Hivi ndivyo funga inavyolinda afya

Dar es Salaam. Waislamu na Wakristo duniani wanatarajia kuanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na Kwaresma kuanzia Februari 18, 2026.

Kufunga ni ibada ya muda mrefu inayotekelezwa na wafuasi wa dini mbalimbali pamoja na makundi mengine ya kijamii. Sababu za kufunga hutofautiana; baadhi hufuata mafundisho ya dini zao, huku wengine wakizingatia ushauri wa kitabibu.

Kwa kawaida, wafungaji hujizuia kula kwa takriban saa 14, kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 12:30 jioni. Wataalamu wa afya wanasema kuwa iwapo kufunga kutazingatia kanuni sahihi za lishe na unywaji wa maji, kunaweza kuwa na manufaa mengi kiafya.

Hivyo, mbali na kuwa tendo la kiimani, tafiti na maelezo ya kitaalamu yanaonyesha kuwa kufunga kunaweza kusaidia kulinda na kuimarisha afya ya binadamu.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Lishe wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Janeth Mzava amesema mtu anapofunga husaidia mwili wake kupumzika na kujirekebisha.

“Kisayansi, mtu anapofunga baadhi ya michakato katika mwili husimama na kutoa nafasi kwa mwili kujirekebisha, kuondoa seli zisizohitajika na kufanya michakato ya mwili kwenda sawa,” amesema.

Pia, husaidia kurekebisha usawa wa vimeng’enya na kuimarisha ufanyaji kazi wa utumbo.

Mzava amesema hiyo inasaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa, hasa yale yasiyoambukiza kama vile kisukari, magonjwa ya moyo na saratani.

Pia amesema inasaidia kuboresha matumizi ya sukari na mafuta mwilini.

Amesema mtu anapokula chakula, sukari inayopatikana huchakatwa na kupelekwa kwenye seli kwa ajili ya kusaidia kuupa mwili nguvu.

“Kiasi cha sukari kilichozidi huhifadhiwa kwa mfumo wa mafuta na ndiyo chanzo kimojawapo cha mtu kuongezeka uzito,” amesema.

Amesema mtu anapofunga au kujizuia kula kunasaidia kupunguza uwepo wa michakato mingi ya kuhifadhi sukari ndani ya mwili.

Amesisitiza kuwa kufanya hivyo kunasaidia kuboresha uwezo wa mwili kutumia sukari vizuri na kupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari, hasa aina ya pili.

Vilevile amesema kufunga pia kunasaidia kupunguza mafuta mwilini.

Amesema mtu anapofunga huchochea mwili kutumia yale mafuta yaliyohifadhiwa kama nishati.

Mzava amesema pamoja na afya ya mwili, kufunga pia kuna mchango katika kuboresha afya ya akili kwa kusaidia kuimarisha utendaji kazi wa ubongo.

Amesema inasaidia kuboresha kumbukumbu, kuongeza umakini na hata kupunguza msongo wa mawazo kama muhusika hana changamoto nyingine.

Kuboresha nidhamu ya kula

Amesema funga husaidia kupunguza tamaa ya ulaji wa mara kwa mara, hasa vyakula vilivyo na sukari nyingi, na kuhimiza nidhamu ya chakula.

“Kuna ile tabia mtu mara anakula ubuyu, mara chipsi kidogo, mishkaki, mara karanga au biryani inapungua kwa sababu unakuwa kwenye utaratibu wa kujizuia kula,” amesema.

Kuongeza na kuimarisha kinga dhidi ya maradhi

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Binadamu, Rachel Mwinuka amesema kuwa faida kubwa inayozibeba nyingine juu ya tendo la kufunga kwa binadamu ni kuongezeka kwa kinga dhidi ya maradhi.

Dk Mwinuka amesema kinga hizo huweza kuongezeka kutokana na muhusika kuacha baadhi ya tabia ambazo alikuwa akifanya awali zikiwa hatarishi kwa afya yake.

“Katika kipindi cha mfungo, watu wengi huacha tabia za unywaji pombe na uvutaji sigara, hivyo hufanya afya yao kuimarika.”

Amesema pia katika kipindi hiki baadhi ya watu hujikuta, aidha kwa kutarajia au kutotarajia, wakila vyakula vya mchanganyiko vyenye virutubisho muhimu mwilini wanapofuturu au kula daku.

“Wengine kabla ya kufunga walikuwa hawazingatii ulaji wa lishe, lakini kwa kipindi hicho wengi wao hujitahidi kula vyakula vya lishe ambavyo hupelekea kinga zao kupanda,” amesema.

Vyakula vipi vinafaa kufungulia?

Mlo wa futari ni ule ambao mfungaji anautumia ili kufungua kinywa mara tu jua linapozama. Mtaalamu wa Lishe, Daudi Gambo amesema ni vyema mtu kufungua kwa kula vyakula vya moto, vyepesi ambavyo vitasagika tumboni kwa urahisi na vyenye glukosi, kwa kuwa mtu amekaa muda mrefu bila kula chakula.

Dk Gambo amesema mtu anapokuwa katika mfungo, kiwango chake cha sukari mwilini hupungua, hivyo hutakiwa kukirejesha kwa kula vyakula vitakavyosaidia kurejesha kiwango cha sukari kilichopotea.

“Pia, wakati anapokuwa amefunga, utumbo unapokuwa unatafuta chakula na kukikosa husinyaa. Hivyo ni vyema wakati wa kufungua kuanza na aina ya chakula au kinywaji cha moto na chenye glukosi ambacho kitasaidia kusisimua vimeng’enya na kuuweka utumbo tayari kwa ajili ya mmeng’enyo wa chakula.

“Mfano wa baadhi ya vyakula hivyo ni tende, uji wa moto, supu, magimbi, maboga, juisi ya matunda pamoja na mihogo, ila ni vyema unapoanza kufuturu kuanza na uji ama chai ya moto,” amesema.

Aliongeza kuwa kwa mtu anayefunga ni vyema kuzingatia unywaji wa maji ya kutosha.

Hata hivyo, Mzava ameonya wale wenye tabia ya kula kupita kiasi wakati wa kufuturu na kusisitiza umuhimu wa kula mlo kamili.

“Kuna watu muda wa kufuturu wanakusanya kila kitu na wakati mwingine hujikuta wakila kundi moja la chakula, hasa wanga kuliko protini,” amesema.