Nchi za Afrika Mashariki zakemea uvuvi haramu wa meli Bahari ya Hindi

Zanzibar. Nchi za Afrika Mashariki zimeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kwa uvuvi haramu unaofanywa na meli kubwa za kigeni katika Ukanda wa Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi, zikisema unanyonya rasilimali za bahari na kuhatarisha uchumi wa jamii za pwani.

Kauli hiyo imetolewa na viongozi wa serikali na taasisi za uvuvi wakati wa Mkutano wa Kikanda wa Blue Voices uliofanyika Zanzibar kwa siku tatu, Januari 26–28, chini ya Mradi wa Jahazi, uliowakutanisha wadau kutoka Tanzania na Kenya kujadili mikakati ya pamoja dhidi ya uvuvi haramu, usioripotiwa na usiodhibitiwa (IUUF).

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mboja Ramadhani Mshenga, amesema uvuvi haramu si tatizo la mazingira pekee bali ni tishio kwa usalama wa chakula, kipato cha wananchi na mamlaka ya nchi juu ya rasilimali zake.

“Uvuvi haramu unagusa maisha ya watu wetu moja kwa moja. Ni suala la chakula, kipato na kulinda mamlaka yetu juu ya bahari,” amesema.

Washiriki wameeleza kuwa changamoto kubwa ipo kwenye maeneo ya bahari ya kina kirefu ambako meli kubwa za kigeni zina uwezo mkubwa wa kuvua kuliko uwezo wa nchi nyingi za ukanda kusimamia shughuli hizo. Baadhi ya meli hizo zilihusishwa na makampuni ya Asia, ingawa mkutano ulisisitiza kuwa hoja kuu ni uwajibikaji, uwazi wa umiliki na uzingatiaji wa sheria.

Imeelezwa pia kuwa mifumo ya kisheria isiyooana na viwango tofauti vya adhabu kati ya nchi za Afrika Mashariki imekuwa mianya inayowapa nafasi wahusika wa uvuvi haramu kuhamisha shughuli zao kutoka nchi moja hadi nyingine ndani ya ukanda.

“Hatupaswi kuruhusu mtu yeyote kunyonya bahari zetu na kukimbilia nchi jirani kujificha. Ukanda wetu lazima uwe na msimamo mmoja,” amesisitiza Mshenga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi Kenya (KMFRI), Dk Paul Orina, amesema uvuvi haramu hauwezi kudhibitiwa na nchi moja pekee bila ushirikiano wa kikanda.

“Uvuvi haramu hushamiri pale kila nchi inapojaribu kujilinda peke yake. Suluhisho lake ni nchi kushirikiana kama ukanda mmoja,” amesema.

Naye Naibu Mshauri Mkuu wa Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kenya, Leonard Bett Cheruiyoti, amesema tofauti za viwango vya adhabu kati ya nchi zinaendelea kuwavutia wahusika wa uvuvi haramu kuchagua maeneo yenye sheria dhaifu.

“Adhabu zinapokuwa ndogo katika nchi fulani, wahalifu huhamishia shughuli zao huko,” amesema.

Washiriki walikubaliana kuwa uvuvi haramu ni sawa na wizi wa rasilimali unaoathiri moja kwa moja jamii za pwani, kwani uvuvi ni chanzo kikuu cha chakula na kipato kwa maelfu ya wananchi Tanzania na Kenya.

Mkutano huo uliazimia kuimarisha ushirikiano wa kisheria, kuratibu mashtaka na kuboresha mifumo ya kubadilishana taarifa kati ya mamlaka za uvuvi na usalama wa baharini katika ukanda.

Akifunga mkutano, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Kapteni Hamad Bakari Hamad, amesema usimamizi wa pamoja wa rasilimali za bahari ni muhimu kwa ustawi wa uchumi na vizazi vijavyo.

“Kulinda bahari yetu kwa pamoja si kauli ya kisiasa tu, bali ni jambo la lazima kwa uchumi wetu na vizazi vijavyo,” amesema.

Mkutano huo ulihitimishwa kwa kutiwa saini makubaliano ya ushirikiano wa kikanda kati ya baadhi ya nchi zilizoshiriki, hatua inayotajwa kuwa mwanzo wa enzi mpya ya usimamizi wa pamoja wa rasilimali za Bahari ya Kusini Magharibi mwa Hindi.