuli za Utalii (Tato), Mkoa wa Arusha, Wilbard Chambulo amepongeza utendaji kazi wa TRA ambao umeisogeza karibu na wananchi hali ambayo imeongeza makusanyo ya Kodi kwa wilaya ya Karatu.
Amesema wafanyabiashara wa mji wa Karatu wapo tayari kulipa kodi kwa hiari na kupongeza mfumo mpya wa usimamizi wa mapato ya ndani wa IDRAS, ambao ni wiki moja sasa tangu uanze kufanya kazi lakini tayari wameanza kuonja matunda yake kupitia huduma zinazotolewa na mfumo huo.
Amesema mfumo wa IDRAS utakuwa mwarobaini wa changamoto nyingi za kikodi ikiwemo kuokoa muda wa walipakodi kwenda kufuata huduma za kodi TRA.
“Kupitia mfumo huu kutakuwa na usawa katika ukadiriaji wa kodi maana mfumo huu ni wa uwazi na unaonyesha mauzo, manunuzi na faida hivyo Mlipakodi atapata faida yake na TRA watapata kodi yao,” amesema Chambulo.
Kuhusu ukwepaji kodi, Chambulo amesema wanaokwepa kodi kwa kutokutoa risiti hawana nafasi kwenye sekta ya utalii ambapo wamekuwa wakiwatenga katika kuwapa huduma za manunuzi ya vitu mbalimbali, hali inayowalazimu nao kuanza kutoa risiti.
Naye Esther Dominic akizungumza katika kikao hicho amesema IDRAS itasaidia kuokoa muda wao na kuwa shughuli nyingi zimerahisishwa ikiwemo kuomba namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) mtandaoni.