Dar es Salaam. Shahidi wa saba wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameieleza Mahakama kuwa aliposikia ujumbe wa Lissu wa kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, alihamasika na akajiandaa kwa utekelezaji.
Shahidi huyo, ambaye ni miongoni mwa mashahidi fiche wa Jamhuri (waliopewa ulinzi, yaani wasiotakiwa kuonekana wala kutambulika), anatoa ushahidi akiwa ndani ya kizimba maalum ambamo hawezi kuonekana na wasikilizaji wala mshtakiwa isipokuwa kwa majaji tu. Ametambulishwa kwa jina la P2 (34).
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kweli kweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Kwa mujibu wa shahidi huyo leo Jumatatu, Februari 16, 2026, akiongozwa na Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Ignas Mwinuka, shahidi huyo wa saba ni mkazi wa Matalawe, Songea, Mkoa wa Ruvuma.
Yeye ni fundi umeme na ni mfuasi wa Chadema tangu mwaka 2021, na amekuwa akishiriki katika mikutano mbalimbali.
Aprili 4, 2025, saa 4, akiwa kwenye shughuli zake, alipitia mitandao ya kijamii kuangalia yaliyojiri. Katika mtandao wa kijamii wa YouTube, alikutana na video ya Lissu ya mkutano na waandishi wa habari akieleza kuwa mwaka huo hakutakuwa na uchaguzi na kwamba waliokuwa wanataka kugombea udiwani, ubunge na urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 wasahau.
Katika maelezo hayo, Lissu alisisitiza namna ya kuzuia Uchaguzi Mkuu usifanyike kama njia ya kuleta mabadiliko na akawataka kila mmoja kuwa jasiri.
Baada ya kupata ujumbe huo, aliwafuata viongozi wa Chadema Songea kupata ufafanuzi kuhusu namna ya kutekeleza ujumbe huo.
Alimfuata Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Esau Chiza, ili kupewa ufafanuzi, na Chiza aliwaelekeza kuwa wanaendelea kuwasiliana na viongozi kupata mwongozo. Aprili 7, 2025, akawambia kuwa kuna ziara ya Mwenyekiti itafanyika Mkoa wa Ruvuma, na akachangia Sh10,000 kuwezesha ziara hiyo.
Chiza alimweleza kuwa katika Wilaya ya Songea mkutano ungefanyika Aprili 10, 2025, katika uwanja wa Shule ya Msingi Matalawe, hivyo aliendelea na shughuli zake.
Aprili 9, 2025, wakati akidurusu mitandao ya kijamii, alipata taarifa kuwa Lissu alikuwa amekamatwa. Hivyo, kesho yake Aprili 10 asubuhi alijiandaa kwenda mkutanoni kupata taarifa zaidi.
Alipofika eneo la DS Kitimoto, alikuta magari ya polisi waliowaeleza kuwa hakuna mkutano na kuwataka watawanyike.
Baadaye mchana alikwenda katika ofisi za Chadema eneo la Mfaranyaki, huku akiwasiliana na wanachama wengine wa Chadema. Aliwakuta viongozi wa Chadema wa mkoa na kitaifa, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche.
Viongozi hao walikuwa wanajiandaa kuongea na waandishi wa habari, lakini kabla ya kuanza mazungumzo hayo, yalifika magari ya polisi waliowakamata na kuwapeleka kituo cha polisi, ambapo aliwekwa mahabusu na baadaye alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi.
Baada ya kuchukuliwa maelezo, aliachiwa kwa dhamana akitakiwa kuripoti kituo cha polisi kila Jumatatu. Mara ya pili alipokwenda kuripoti Aprili 22, 2025, baada ya Jumatatu ya Pasaka, alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Songea.
Huko alichukuliwa tena maelezo na askari Baltazar na akaambiwa aeleze yote anayoyafahamu yaliyosababisha mpaka akakamatwa.
Hakujua uchaguzi huo ungezuiwa vipi, lakini kwa kuwa Mwenyekiti alikuwa na ziara ya Ruvuma, alitarajia angewapa ufafanuzi wa namna gani wangezuia kwa uasi na kuhamasisha. Hata hivyo, alivutiwa na maelezo hayo na akahamasika, hivyo akajiandaa.
Baada ya shahidi huyo kumaliza ushahidi wake, kabla ya mshtakiwa Lissu kumhoji maswali ya dodoso, alimsomea kwanza maelezo yake aliyoyatoa polisi Aprili 22, 2025, na kumuuliza kama ndiyo maelezo yake. Shahidi huyo akakubali kuwa ni yake.
Pia Lissu alimuuliza kama angependa maelezo hayo yawasilishwe mahakamani kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa utetezi (upande wa mshtakiwa), naye akakubali.
Upande wa mashtaka, jopo la waendesha mashtaka linaloongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Lenatus Mkude, uliieleza Mahakama kuwa hauna pingamizi maelezo hayo ya shahidi wa Jamhuri kupokewa kama kielelezo cha upande wa utetezi.
Hivyo, Mahakama imeyapokea maelezo hayo na kuyasajili kuwa kielelezo cha sita cha upande wa utetezi (D6).
Kwa mujibu wa maelezo hayo, pamoja na mambo mengine, hajapata kadi ya uanachama wa Chadema licha ya kulipia, kwani aliambiwa kuwa kadi hizo ni za kidijitali.
Hata hivyo, amekuwa katika timu ya Lissu kwani amekuwa mfuasi wa mwanasiasa huyo nguli, na baada ya kupata ujumbe wa Lissu wa kuzuia uchaguzi kwa “kukinukisha”, alijiandaa kukinukisha.
Usikose sehemu ya mahojiano hayo baina ya mshtakiwa Lissu na shahidi huyo wa Jamhuri.