Serikali yaondoa dirisha la kusubiri wanufaika wa bima ya afya

Dar es Salaam. Serikali imesema wananchi wasio na uwezo wanaosajiliwa katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote wataanza kupata huduma ndani ya siku saba hadi 14 baada ya kukamilisha taratibu, huku wakilipiwa na Serikali bila dirisha la kusubiri.

Akizungumza leo Jumatatu, Februari 16, 2026, Mratibu wa Bima ya Afya kwa Wote, Saidi Makora, amesema muda huo ni mchakato wa kiutendaji (business process), lakini endapo usajili na uanzishaji wa kadi vitakamilika mapema, mnufaika anaweza kuanza kupata huduma siku hiyohiyo au kesho yake.

“Kwa mujibu wa sheria, wale wote wanaolipiwa na Serikali hawana dirisha la kusubiri. Akikamilisha usajili, anaanza kupata huduma mara moja,” amesema.

Hata hivyo, Makora ameeleza kuwa kwa wananchi watakaojisajili na kulipia wenyewe katika awamu ya pili, watasubiri kwa siku 30 kabla ya kuanza kupata huduma, kama kanuni zinavyoelekeza.

Moja ya kaya mkoani Geita wakiwa wanafurahia kadi ya Bima ya Afya kwenye mpango wa kaya zisizo na uwezo, ambapo Serikali inawalipia.



Amesema kundi la kwanza la wanufaika lilianza kupata huduma Januari 26, siku ambayo zoezi la usajili lilianza kutekelezwa rasmi. “Wanaendelea kwenda kwenye vituo vya afya wakiwa na kadi zao na wanahudumiwa kwa mujibu wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote,” amesema.

Usajili wa walengwa milioni 1.4

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, jumla ya kaya 276,002 wakazi wake wanatarajiwa kusajiliwa katika hatua ya sasa, wakiwemo watoto yatima 267 na wazee 335 kutoka katika vituo vinavyomilikiwa na Serikali nchi nzima.

Meneja Uhusiano kwa Umma wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), James Mlowe, amesema zoezi la kuwasajili walengwa 1,400,000 linaendelea nchi nzima, huku timu zikisambazwa katika mikoa yenye idadi kubwa ya watu ili kuongeza kasi.

“Hadi sasa tunaendelea na usajili, na mwisho wa wiki tutaweka ripoti kubaini ni wangapi wamefikiwa kati ya walengwa wote,” amesema.

Hata hivyo, Mlowe amekiri kuwa baadhi ya zahanati bado hazina mifumo inayoweza kumtambua mgonjwa mara anapofika kupata huduma, jambo linalohitaji maboresho kabla ya kuingiza idadi kubwa zaidi ya wanachama.

“Kimsingi fedha zao zipo tayari. Tunachofanya sasa ni kuhakikisha mifumo inakwenda sambamba ili kuepusha changamoto za madai au malalamiko pale wanapoanza kupata huduma,” amesema.

Moja ya kaya mkoani Shinyanga wakionyesha Bima za Afya kwa Wote.



Ameongeza kuwa baada ya uzinduzi wa awamu ya pili, Serikali itapitia mapungufu ya mifumo katika vituo vya afya ili kuyafanyia kazi kabla ya kupanua usajili kwa kundi kubwa zaidi.

“Hatupendi kuingiza watu wengi halafu wakaanza kupata matatizo na kelele zikawa nyingi. Tunataka waingie wakianza kupata huduma kwa ufanisi, ndipo tuendelee na hatua inayofuata,” amesema.

Serikali kuunganisha mifumo

Kuhusu mifumo ya TEHAMA, Makora amesema ipo lakini imegawanyika katika makundi manne tofauti.

Ametaja mfumo wa usajili wa wanachama unaojumuisha taarifa za biometria, uhamiaji na vyeti vya kuzaliwa; mfumo wa madai unaowezesha vituo kudai fedha kwa huduma walizotoa; mfumo wa ukusanyaji wa takwimu na udhibiti wa huduma kwa mgonjwa kuanzia anapoingia hadi anatoka; pamoja na mfumo wa usimamizi wa dawa.

“Mifumo yote ipo na inafanya kazi, lakini kila mmoja umesimama peke yake. Haikuwa rahisi kusafirisha taarifa au picha za vipimo kutoka hospitali moja hadi nyingine,” amesema.

Amesema Serikali iko katika kipindi cha mpito kuandaa mfumo mmoja jumuishi utakaoziwezesha taasisi zote kusomana na kubadilishana taarifa. Kupitia mfumo huo, rufaa za vipimo, picha au dawa zitaweza kufanyika kidijitali kutoka kituo kimoja hadi kingine bila kumlazimu mgonjwa kusafirishwa.

“Kwa mfano, mgonjwa akienda zahanati ya Kantaramba na kuhitaji rufaa ya kipimo au tiba ya juu zaidi, taarifa zake zitaweza kuhamishwa hadi hospitali ya rufaa bila kumsafirisha kwanza,” amesema, akiongeza kuwa mfumo huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita.

Moja ya kaya ya jamii ya Wamasai iliyopo Mkoa wa Pwani, ikiwa imekamilisha usajili wa bima ya afya kwa wote.



Kwa mujibu wake, hatua hiyo itapunguza gharama, kuongeza uwazi na kudhibiti upotevu wa dawa na mianya mingine ya ubadhirifu.

Akizungumza na Mwananchi jana, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema kufunguliwa kwa dirisha la pili kutategemea kukamilika kwa mifumo.

Akitoa maagizo katika kikao chake na wahariri na waandishi wa habari Februari 2 mwaka huu, Mchengerwa alitoa onyo kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na watoa huduma dhidi ya wizi, ulaghai na ubadhirifu wa fedha za bima ya afya kwa wote, huku akivipa rungu vyombo vya habari.

Mchengerwa alisema wakati nchi ikiingia katika mfumo wa bima ya afya kwa wote, ndani ya mfumo huo tunakabiliwa na maadui wawili; akitaja ugonjwa na mifumo. Ili kufanikisha mifumo hiyo, amevitaka vyombo vya habari kuibua changamoto za kimifumo kupitia kalamu zao kwa uandishi wa habari za kiuchunguzi.

“Sitakubali chini ya uongozi wangu NHIF ichezewe. Kwenye hili niko tayari kuchukiwa na watu, na katika hili tunaomba waandishi wa habari mtubainishie haya mapungufu kupitia kalamu zenu kwa sababu tumedhamiria kuboresha sekta ya afya,” alisema.

Alisema NHIF kuchelewa kulipa madai kwa sababu ya ulaghai, wizi na utapeli kupitia mifumo ni mambo aliyoyataka yakamulikwe, akisema hayupo tayari wakati wake kuona mifumo ikiyumba.

“Ulaghai ukiachwa, fedha zinaanza kutoka na kupotea. Wahudumu wasiwafanye wananchi wakaikatia tamaa bima na wagonjwa wanarudi kwenye hofu ya gharama; mwisho, imani ya wananchi itaondoka,” alisisitiza na kuongeza;

“Hata sera itakuwa ngumu kutekelezeka. Ulaghai si wizi wa fedha pekee, ni wizi wa huduma. Msimamo wa Serikali ni kulinda mifumo na kulinda wanaofichua maovu. Tutaongeza nguvu kwenye malipo ya madai, tutakagua nyayo za miamala ili kudhibiti, na tutagundua mapema kwa ukaguzi wa ndani, tukishirikiana na vyombo vya uchunguzi.”