Morogoro. Kuanza kutumika kwa mtaala wa kufundisha wafanyakazi wa majumbani kwenye vyuo vya ufundi stadi (Veta), kumewasaidia kutambua vyema majukumu na haki zao ikiwemo ya kupata mikataba ya ajira na mishahara inayostahili.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Februari 16, 2026 na Maria Shimba, mratibu wa mradi wa kuandaa mtaala wa ufundishaji wafanyakazi wa majumbani unaotekelezwa na Jumuiya ya Watu Wanaojitolea Ulimwenguni (CVM), kwa kushirikiana na Veta wakati wa kufunga mafunzo kwa walimu wa Veta Tanzania bara na Zanzibar yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kufundisha mtaala huo.
Shimba amesema miaka ya nyuma kulikuwa hakuna mtaala wa kufundishia wafanyakazi wa majumbani hivyo kazi hizo zilichukuliwa ni za watu wasiokuwa na elimu na wasiojua haki zao.
Amesema mwaka 2022 CVM kwa kushirikiana na wadau wakiwemo Veta waliandaa mtaala ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2024 ambapo mpaka Februari 2026 jumla ya wafanyakazi wa majumbani 1,280 wamehitimu kwenye vyuo mbalimbali.
“Mwanzoni Veta hawakuwa na mtaala wa kufundishia wafanyakazi wa majumbani lakini sasa hivi wamepata mtaala na wameweza kufundisha wafanyakazi hao kuhusu majukumu yao wanapokuwa kazini pamoja na haki zao, ikiwemo kupewa mkataba ya ajira na kupewa likizo.”
“Tulipokabidhi mtaala huu tulifanya majaribio kwenye vyuo vitatu vya Veta ambavyo ni Dodoma, Mikumi na mkokotoni na tulitoa mafunzo kwa walimu 18 wa Veta ambapo 12 walitokea Tanzania bara na sita waliitokea Zanzibar.”
Amesema kupitia mtaala huo zipo kozi za mwezi mmoja, miezi mitatu na miezi sita ambapo mbali ya kufundishwa masuala ya mapishi, usafi na kazi nyingine za nyumbani lakini pia wafanyakazi wa majumbani watafundishwa namna ya kutoa huduma kwa watoto na wazee.
Mratibu huyo ameiomba Veta kuendelea kutekeleza mtaala huo na kutangaza nafasi za masomo hayo ili waweze kupatikana wafanyakazi wa majumbani mahiri, wenye weledi na watakaoweza kufanya kazi ndani na nje ya nchi.
Awali, akifunga mafunzo ya walimu hao wa Veta, Mkurugenzi wa elimu na mafunzo stadi Veta, Dk Abdallah Ngudo amesema kazi za majumbani sio tu kupikia na kufanya usafi bali ni kazi inayohitaji ujuzi na maarifa ambayo yanaoatikana darasani.
Amesema kabla ya kuandaa kwa mtaala huo Veta kwa kushirikiana na wadau wengine ilifanya utafiti wa mahitaji ya soko la ajira kwa wafanyakazi wa majumbani ambapo walibaini kumekuwa na mahitaji makubwa ya wafanyakazi wa majumbani ndani na nje ya nchi, zikiwemo za Kiarabu.
Akitoa taarifa yake, Mwakilishi mkazi wa CVM Tanzania, Laura Vallesi amesema baada ya kukamilika kwa mtaala huo pia mradi uliwajengea uwezo walimu wanaofundisha kwenye vyuo vya Veta Tanzania bara na VTA Zanzibar.