Dar es Salaam. Licha ya mfumo wa uongozi unaoweka viongozi katika ngazi mbalimbali za mamlaka za utendaji, ziara za viongozi wa kitaifa nchini, zimekuwa zikifurika sauti za wananchi wenye kero na maumivu wanayopitia katika maeneo yao.
Misafara ya viongozi wakuu wa Serikali au wa chama tawala- Chama cha Mapinduzi (CCM) inapowasili, shangwe za mapokezi huwa zinaambatana na mabango na sauti za wananchi wanaoeleza kero na maumivu yao moja kwa moja mbele ya jukwaa la kitaifa.
Ziara hizo za kikazi za viongozi wa juu kwa maana ya Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu zimekuwa zikipokewa na mabango.
Mikutano yao mingi imekuwa ikigeuka vikao vya kusikiliza malalamiko na kero ndogondogo za jamii kama vyoo na majengo ya shule, maboma ya madarasa, umeme unaokatikakatika, huduma mbaya za maji, barabara kuharibika na migogoro ya ardhi.
Zingine ambazo zimekuwa zikijirudiarudia maeneo mbalimbali ni kero za watu kudhulumiana haki zao, migogoro ya wakulima na wafugaji na kusuasua kwa miradi iliyotolewa fedha na Serikali.
Mbali na viongozi hao, hata ziara za mawaziri nazo zimekuwa zikikumbana na yaleyale huku kukiwa na viongozi ngazi ya wilaya na mikoa wanaomwakilisha Rais, ambapo kiuhalisia au inavyotakiwa iwe baadhi ya kero zinazotolewa wana uwezo wa kuzishughulikia.
Wateule hao watano wa Rais kwenye maeneo hayo ni Wakurugenzi wa Halmashauri (DED), Katibu Tawala Wilaya (DAS), Mkuu wa Wilaya (DC), Katibu Tawala Mkoa (RAS) na Mkuu wa Mkoa (RC).
Kero za wananchi kwa viongozi wakuu zimekuwapo tawala na tawala na limekuwa likikemewa na viongozi kwa kuwataka wasaidizi wao kuzitafutia ufumbuzi si kuziacha hadi ziara za viongozi wananchi wakabeba mabango.
Mathalani, Rais Samia Suluhu Hassan mara kadhaa amekuwa akisisitiza umuhimu wa wasaidizi wake kuwa watumishi wa wananchi kwa kutoka maofisini kwenda kuwasikiliza wananchi kwenye maeneo yao.
“Nitawapima kwa matokeo, sitosita kuchukua hatua kwa atakayeshindwa kazi. Nendeni mkasimamie maendeleo ya wananchi kwa kutatua kero zao,” alisema Rais Samia akiwaapisha mawaziri Novemba 2025 na ameendelea kurudia kauli hiyo mara kwa mara.
Maono na viongozi wakuu hao juu ya utekelezaji wa maagizo hayo ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, zimeendelea kujitokeza tena na kushuhudiwa katika ziara za Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ikiwemo inayoendelea sasa mkoani Tanga.
Anachokutana nacho Dk Mwigulu ndicho kinamtokea Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi ambaye yupo mkoani Tabora katika ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2025/2030.
Uwezekano huo wa utekelezaji unaibua mjadala kuhusu viongozi wa ngazi husika kushughulikia kero za umma, ikiwa uwezo wa kutatua upo, kwa nini kero hizo zinasubiri ziara za kitaifa ndipo zichukuliwe hatua tena za haraka bila kushindwa?
‘Wamezembea kutatua kero’
Mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana anasisitiza kuwa viongozi wa mikoa na wilaya hawapaswi kusubiri ziara za viongozi wakuu ili kusimamia vyema majukumu yao.
“Tatizo kubwa hapa ni ukosefu wa kujiamini na ratiba madhubuti kwa viongozi katika kukagua miradi na kushughulikia kero za wananchi. Kwa hiyo, wananchi wanaibua kero zao kwa viongozi wakuu wanadai uwajibikaji na hii inaonesha dhahiri viongozi katika maeneo yao wamezembea kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” anasema.
Dk Bana aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, anasema taasisi muhimu kama ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zinatakiwa kufuatilia malalamiko ya wananchi, hasa yanayohusu miradi ambayo imetolewa fedha lakini haijakamilika, jambo litakalosaidia kubaini changamoto katika utekelezaji na kusimamia vyema matumizi ya fedha, na kuwawajibisha viongozi wazembe.
Vilevile, Dk Bana anasema viongozi wa ngazi za mikoa, wilaya, halmashauri na mitaa wanapaswa kujiwekea utaratibu wa kuzungukia maeneo yao ili kubaini kero za wananchi na kuzitatua, akisema bila kufanya hivyo wanaitwisha mzigo Serikali kuu na viongozi wakuu ambao tayari wana majukumu mengi ya kitaifa.
“Hawa wakuu wa mikoa na wilaya, makatibu tawala na wakurugenzi wanapaswa kujiamini na kujiwekea utaratibu wa kushughulikia kero za wananchi kama ilivyoagizwa kwenye miongozo yao ya kazi, ili kutowaachia mzigo mkubwa viongozi wa kitaifa na huu ndio ugatuaji wa madaraka tunaoutaka nchini,” anasema.
Mmoja wa viongozi waandamizi serikalini ambaye ameomba hifadhi ya jina lake anasema wateule hao wa Rais ngazi ya mikoa na wilaya wanaweza kuzitatua kero hizo lakini kinachoonekana hawajipangi vizuri.
“Ni uzembe tu, huwezi kuwa na Ma DAS, DED, DC, RAS na RC wakashindwa kutatua migogoro au kero ndogondogo hadi usubiri viongozi wakuu. Kukiwa na ufuatiliaji wa karibu na kuwawekea mkazo, hawa wanaweza kuzitatua kabisa,” anasema.
‘Utawala haufanyi kazi’
Katika hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda, anasema hicho ni kiashiria cha utawala ambao haufanyi kazi vizuri. Akiweka wazi kuwa mamlaka za uwajibikaji hazijakaa sawa.
“Katika mamlaka za mikoa na wilaya wananchi wanapaswa kuwa na uwezo wa kuwawajibisha viongozi wao, lakini kwa sasa viongozi hawa wote hawawajibiki kwa wananchi, wanawajibika moja kwa moja kwa Rais.”
“Hivyo wengi hujiona kama si watumishi wa wananchi, hujiona kama watawala wanaotakiwa kuamrisha wanakuwa imara wanapokuja viongozi wa kitaifa na kusimamia maelekezo ya viongozi kwa kuwa hao ndio wanaowawajibisha,” anasema.
Ili kuondokana na hili, Dk Mbunda anasema yanahitajika mabadiliko ya mfumo wa uongozi kupitia mifumo ya katiba, badala ya kuwa na viongozi wa mikoa na wilaya wanaoteuliwa na kumuogopa Rais pekee.
“Viongozi hawa wachaguliwe na watu watawajibika wala hawatasubiri ziara ya kiongozi wa kitaifa, maana akitokea kiongozi asiyeogopeka hawatawajibika kabisa,” anasema.
Anafafanua, “Viongozi wana nguvu kuliko mifumo ya kiutawala, bado hatujajenga mifumo ya taasisi imara ambayo inafanya kazi, badala yake viongozi wamekuwa na nguvu kubwa, hasa katika mambo yanayohitaji bajeti inakuwa ngumu kwa viongozi walipo chini kusimamia ila kiongozi mkubwa kama Waziri Mkuu akitoa maelekezo pesa zinatoka na kumaliza mambo hayo,” anaongeza mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, Ezekiel Kamwaga.
Kamwaga anasema kero nyingi zinazoibuka kwenye ziara za viongozi wa kitaifa zinakuwa ndogo sana ambazo wangeweza kuzimaliza viongozi wa mikoa na wilaya, lakini kutokana na changamoto za kimfumo na kibajeti usimaizi wake unakuwa mdogo akisema maelekezo ya kiongozi wa kitaifa kama Waziri Mkuu huongeza nguvu kwa kuwa ana vyanzo vingi na anaweza kuamuru kutoka mfuko wa Serikali kuu.