KOCHA Mkuu wa Dodoma Jiji, Aman Josiah amelitaja suala la saikolojia kwa wachezaji kuwa ni eneo muhimu nje ya uwanja ambalo makocha wanapaswa kulijua ipasavyo.
Josiah amesema kocha mwenye diploma A ya Shiriksho la Soka Afrika (CAF), ni lazima apitie eneo la saikolojia litakalomsaidia kuwajua wachezaji na kuendana nao ili kutimiza malengo ya timu.
“Mbali na majukumu ya uwanjani, kocha anasimama kama mlezi, mshauri na lazima awe na udikteta kidogo ili kuwasaidia wachezaji kuwa na nidhamu, ukitumia hekima pekee wengine ni wasumbufu, lakini umuhimu wa wanasaikolojia upo ingawa makocha wengi tunafanya jukumu hilo,” amesema Josiah na kuongeza;
“Mfano mchezaji chipukizi kafanya vizuri msimu mmoja unaofuata anapotea kabisa, moja ya sababu ni familia wanazotokea wanakuwa wanawaona wana pesa, tofauti na uhalisia wa mchezaji, jina la mchezaji likianza kuwa kubwa ni vizuri akawa na wasimamizi wazuri na siyo pesa zake.
“Kitu kingine ninachokifanya naweza nikaamka usiku naangalia namba za wachezaji ambao wapo online, siwapigii simu ila tukifika mazoezini, nawaeleza kwa upendo wewe ulichelewa kulala ndiyo maana unashindwa kucheza vizuri, mchezaji anayecheza kwa muda mrefu katika kiwango anazingatia kulala vizuri, chakula, kunywa maji na juisi asilia.”
Amesema ili kuweza kumudu majukumu yote, anapotoka mazoezini anapitia data za mchezaji mmoja mmoja, kisha anajitenga mwenyewe kupumzika akisikiliza muziki wa dini na wa taratibu, baadaye anaanza kujisomea ili kuongeza ujuzi.
“Kuna wakati nawafuatilia makocha mbalimbali kama Jose Mourinho, Jurgen Klopp, Pep Guardiola na wengine, naangalia ni vitu gani vya kuniongezea katika kazi yangu,” amesema.
Kwa upande wa kocha wa Songea United, Meja Mstaafu, Abdul Mingange amesema: “Saikolojia kwa wachezaji ni kitu kikubwa, kwani wanatoka katika maisha yenye historia tofauti, wengine wanakuwa na changamoto nzito za wenza wao, hivyo nje na kocha kufanya majukumu hayo ni muhimu kuwepo wanasaikolojia.”
Staa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Emmanuel Gabriel amesema: “Nimtolee mfano mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah ni bonge la mchezaji, lakini ninachokiona anapaswa kukaa na wanasaikolojia, ili kumsaidia kupunguza makosa ya uwanjani, kunaweza kukawa na vitu nje ya kazi na huenda haoni kama anakosea akijengwa atafanya vizuri, maana changamoto hizo hajaanzia Simba.”
Nahodha wa Namungo, Jacob Masawe amesema: “Kuna umuhimu mkubwa wa wanasaikolojia kuwepo katika timu, mchezaji unaweza ukawa fiti, lakini kama akili haipo vizuri inakuwa changamoto.”
Mwanasaikolojia Charles Nduki, alielezea umuhimu wao wa kufanya kazi na wanamichezo: “Mchezaji anapokuwa anaingia uwanjani, akili yake inatakiwa iwe na utayari na kuacha changamoto nje, maana akiwa amezidiwa na mawazo anaweza akafanya vitu vya hovyo ambavyo vinaweza vikawa vinashangaza wengine, mfano kukosa nidhamu, wakati mwingine na umakini unakuwa mdogo.”