Prisons yaipeleka Simba Dodoma, Otieno bado hakijaeleweka

SIKU chache baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuufungia Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Tanzania Prisons imesema inatarajia kutumia Uwanja wa Jamhuri uliopo Dodoma kuikaribisha Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku ikieleza hatma ya Kocha Mkuu, Zedekiah Otieno.

Februari 14, 2026, TFF ilitangaza kuufungia uwanja huo kwa kutokidhi matakwa ya kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya kanuni za leseni za klabu, ikiwa ni muda mchache tangu kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Bara ambapo Prisons iliichapa Namungo mabao 3-2.

Prisons inatarajia kushuka uwanjani Februari 22, 2026 kuikaribisha Simba, mechi ambayo ilitarajiwa kupigwa Uwanja wa Sokoine na sasa itapigwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma sawa na mechi ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Moro Kids, itakayotangulia kuchezwa Februari 19, 2026.

Katibu Mtendaji wa Prisons, Godfrey Madegwa, ameliambia Mwanaspoti kuwa, hadi sasa mipango yao ni kupeleka michezo hiyo jijini Dodoma, ambapo wanasubiri kuwasilisha tu taarifa kwa mamlaka za soka kuthibitishwa.

Amesema walitamaani michezo hiyo ipigwe Sokoine ili kuwapa burudani mashabiki na wadau wa soka jijini Mbeya, lakini kutokana na jambo hilo kuwa nje ya uwezo wao na sasa wataenda Dodoma.

“Tunajua ni mchezo mgumu lakini ni muhimu sana kwetu, uongozi unaendelea kuweka mambo sawa kiutawala kuhakikisha tunaendeleza ushindi baada ya kufanya hivyo dhidi ya Namungo.

“Bonasi ni kawaida kwa Prisons kutoa kwa wachezaji pale timu inaposhinda, hatuna matokeo mazuri hivyo kila mechi kwetu ni vita ya pointi tatu, tutatumia mchezo wetu dhidi ya Moro Kids kama kipimo kuwakabili Simba,” amesema Madegwa.

Ameongeza kuwa, kinachowapa nguvu na morali ndani na nje ya uwanja ni ushindi walioupata mechi iliyopita akieleza kuwa kwa sasa presha imeshuka baada ya kusota kwa muda mrefu bila matokeo mazuri.

Kuhusu hatma ya Kocha Otieno, kigogo huyo amesema hawafanya uamuzi kwani bado anao mkataba na kinachosubiriwa ni kamati ya usajili kuamua.

“Huyu ni kocha wa kigeni kwahiyo zipo taratibu za kuachana naye, lazima kuwepo makubaliano ya pande zote, iwapo itaamuliwa hivyo tutatangaza, lakini hadi sasa tuko naye kambini,” amesema.

Timu hizo zinakutana ikiwa rekodi inawabeba Simba baada ya msimu uliopita kushinda nyumbani na ugenini kwa jumla ya mabao 4-0. Simba ipo nafasi ya saba kwa pointi 19 baada ya mechi nane, huku Prisons ikiwa nafasi ya 14 kwa pointi 12 ikicheza mechi 13.