Makonda ampa msajili siku 12 kumaliza utata Simba

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amemtaka Msajili wa Vyama vya Michezo Tanzania, kuipa Simba majibu ya kinachoendelea kuhusu mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji.

Makonda amesema, msajili anatakiwa kabla ya mwezi Februari 2026 kumalizika, awe ametoa majibu kwa Wanasimba.

“Msajili wa michezo nilitaka mkamilishe taratibu za Simba. Na nilitaka niwahakikishie kwamba katika kipindi ambacho sheria na kanuni zitafuatwa sana ni hiki cha uongozi wangu.

“Kamilisha na ikiwezekana kabla ya mwezi huu uwape majibu Wanasimba. Tunachotaka sisi tuone timu hizi zikifanya vizuri. Kabla ya mwezi huu, jambo hili liwe limekamilika,” amesema Makonda.

Agizo hilo la Makonda limekuja siku sita tangu Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji, kuhoji ulikofikia mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo

“Transformation mmefikia wapi?” aliandika Dewji, wakati akichangia taarifa iliyotolewa na klabu hiyo ikinukuu kauli ya Mwenyekiti wake, Murtaza Mangungu kuhusu urejeshaji wa usajili wa wanachama, jambo lililoibua gumzo miongoni mwa mashabiki.

Siku moja baadaye, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema kuwa wanaopaswa kutoa majibu ya hilo ni serikali.

“Binafsi sijaona na nasikia tu lakini nyie mnapaswa kumuuliza yeye kwa nini ametumia njia hiyo na kwa nini ameuliza hivyo. Mimi sina ninachoweza kujibu, sina jibu. Kwa sasa mchakato wa ‘Transformation’ unaendelea na upo katika vyombo vya serikali,” alisema Mangungu. 

Inaripotiwa kwamba, yapo mapendekezo ambayo Simba ilitakiwa kuyafanya ili mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo ukamilike na ndio yamechangia hadi sasa ukwame kwa msajili.

Baadhi ya mapendekezo hayo ni kubadilisha kipengele cha katiba na kutoa nafasi kwa wawekezaji watatu badala ya mwekezaji mmoja na pia kufanya tathmini ya thamani halisi ya klabu pia kutoa nguvu kwa upande wa wanachama.