Vifaa saidizi, Sh342 milioni za mikopo yatolewa Mtwara Mikindani

Mtwara. Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani imekabidhi vifaa saidizi na Sh342 milioni za mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Vifaa na fedha hizo zimekabidhiwa leo Jumatatu, Februari 16, 2026 na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga.

Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa sera na mwelekeo wa maendeleo unaolenga kujenga uchumi jumuishi unaowawezesha wananchi wote kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya Taifa.

Nderiananga amesema mikopo hiyo inalenga kuchochea na kuinua uchumi wa chini kwenda juu sambamba na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya kujenga uchumi shindani, jumuishi na endelevu ifikapo mwaka 2050.

Amesema utoaji wa vifaa saidizi, ikiwemo viti mwendo, magongo, fimbo nyeupe za wasioona pamoja na taulo za kike, ni utekelezaji wa sera ya kutomwacha mtu nyuma katika safari ya maendeleo, sambamba na maono ya kitaifa ya kujenga jamii yenye heshima, utu na usawa wa fursa.

“Mikopo hii inalenga kuchochea na kuinua uchumi wa chini kwenda juu sambamba na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya kujenga uchumi shindani,” amesema Naibu Waziri Nderiananga.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Dk Joel Nanauka, ameweka wazi kuwa Serikali katika jitihada za kuwakwamua wananchi kiuchumi itaendelea na utekelezaji wa kupeleka miradi mikubwa ya kimkakati katika Mkoa wa Mtwara, ikiwemo kuboresha Bandari ya Mtwara, ujenzi wa reli na uboreshaji wa uwanja wa ndege pamoja na marekebisho ya miundombinu ya barabara.

Dk Nanauka amehimiza wanufaika wa mikopo hiyo kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati ili kushirikiana katika kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo chanya kwao binafsi na Taifa kwa ujumla.

“Niwatake wanufaika wote wa mikopo kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati ili kushirikiana katika kuhakikisha mikopo inaleta matokeo chanya,” amesema Dk Nanauka.

Naye Jamila Abdallah, mmoja wa kikundi cha vijana, ameishukuru Serikali kwa kuweza kuwapatia vifaa saidizi pamoja na fedha kwa ajili ya kuweza kujikwamua kiuchumi.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuweza kutuona sisi tuliokuwa na uhitaji kwa kutupatia vifaa saidizi pamoja na fedha kwa ajili ya mikopo. Imani yangu tutakwenda kurejesha kwa wakati na kuweza kusonga mbele zaidi,” amesema Abdallah.