Dar es Salaam. Shahidi wa nane katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amejitambulisha mahakamani kuwa ni mwanachama wa Chadema, lakini akasema hamtambui Lissu kama mwenyekiti wake bali kama mshtakiwa katika kesi hiyo.
Aidha, shahidi huyo alidai kuwa Lissu amemsababishia matatizo, jambo lililomfanya Lissu kumuomba radhi mahakamani.
Shahidi huyo ni miongoni mwa mashahidi fiche wa Jamhuri waliowekewa ulinzi maalumu, wasiopaswa kuonekana wala kutambulika hadharani.
Hutoa ushahidi wakiwa ndani ya kizimba maalumu ambacho hakiwaruhusu kuonekana na wasikilizaji wala mshtakiwa, isipokuwa majaji pekee. Ametambulishwa mahakamani kwa jina la P8 (miaka 26).
Katika ushahidi wake wa awali, alijitambulisha kuwa mwanachama wa Chadema, lakini akamkana Tundu Lissu kuwa si kiongozi wake.
Aidha, alimlaumu kwa kumletea majanga wakati wa mahojiano, ambapo Lissu alimhoji kwa maswali ya dodoso kuhusu ushahidi alioutoa mahakamani.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Kwa mujibu wa shahidi wake leo Jumatatu, Februari 16, 2026 akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, amesema anaishi Moshi, Njoro mkoani Kilimanjaro ni mfanyabiashara wa matunda, katika soko la Manyema lililopo Mbuyuni, Moshi Mjini.
“Najishughulisha na siasa lakini sio kwa undani sana kupitia Chadema ambacho ni mwanachama wake na anamfahamu Tundu Lissu kuwa ni Mwenyekiti Taifa wa Chadema.
Aprili 4, 2025 alikuwa katika shughuli zake kwa kutumia simu yake janja aina ya Oppo F1X aliingia katika mitandao ya kijamii na katika mtandao wa Youtube kwenye Jambo TV alikutana na tamko la Tundu Lissu ambaye kwa sasa ni mshtakiwa.
Katika tamko hilo Lissu alikuwa akiwahamasisha vijana wake kuwa lazima wafanye uasi dhidi ya Serikali na watakinukisha na watazuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kama Serikali haitafanya mabadiliko kwa kauli kuwa “no reforms, no election”.
Kutokana na kauli hiyo kama mwanachama, alipata hamasa kwa kukumbuka kipindi cha uchaguzi serikali za mitaa mwaka 2024, viongozi wao wa mitaa walikatwa na kupewa CCM, kitu ambacho kilimuuma sana.
Hivyo aliamua kuhamasisha vijana wenzake wa mtaani wakati wakisubiria kauli Lissu waanze kukinukisha mtaani.
Aprili 8, 2025 akiwa katika harakati za kuhamasisha vijana eneo la Njoro ya Pepsi, ghafla alikamatwa na askari polisi huku wenzake wakikimbia.
Alipelekwa ofisi za Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) mkoani Kilimanjaro, akakabidhiwa kwa askari Rashid ambaye alimuuliza baadhi ya maswali na kutokana na woga aliamua kusema ukweli.
Alimueleza Afande Rashid kuwa alikuwa anahamasisha vijana wafanye uasi dhidi ya Serikali kumuunga mkono mwenyekiti wao kuhusu kauli yake aliyoitoa ya no reforms no election.
Baada ya mahojiano hayo aliingizwa mahabusu lakini saa 11 jioni aliachiwa kwa dhamana ambapo alijidhamini mwenyewe kwa sharti la kuripoti Polisi kila Jumatatu.
Aliripoti polisi mara ya kwanza Aprili 14, 2025, akatakiwa kuripoti tena Aprili 22, 2025, ambapo alichukuliwa maelezo na askari Michael.
Baada ya kuhitimisha ushahidi wake huo ndipo mshtakiwa Lissu akaanza kumhoji maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wale huo na hali ilikuwa kama hivi:
Lissu: Shahidi, tarehe 22 uliandika maelezo polisi?
Lissu: Ukioneshwa utayatambua?
Shahidi: Hilo ni suala la mawakili maana ndio wana maamuzi wanioneshe au wasinioneshe.
Lissu: Mimi nakuuliza kama ukioneshwa utayatambua?
Shahidi: Mawakili wao ndio wana uamuzi.
Lissu: Shahidi, sasa unabishana na mwenyekiti wako?
Shahidi: Wewe ni mshtakiwa (jibu hilo linawafanya wasikilizaji kuangua kicheko)
Lissu: Sasa mimi kama mshtakiwa na wewe kama shahidi, sasa naomba ujibu maswali yangu, ukioneshwa maelezo yako hayo utayatambua?
Shahidi: Kama nilivyosema mawakili wa Serikali ndio wanaweza kuamua kunionesha au kutonionesha.
Mwendesha mashtaka, Wakili Katuga: Shahidi, sikiliza mshtakiwa anavyokuuliza wewe mjibu tu kama anavyokuuliza, anakuliza kama ukioneshwa unaweza kuyatambua, kwa hiyo ni rahisi tu.
Lissu anamuuliza tena swali hilo.
Shahidi: Naweza kuyatambua nikioneshwa.
Baada ya kupewa na kukiri kuwa ndio maelezo yake na Lissu akamuuliza kama anaweza kuyatoa mahakama iyapokee kama kielelezo cha upande wake Lissu, shahidi amekubali na upande wa mashtaka ukaieleza mahakama kuwa hauna pingamizi.
Hivyo, mahakama imeyapokea na kuyasajili kama kielelezo cha saba cha upande wa utetezi (D7) kisha Lissu akaanza kumuhoji maswali mbalimbali alitumia maelezo hayo pamoja na maswali mengine nje ya maelezo hayo ya onyo.
Lissu: Umesema sana hapa mahakamani kuwa mwenyekiti alisema atakinukisha maana yake ni nini?
Shahidi: Wewe ulisema utakinukisha.
Lissu:- Unafahamu kwa Kiswahili kukinukisha?
Shahidi: Mimi nafahamu kukinukisha, hivyo vingine sijui.
Lissu: Ulisema kuwa mambo yaliyokupa hamasa kuwashawishi vijana ni pamoja na wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 viongozi wako walikatwa kugombea.
Lissu:- Kwa hiyo hasira zako ni kutokana na wizi wa kura za uchaguzi?
Shahidi: Hayo ni maoni yako, twende kwenye pointi.
Lissu: Ulisema mlikuwa mnasubiri kauli ya mwenyekiti ya kukinukisha, kuanzia siku hiyo ya Aprili 4, 2025 hadi sasa, kauli hiyo ya kukinukisha ilifanyika au haijafanyika?
Shahidi: Sasa si tayari umekuwa mshtakiwa.
Lissu: Sasa shahidi baada ya kusubiri kauli yangu ya kukinukisha, wewe ukaamua kujiongeza kwa kuhamasisha vijana kufanya uasi?.
Lissu: Sawa shahidi, ngoja nimalizie maswali machache, wewe ni kijana wangu sitaki kukuchosha na maswali mengi.
Shahidi: Mimi sio mwanachama wako wewe mshtakiwa.
Shahidi: Kwa sababu umeniingiza katika hatia, sikutarajia kama nitafikishwa sehemu kama hii.
Lissu: Samahani bana kama nimekuleta kwenye majanga haya.
Shahidi: Wewe kwa mtazamo wako unaona haya ni mazuri?
Lissu: Kuna kiongozi au mwanachama yeyote ambaye alikutishia maisha kuhusiana na kesi hii?
Shahidi: Sijatishiwa, ila nimesikia kwenye mitandao taarifa kuwa mtu atakayetoa ushahidi kwenye kesi ya mwenyekiti wetu Tundu Lissu, tutasalimiana naye.
Lissu: Nani aliyesema hayo, huyo mtu hana jina?
Shahidi: Siwezi kumtaja jina kwa sababu ya usalama wangu lakini tu huyo ni mwanaume.
Shahidi: Nilienda kwa afande Rashidi akasema nisijali, nitakuwa salama.
Lissu: Kwa nini hukutoa taarifa Polisi?
Shahidi: Kwa sababu hawanijui, na watu hao hawajawahi kunijua.
Lissu: Nitakuwa sahihi nikisema kuwa ulifutiwa kesi ile ya uasi ili uje utoe ushahidi kwenye kesi ya Lissu?
Shahidi: Hautakuwa sahihi.
Lissu: Kwa kosa ulilokuwa nalo la kuhamasisha uasi, kwa nini hukufunguliwa kesi mahakamani?
Shahidi: Kwanza naishukuru Serikali, kwa kweli Serikali achana nayo kabisa. Ningekataa kusema ukweli Serikali ina mkono mrefu ingenikamata tu ila ukweli unamuweka mtu huru.
Siku ile nilipokamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi, kweli nilieleza ukweli na siamini mpaka sasa kama bado nipo huru hadi muda huu.
Amejibu shahidi huyo na kusababisha ukumbi mzima wa Mahakama kulipuka kwa vicheko na minong’ono kwa sekunde kadhaa hadi Jaji Ndunguru alipowataka watu watulie.
Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho.