Sh588 milioni zakamilisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari wilayani Ludewa

Njombe. Zaidi ya Sh588 milioni zimetumika kukamilisha ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Chief Dastan Masasi, iliyopo Kata ya Masasi, wilayani Ludewa mkoani Njombe.

Akizungumza leo Jumatatu, Februari 16, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ludewa ya kukagua mradi huo, amesema ujenzi wa shule hiyo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuboresha sekta ya elimu, hususan katika maeneo ya pembezoni.

Amesema Serikali imetoa Sh583 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo, akiishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha hizo zilizosaidia kukamilika kwa mradi huo.

Thomas amesema tayari wanafunzi wa kidato cha kwanza wamepokelewa na wameanza masomo kwa mwaka huu wa masomo, huku akieleza matarajio makubwa ya kufanya vizuri kitaaluma na kufaulu mitihani yao.

Amebainisha kuwa ubora wa majengo na miundombinu iliyojengwa unaakisi thamani ya fedha zilizotolewa na kwamba walimu wa masomo yote wanapatikana na wapo tayari kuanza safari ya taaluma pamoja na wanafunzi hao.

Awali, Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Ludewa, Mikael Hadu, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, amesema ujenzi umekamilika kwa asilimia 100 na masomo yameanza rasmi.

Hadu amesema kiasi cha Sh583 milioni kilipokelewa kupitia Shule ya Sekondari Manda kama shule mama, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuweka mazingira salama kwa wanafunzi, hasa wa kike waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata elimu.

Amesema mradi huo umegharamiwa kupitia Programu ya Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ludewa, Stanley Kolimba, amesema wasimamizi wa mradi huo wamefanya kazi yenye ubora unaolingana na thamani ya fedha zilizotolewa.

Amempongeza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika.