Wananchi 3,498 wa Kijiji cha Ghona wasogezewa huduma za afya

Moshi. Wananchi wa kijiji cha Ghona, kata ya Kahe Mashariki, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, wameishukuru Serikali kwa kuwajengea zahanati katika kijiji chao iliyogharimu zaidi ya Sh110 milioni.

Wamesema kukamilika kwa zahanati hiyo itakayohudumia wananchi 3,498 kutawapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika maeneo ya jirani.

Awali, wananchi hao walikuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya, hali iliyokuwa ikiwagharimu fedha nyingi pamoja na kusababisha wagonjwa kuchelewa kupata huduma za haraka kutokana na umbali.

Wakizungumza leo Februari 16, 2026 wananchi hao wamesema kukamilika kwa zahanati hiyo kutawapunguzia gharama za usafiri kwani baadhi yao walikuwa wakishindwa kusafiri kufuata huduma za afya kutokana na gharama.

Ernesta Joachim, mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, amesema juhudi zilizofanywa na Serikali ya kuwasogezea huduma za afya karibu, itawasaidia kupunguza changamoto za usafiri pamoja na kusafiri umbali mrefu.

Mganga mkuu wa Wilaya ya Moshi, Dk Juma Mombokaleo akisoma taarifa ya ujenzi wa zahanati ya Ghona iliyojengwa katika Kijiji cha Ghona, Kahe Mashariki, Wilaya ya Moshi. Picha na Janeth Joseph



“Hapa kwetu ilikuwa ukiumwa unawaza utatokaje kwenda kutafuta huduma za matibabu, kwa sababu tulikokuwa tunafuata huduma ni mbali sana, yaani mwananchi wa chini kama sisi ukiumwa unakufa maana huna fedha ya usafiri,” amesema.

Mwananchi mwingine wa kijiji hicho, Yohan Mtweve ameishukuru Serikali kwa kuwajengea zahanati katika Kijiji hicho, ambapo itawarahisishia kupata huduma za matibabu kwa karibu na hata kupunguza vifo vilivyokuwa vikitokana na ucheleweshwaji wa huduma za afya.

“Awali  ilikuwa mtu unasafiri umbali mrefu zaidi ya kilomita 20 kwenda kutafuta huduma za matibabu,” amesema Mtweve.

Akizungumzia ujenzi wa zahanati hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amesema kuwa Serikali itaendelea kusogeza huduma za afya karibu na maeneo ya wananchi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo muhimu.

“Nawapongeza sana wananchi wa Ghona kwa kuanza wenyewe kuona umuhimu wa kuwa na huduma za afya karibu. Serikali imekuja kuwaunga mkono na kuendeleza juhudi zenu,” amesema DC Mnzava.

Aidha, DC Mnzava ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo kutaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa kijiji hicho, ikiwemo kupunguza umbali wa kufuata matibabu, gharama za usafiri, pamoja na kuboresha huduma za afya kwa ujumla.

Naye, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Juma Mombokaleo, amesema ujenzi wa mradi wa zahanati hiyo ulianza mwaka 2017 na ulikamilika mwishoni mwa mwaka 2025 na tayari imeanza kutoa huduma kwa wananchi.

“Utekelezaji wa mradi huu ulianza 2017 kwa nguvu za wananchi ambapo walijichanga Sh50 milioni na baadaye Serikali katika bajeti ya mwaka 2023/24 ikatoa Sh60 milioni kwa hatua za ukamilishaji,” amesema Dk Mombokaleo.