Na: Mwandishi Wetu, DAR
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeanza rasmi kupokea maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ngazi ya Stashahada (Diploma) katika kozi za vipaumbele wanaotarajiwa kudahiliwa mwezi Machi, 2026.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, Jijini Dar es Salaam ambapo dirisha la maombi ya mikopo hiyo limefunguliwa Februari 15, 2026 hadi Machi 15, 2026.
“Niwahimize wale wote wanaotarajiwa kudahiliwa mwezi Machi, 2026, katika kozi za vipaumbele kutumia vyema dirisha hili la uombaji mikopo ili waweze kutimiza malengo yao ya kielimu,” amesema Dk. Kiwia.
Katika hatua nyingine, Dk. Kiwia amewasisitiza waombaji wote kusoma vyema mwongozo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya Stashahada unaopatikana katika tovuti ya Bodi ya Mikopo ili kuzingatia vigezo muhimu vilivyoainishwa.
Kimsingi, serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo wa kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata elimu bila vikwazo ambapo elimu ya Awali hadi Kidato cha Sita inatolewa bila ada.
Kwa upande wa elimu ya kati na Ile ya ngazi ya Stashahada katika kozi za vipaumbele na kozi nyingine za Shahada, serikali kupitia HESLB inatoa mikopo ili kuwawezesha vijana wengi zaidi hasa wanaotoka familia zenye changamoto za kiuchumi kupata mikopo hiyo ya elimu kwa ustawi wa maisha yao.