SMZ yakiri kutokuwa na takwimu za ajira kwa wageni, yakusanya Sh12 bilioni za vibali na mikataba

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekiri kutokuwa na takwimu maalumu za ajira za kitaalamu kwa wageni zilizotangazwa baada ya kukosekana wazawa Zanzibar.

Hata hivyo, katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, Serikali kupitia kamisheni ya kazi imekusanya Sh12.468 bilioni ya vibali na mikataba.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira, Nambari 11 ya 2005 imeweka masharti ya ajira kwa wageni, ikiwa ni pamoja na kutangazwa ajira hiyo pale anapokosekana mtaalamu wa ndani kwenye eneo hilo.

Vilevile, baada ya kuajiriwa mgeni, anatakiwa amfundishe mzawa kushikilia nafasi hiyo baada ya mkataba wake wa ajira kumalizika.

Hayo yamebainishwa Barazani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma, ambapo amesema serikali ilikuwa haijalibaini hilo lakini kwasasa watakusanya takwimu hizo na katika sekta husika.

Hamza alitoa kauli hiyo leo Jumatatu, Februari 16, 2026 wakati akijibu swali la mwakilishi wa Ole, Seif Hamad Suleiman aliyetaka kujua ajira ngapi zilizotangazwa baada ya kukosekana wazawa katika kipindi cha miaka mitano.

Na kwa kuzingatia takwimu rasmi za kila mwaka kwa miaka mitano ya hivi karibuni, Serikali imepata mapato ya kiasi gani kwa kutoa vibali vya wafanyakazi kutoka nje ya nchi.

“Sheria imeweka utaratibu wa uajiri katika sekta binafsi kwa kumpa mamlaka Wakala binafsi wa ajira akiwa ni mwakilishi wa mwajiri ambaye ni sehemu ya uhusiano wa ajira katika kuajiri na kumkabidhisha muajiriwa kwa mtu au taasisi itakayotoa kazi na kusimamia utekelezaji wake,” amesema.

“Katika utekelezaji wake, hakuna twakwimu rasmi za utangazaji wa ajira hizo lakini kwa vile ni jambo muhimu wizara imelipokea na itaweka utaratibu maalumu wa uwekaji wa takwimu rasmi za utangazaji huo,” amesema Hamza.

Amesema Wizara kupitia Kamisheni ya Kazi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuratibu suala la vibali vya kazi kwa wafanyakazi na wawekezaji wanaowekeza hapa Nchini.

Amesema kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, serikali imekusanya Sh12.468 bilioni ya vibali na mikataba.

Naye Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad amesema kukosekana takwimu za ajira hizo, hatua hiyo inadhihirisha wazi kwamba serikali imeshindwa kudhibiti ajira za wazawa kwani bila kuwa na takwimu maalumu hawawezi kushughulikia changamoto iliyopo.

“Inaonesha wazi kwamba tumeshindwa kuhesabu ajira zetu, if you fail to account, you fail to control, you fail to manage, sasa inatumia utaratibu gani kudhibiti ajira hizo ambazo zimechukuliwa na wa nje wakati wazawa wapo,” amehoji.

Profesa Fakih ameishauri serikali kutumia mifumo ya kielektroniki itakayotoa taarifa kwa wakati katika ajira.

Hata hivyo, akijibu hoja hizo, Waziri Hamza amesema, “ikiwa kuna jambo halipo sawa unakiri na kulifanyia kazi, na serikali imeshakiri kwamba haina takwimu hizo ila inakwenda kulifanyia kazi…na si hilo tu tumegundua hata ajira ambazo sio za kitaalamu kuna wageni wanazifanya Zanzibar.”

“Tunapoteza nafasi nyingi kupitia ajira za wageni, na serikali imeshajipanga kuhakikisha kila eneo tunapitia kuna watu ambao ajira si wageni na wataanza kufanya operesheni,” amesema.