MSHAMBULIAJI mpya wa Mbeya Kwanza, Lucas Sendama, amesema kwa sasa ameamua kujipanga upya ili kurejesha kiwango chake, baada ya kukosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara akiwa na maafande wa Tanzania Prisons kwa msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, mshambuliaji huyo aliyejiunga na Mbeya Kwanza dirisha dogo la Januari 2026, amesema ameamua kujipanga upya kwa ajili ya kurudisha kiwango chake cha mwanzoni, licha ya ushindani na washambuliaji wenzake kikosini.
“Sijutii kucheza Championship ambapo mimi ndipo nilipoanzia, malengo yangu ni kufanya vizuri na kuisaidia Mbeya Kwanza kupanda daraja kwenda Ligi Kuu Bara, nashukuru nimepata mapokezi mazuri kutoka kwa wachezaji wenzangu,” amesema Sendama.
Mshambuliaji huyo aliyezichezea pia KenGold, Geita Gold, Biashara United na DTB iliyobadilishwa jina baadaye na kuitwa Singida Big Stars baada ya kupanda Ligi Kuu Bara, alijiunga na Prisons Agosti 14, 2025, baada ya kuondoka Stand United.
Msimu wa 2024-2025, Sendama aliifungia Stand mabao manne Ligi ya Championship na kuiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu na pointi 61, jambo lililosababisha kucheza mechi za (Play-Off) kusaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara na kukwama.
Stand ilicheza mtoano na Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56 na kuiondosha kwa kuichapa jumla ya mabao 4-2, kisha hatua iliyofuata ikakutana na Fountain Gate iliyotolewa na Tanzania Prisons na kikosi hicho kuchapwa jumla ya mabao 5-1.