Waziri Mkuu aeleza manufaa na fursa za kijografia nchini

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali inatambua ushindani uliopo katika ukanda wa bahari ya hindi, hivyo tayari hatua zimeanza kuchukuliwa Tanzania inufaike na fursa za kijografia zilizopo.

Hatua mojawapo aliyoitaja Dk Mwigulu, ni uboreshaji wa bandari ya Tanga uliofanyika kwa awamu ya kwanza huku akisema awamu ya pili ni matarajio ya ukarabati wa gati namba moja na mbili wenye urefu wa mita 300.

Mtendaji mkuu huyo wa Serikali ametoa kauli hiyo leo Februari 16, 2026 wakati akikagua shughuli za bandari ya Tanga.

 “Tunatarajia kuendelea na maboresho ya miundombinu ambayo tumeonyeshwa lengo ni kuongeza ufanisi ili meli kupishana kwa idadi yeyote inayoweza kuja na kuhudumiwa kwa haraka bila kusubiri kwa muda mwingi,” amesema.

Waziri Mkuu akizungumzia uchache wa vifaa vya kushusha mizigo, amemuagiza Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile kulifanyia kazi kwani changamoto hiyo huleta kero kwa watumiaji wa bandari hiyo.

Amesema ufinyu wa eneo la bandari unaochochea msongamano wa mizigo, waziri wa uchukuzi anapaswa kufanyia kazi kupatikane eneo la kutosha kuepusha msongamano wa mizigo.

Dk Mwigulu ameeleza kuwa, ana taarifa Bandari ya Tanga ina eneo dogo, wameshaomba kuongezewa eneo nje ya gati namba mbili kwa ajili ya utanuzi wa bandari awamu ya pili, na mchakato umeshafikishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Amesema jambo hilo linalohusu uzalishaji ni vyema uamuzi ufanyike haraka ili hatua zinazohitajika zifanyike haraka, akisisitiza suala la kuongeza eneo halipaswi kuchukua muda hivyo ni vyema wizara hizo mbili kukaa na kuyafanyia kazi haraka.

“Waziri wa Uchukuzi (David Kihenzile) kaeni na wenzenu wa ardhi, haya mambo yanayohusu uzalishaji hayapaswi kusubiri, haya ni mambo ya uamuzi ufanyike eneo lipatikane ili hatua zinazotakiwa zifanyike,” amesema.

Dk Mwigulu katika hatua nyingine, ametaja mlolongo wa kero alizopokea katika bandari hiyo ikiwemo uchache wa watumishi, watumishi wanaoumia kazini kutolipwa stahiki zao kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

“Pia kuna ucheleweshaji wa malipo ya watumishi wa kutwa, vibarua kutolipwa kwa wakati Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imeshalipa fedha zao, uchache wa vifaa vya kupakulia, ufinyu wa eneo la bandari, uwepo wa majengo ya watu karibu na bandari  na uchache wa redio mawimbi (radio call),” amesema.

Dk Mwigulu amesema suala la ucheleweshaji wa malipo kwa vibarua licha ya TPA kulipa kwa wakati, mamlaka hiyo yenyewe ihakikishe fedha zinafika moja kwa moja kwa wahusika.

Amesema kama watu wanaowasimamia vibarua wanachelewesha kwa nini wasilipwe moja kwa moja wahusika.

“Angalieni utaratibu ambao hatutachelewesha malipo haya, tuna watu ili waonekane ni wa maana inabidi acheleweshe kufanya uamuzi, afuatwe fuatwe aonekane ndio mkubwa haya ni mambo ya kishamba na ni mambo ya zamani,” amesema.

Akizungumzia suala la masilahi kwa wafanyakazi, Dk Mwigulu amesema Rais Samia ameshapitisha uamuzi na sheria ya fedha imekwisha pitishwa na imekuwepo mijadala baina ya Serikali na sekta ya umma.

“Niwaelekeze bandari kuharakisha majadiliano wanayofanya na sekta binafsi na sekta ya umma ili ndugu zetu wanufaike na ongezeko hili la kima cha chini, ongeeni na ndugu zetu hatua mnazofanya kama uwezo hauruhusu hata hapana ni jibu,” amesema.

Dk Mwigulu alimuagiza Mkurugenzi wa bandari kukaa na taasisi zilizoingia mkataba na wafanyakazi hao kukubaliana kuanza utekelezaji wa viwango vya mshahara kama ilivyo maeneo mengine.

Agizo hilo la Dk Mwigulu limekuja  baada ya Mbunge wa Tanga, Kassimu Mbaraka kuwasilisha ombi kwa mtendaji mkuu huyo wa Serikali juu ya uwepo wa vibarua waliofanya kazi kwa muda mrefu kutoongezewa malipo, licha ya Serikali kuelekeza kima cha chini cha mishahara.

Amesema vibarua hao kwa siku wanalipwa Sh11,000 hivyo Serikali inapaswa kuangalia jambo hilo wafanyakazi wapate haki stahiki.

“Tunaomba sasa kima hiki sasa kiendane na agizo la Serikali, kampuni zilizochukua tenda ya kuajiri vibarua ni wakati sasa tuone mabadiliko katika mishahara na ujira wa vijana hawa,” amesema.

Hoja hiyo iliungwa mkono pia na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma akisema  mafanikio ya bandari ya Tanga hayaji na manufaa ya Jimbo la Tanga mjini pekee bali kwa mkoa mzima.

“Tunaomba kuongezewa gati lingine ili bandari hii iongeze uwezo wa kufanya kazi, pia wafanyakazi wa bandari hii waangaliwe masilahi yao, kwa zaidi ya miaka 10 hawajaongezewa, ilihali bandari zingine wameongezewa,” amesema.

Akizungumzia hitaji la maboresho ya bandari ya Tanga, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema kumekuwa na ongezeko la ajira kutoka 6,000 hadi 17,000.

“Tumeona tija kubwa inayosababisha tuombe gati la pili, tumepewa na jitihada zimeanza kuongeza gati la pili, pia tumeelemewa na majahazi, tuna biashara kubwa ya mazao kwenda Zanzibar na vifaa vya ujenzi.

“Tunaomba mchakato wa kujenga bandari kwa ajili ya majahazi uanze kupisha meli kubwa zinazokuja kwa siku, zifanye kazi kwa tija kubwa,” amesema.

 Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema uwekezaji mkubwa unaofanyika wa bandari hauwezi kuwa na ufanisi kama mizigo itapokelewa na kuwekwa bandarini hapo badala yake kupokelewa na kuondolewa.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema bandari ya Tanga ndio isaidie kuondoa msongamano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam.

Amesema mwaka 2021 meli zilizohudumiwa na bandari zote nchini zilikuwa 4,241 na kutokana na jitihada zilizofanyika idadi hiyo iliongezeka na kufikia 4,888.