Kigogo Mtibwa Sugar aachia ngazi

LICHA ya timu kufanya vizuri kwa kushika nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Aboubakar Swabri amejiuzulu nafasi yake ndani ya timu hiyo.

Mabingwa hao mara mbili wa zamani wa msimu wa mwakla 1999 na 2000, iliyorejea Ligi Kuu msimu huu kutoka Ligi ya Championship, inashika nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi 21 kupitia mechi 14 ilizocheza ikishinda tano, sare sita na kupoteza tatu, huku ikifunga mabao 12 na kufungwa 11 na kwa sasa inajiandaa na mechi za hatua ya 64 Bora ya Kombe la Shirikisho (FA).

Akizungumza na Mwanaspoti, Swabri alikiri ni kweli amechukua uamuzi wa kukaa pembeni kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wake, huku akiitakia kila la kheri timu na uongozi mpya ujao ili waweze kufikia malengo ya klabu hiyo.

“Nimefanya hivyo nikiwa na akili timamu sijashinikizwa na mtu na nimefanya timu ikiwa katika nafasi nzuri ili niondoke bila deni wanamtibwa Sugar asanteni kwa ushirikiano mzuri mlionipa kipindi chote cha uongozi wangu,” amesema Swabri.

“Hii ni timu ya wana Morogoro kila mtu ana nafasi ya kuongoza wamepita wengi na wengi wataendelea kuja kuipa sapoti, nilipofikia inatosha ndio maana nimeamua kukaa pembeni na matumaini yangu ni kuona timu inaendelea kusonga mbele zaidi.”

Wakati Swabri akigoma kuweka wazi sababu zilizomuweka nje ya timu, inaelezwa amefanya hivyo kutokana na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Morogoro kuingilia majukumu yake hasa kipindi hiki timu ikiwa inafanya vizuri.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa kiongozi huyo kimedai alipambana kuipandisha timu bila sapoti kutoka kwa viongozi wa mkoa, lakini sasa baada ya timu kurudi na kuanza kufanya vizuri watendaji wamekuwa wengi na kila mmoja anaona ana haki ya kufanya atakalo, hivyo ameamua kuwaachia.

“Sababu kubwa ni kuingiliwa katika majukumu, hakuna kitu kingine nafikiri wanataka kuitumia timu katika ishu za siasa kipindi hiki ambacho inafanya vizuri, hicho hakijampendeza Swabri ndio maana ameandika barua ya kuachia ngazi,” kilisema.

Hata hivyo, hii ni mara ya kwanza kuingia na kutoka ndani ya klabu hiyo, kwani alishafanya misimu miwili iliyopita na kurejea tena miezi ya karibuni.