AZAM FC leo imekamilisha ratiba ya meci za makundi kwa kipigo cha mabao 2-0 ugenini mbele ya Wydad AC ya Morocco na kuunganana na Singida Black Stars kung’oka katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Wawakilishi hao wa Tanzania walikumbana na kipigo hicho kwenye Uwanja wa Mohammed V, Casablanca ambapo licha ya kukomaa na kwenda mapumziko ikiwa nguvu sawa na wenyeji, hali ilibadilika na kuruhusu mabao mawili kipindi cha pili na kuifanya isalie nafasi ya tatu katika Kundi B.
Jahazi la Azam lilianza kuzama katika dk64 baada ya beki wa kushoto, Pascal Msindo kushindwa kuokoa mpira uliopigwa na nyota wa Wydad, Hakim Ziyech.
Ziyech aliyewahi kutamba na timu mbalimbali Ulaya ikiwamo Chelsea ya England, alikuwa mwiba mkali kwa kikosi cha Azam, baada ya kusababisha bao la pili dakika ya 90+4, lililofungwa na Walid Nassi aliyechukua nafasi ya Hamza Hannouri.
Bao hilo lilitokana na shuti kali lililopigwa na Ziyech na kumkuta kipa wa Azam, Aishi Manula aliyeokoa, ingawa jitihada hizo hazikuweza kuzaa matunda, baada ya Walid Nassi kuunasa mpira uliotemwa na kuihakikishia ushindi wa moja kwa moja.
Azam ilianza mechi hiyo vizuri kwa kushambulia kwa kushtukiza ikiwategemea Idd Seleman ‘Nado’, Zidane Sereri waliokuwa wanatokea upande wa pembeni na mshambuliaji, Jephte Kitambala, ingawa wenyeji waliingia kipindi cha pili kwa kasi zaidi.
Hata hivyo, ubora wa, Aishi Manula, uliifanya Azam kuepuka kufungwa mabao mengi, baada ya kipa huyo aliyerejea ndani ya timu hiyo msimu huu akitokea Simba kuokoa michomo ya hatari zaidi ya minne iliyopigwa na nyota wa Wydad, Ziyech.
Azam iliingia katika mechi hiyo ikitaka kulipiza kisasi baada ya kuchapwa nyumbani kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, bao 1-0, la Nordin Amrabat, Novemba 28, 2025, ingawa licha ya jitihada kubwa ila hazikufanikiwa pia.
Matokeo hayo yaliifanya Wydad kufikisha pointi 15 na kufuzu hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo katika Kombe la Shirikisho Afrika, ikiungana na AS Maniema Union ya DR Congo iliyofikisha pointi 12.
Maniema Union imefikisha pointi 12, baada ya kuifunga Nairobi United ya Kenya mabao 3-0, iliyochapwa mechi zote sita za hatua ya makundi, huku kwa upande wa kikosi cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam ikimaliza kundi B na pointi zake tisa.
Azam FC iliandika historia mpya katika michuano ya CAF, baada ya kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake Julai 23, 2004 ikifahamika kwa jina la Mzizima FC na kuvuna pointi nyingi (tisa) ikishinda mechi tatu mfululizo.
Katika mechi nyingine ya michuano hiyo, kwa kundi C Singida Black Stars ikiwa ugenini Afrika Kusini, ilijitutumua na kutoka suluhu na Stellenbosch na kuifanya timu hiyo inayoshiriki makundi kwa mara ya kwanza ikimaliza na pointi tano sawa na wenyeji wa hao.
Hata hivyo, Singida itajilaumu kwa kushindwa kutokaa na ushindi ugenini kwani wenyeji wao walicheza pungufu kwa muda mrefu baada ya Asekho Tiwani kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu dakika 45 ya mchezo huo.
Matokeo hayo yameifanya Singida kumaliza nafasi ya tatu juu ya Stellenbosch licha ya kulingana pointi, lakini zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, kwani mechi ya awali baina ya timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Singida kama wawakilishi wengine wa michuano hiyo zilizotolewa zinarudi sasa katika mechi za Kombe la Shirikisho (FA) hatua ya 64 Bora na Ligi Kuu Bara.