Tabora. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ni endelevu, ukiwa na lengo la kuboresha huduma na kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Miongoni mwa ahadi hizo ni pamoja na kuboresha na kupanua huduma ya bima ya afya, kuhakikisha maiti hazizuiliwi hospitalini kwa sababu ya kushindwa kulipia gharama za matibabu, kutoa ajira 12,000 kwa kada za afya na elimu, pamoja na kutenga Sh200 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia.
Hayo yamebainisha leo Jumatatu Februari 16, 2026 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi wakati akizungumza na WanaCCM shina namba 2 la Puge Jimbo la Nzega Vijijini katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Tabora.
Kihongosi amewataka Watanzania kutobabaishwa na maneno ya mitandaoni au wanaobeza kazi kubwa iliyofanywa kuhusu utekelezaji wa ahadi mbalimbali zenye lengo la kutatua kero za wananchi nchini.
“CCM ndio msingi wa maendeleo, mwaka 2025 mgombea urais wa CCM ( Samia), aliahidi katika ilani nini kinakwenda kufanyika na katika siku 100 alieleza nini atakifanya. Ndani ya siku 100 kazi imefanyika kwa kasi kubwa,” amesema Kihongosi.
Kwa mujibu wa Kihongosi, Rais Samia ametekeleza ahadi ya kutozuiwa maiti hospitalini akisema jambo hilo linatekelezwa na hakuna mwananchi anayezuiwa mwili wake hata kama anadaiwa.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Nkinga jimbo la Manonga wilayani Igunga mkoani Tabora.
“Aliahidi mpango wa bima ya afya bure kwa wote, muda ukifika mkishirikishwa twendeni tukajiandikishe ili kupunguza gharama za matibabu. Pia Samia aliahidi Sh200 bilioni ambazo zitasambazwa nchi nzima kuwasaidia vijana kwa utaratibu utakaotolewa na Serikali,” amesema Kihongosi.
Mwenezi huyo, amesema yapo mambo mengi mazuri hadi kufikia 2030 kila kitongoji kitakuwa na umeme, hivyo wanaobeza wanajihangaisha.
” WanaCCM na wananchi naomba mtambue nchi hii ndio urithi pekee tulioachiwa, tusikubali Tanzania ikavurugwa, tuilinde kwa wivu mkubwa hapa ndio nyumbani kwetu,” amesema.
Akiwa wilayani Igunga, Kihongosi amepokea kero saba zikiwemo za barabara na wanyama pori zilizotolewa katika mkutano wa hadhara, wakitaka zipatiwe ufumbuzi wa haraka.
Mbali na barabara na uvamizi wa wanyama pori, wananchi hao pia walitaja changamoto za upatikanaji wa umeme, maji, huduma za afya, elimu na miundombinu ya stendi ya mabasi ya Nkinga.
Kero hizo ziliwasilishwa jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Gulioni, Nkinga, Jimbo la Manonga wilayani Igunga.
Mkazi wa Mwamala, Lusinde Masunga, alisema wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na ukosefu wa zahanati pamoja na huduma za vivuko, licha ya kuwapo mito miwili inayokatiza katika kijiji hicho.
“Wananchi tunahangaika na wanyama pori wanaoharibu mazao yetu. Pia, barabara za Kata ya Mwamala ni mbovu. Tunaomba Serikali itusaidie kwa sababu kero hizi zinatuumiza sana,” alisema Masunga.
Mkazi mwingine wa Igunga, George Maige, aliibua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika baadhi ya kata, akiiomba Serikali kuingilia kati.
Kwa upande wake, mkazi wa Kata ya Ndembezi, Emmanuel Michael, aliiomba Serikali kujenga upya Shule ya Msingi Charles Kabeho, akisema madarasa yake ni chakavu na baadhi ya kuta zimetoboka, hali inayohatarisha usalama wa wanafunzi na walimu.
Aliongeza kuwa shule hiyo pia inakabiliwa na upungufu wa madawati, jambo linalowalazimu wanafunzi kukaa chini, hali inayodhoofisha usikivu darasani na kuathiri ujifunzaji.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Nkinga jimbo la Manonga wilayani Igunga mkoani Tabora.
“Walimu na wanafunzi wapo hatarini. Mvua ikiongezeka, ukuta unaweza kuanguka na kusababisha madhara makubwa,” alisisitiza.
Akijibu kero ya barabara, Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) Igunga, Solomon Hamis, alisema changamoto hiyo inafahamika na ipo kwenye mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, ikiwemo ujenzi wa madaraja.
Kuhusu zahanati, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Lucia Kafumu, alisema Mwamala tayari kuna zahanati iliyojengwa, lakini katika kijiji cha Ngunga kuna boma la zahanati lililojengwa kwa nguvu za wananchi ambalo halijakamilika. Aliahidi kuwa katika mwaka ujao wa fedha wataliangalia suala hilo.
Baada ya majibu hayo, Kihongosi aliutaka uongozi wa halmashauri kuweka mikakati ya haraka, ikiwemo kutumia mapato ya ndani kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo ili wananchi waanze kupata huduma.
Kuhusu uvamizi wa tembo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga, Joseph Mafuru, alikiri uwepo wa tatizo hilo, hasa katika kata ambazo wanyama hao hupita mara kwa mara.
Alisema halmashauri imekuwa ikiendesha doria kwa kushirikiana na maofisa wanyama pori na wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili ili kuwafukuza tembo wanaoingia kwenye makazi ya watu.
Hata hivyo, Kihongosi aliahidi kulifuatilia kwa karibu suala hilo pamoja na changamoto ya maji kwa kuwasiliana na mawaziri wa sekta husika.
Alimpongeza meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) kwa kusimamia mradi wa maji wa Sh2 bilioni utakaonufaisha vijiji tisa vya Igunga na wananchi takribani 32,000.
“Kuhusu barabara nimepita nimeona hali ilivyo. Itafanyiwa kazi, pamoja na stendi. Maendeleo ni hatua, hakuna anayeweza kumaliza changamoto zote kwa wakati mmoja,” alisema Kihongosi.
Aidha, aliwataka watendaji wa Serikali waliopokea kero hizo kuzifanyia kazi kwa ufanisi na kuhakikisha wananchi wanatendewa haki, akiahidi kufuatilia utekelezaji wake.