Mawakili walivyogonga mwamba kumnusuru Epstein na mashitaka – 7

Jitihada za mawakili wa Epstein kutaka FBI wajiondoe, ili mashauri ya mteja wao yashughulikiwe na mamlaka za jimbo la Florida, ziligonga mwamba. Kazi ya FBI kupitia Oparesheni Leap Year ilitoa matunda ya kwanza. Mei 15, 2007, Mwendesha Mashitaka wa Mamlaka ya Shirikisho, Marie Villafana, aliandika hati ya mashitaka dhidi ya Epstein, yenye kurasa 53, mashitaka makubwa yakiwa 60.

Marie pia aliandika kurasa 82 za taarifa kuhusu mashitaka ya Epstein kwenda kwa wakuu wake wa kazi, akiwemo Alexander Acosta, ambaye wakati huo alikuwa wakili wa Serikali kwa ajili ya Mahakama ya Wilaya, Kusini ya Jimbo la Florida; Wakili Msaidizi wa Kwanza wa Serikali, Jeffrey Sloman; na Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Jinai, jiji la Miami, Florida, Matthew Menchel. Kipindi chote cha uandaaji wa mashitaka, Menchel alimweleza Marie kuwa Acosta hakuwa tayari kwa kesi.

Menchel alikuwa sahihi. Shauri lilipotua mezani kwa Acosta, uliibuka mshangao wa karne. Acosta alifanya makubaliano na Epstein ya kutoendelea na mashitaka dhidi yake. Dili hilo lilimpa kinga ya mashitaka yote ya Epstein kushughulikiwa na mamlaka za shirikisho. Gazeti la Miami Herald liliandika kufafanua makubaliano hayo kwamba yaliizuia FBI kuendelea na uchunguzi dhidi ya Epstein wala kutafuta waathirika zaidi.

Dili hilo la makubaliano lilitoa ulinzi wa kutoshitakiwa kwa washirika wanne wa Epstein, akiwemo aliyekuwa mpenzi wa tajiri huyo, Ghislaine Maxwell, ambaye ndiye aliyefanya kazi kubwa kutafuta wasichana wadogo na kuwashawishi waingie kwenye makasri ya Epstein walikofanyiwa ukatili wa aina mbalimbali wa ngono. Ni makubaliano ambayo yalidhihirisha kuwa kulikuwa na kitu baina ya Acosta na Epstein.

Vyombo vya habari Marekani viliyaita makubaliano ya kutoendelea na mashitaka dhidi ya Epstein kwa jina la “sweetheart deal”, yaani dili la mapenzi. Dhahiri, Epstein alipata upendeleo mkubwa, licha ya kila kitu kuonesha na ushahidi kuthibitisha kwamba bilionea huyo alikuwa mhalifu wa ngono kwa watoto wadogo wa kike. Zaidi, dili hilo lilikwenda kinyume na sheria ya shirikisho kwa kutowajumuisha waathirika kwenye makubaliano husika.

Juni 30, 2008, ndiyo tarehe ambayo makubaliano ya kutoendelea na mashitaka yalisainiwa baina ya Acosta na mawakili wa Epstein. Ndani ya Mahakama ya Kaunti ya Palm Beach (15th Judicial Circuit), Epstein alikiri kosa moja la “Kushawishi Ukahaba”, pia alikubali hatia ya “Kununua Mtoto Chini ya Miaka 18 kwa ajili ya Ukahaba.”

Kwa kukiri makosa, Epstein alihukumiwa kifungo cha miezi 18 jela. Ni hapo, kuanzia Juni 30, 2008, ikawa rasmi kuwa Epstein ni mhalifu wa ngono. Katika sehemu ya makubaliano hayo, Epstein alitakiwa kuwalipa fidia wasichana 36 walioathirika kutokana na vitendo visivyofaa vya bilionea huyo, kama walivyorekodiwa na FBI.

Baada ya kuhukumiwa miezi 18 jela, badala ya kupelekwa kwenye gereza la jimbo kama wahalifu wengine wa makosa ya ngono, Epstein alishikiliwa kwenye kizuizi cha Palm Beach County Stockade. Aliwekwa sehemu ya faragha na mlango wake haukufungwa. Alikuwa na fursa ya kuonana na wakili wake wakati wowote aliohitaji. Alipomaliza miezi mitatu na nusu, alipewa uhuru wa kutoka kwenda kazini kwake kwa saa 12 kwa siku. Ruhusa hiyo ilikuwa ya siku sita katika wiki.

Sera ya jimbo ilitaka mtu mwenye hatia atumikie kifungo cha miezi 10 kwanza, ndipo aweze kupata ruhusa ya kutoka nje na kurudi ndani kwa saa kadhaa. Eneo hilo lilidhihirisha pia jinsi Epstein alivyokuwa na mkono mrefu. Alilindwa, alitetewa ngazi kwa ngazi, pamoja na uhalifu wake mkubwa alioutenda. Mwisho kabisa, jela hiyo ya “picnic” Epstein aliitumikia kwa miezi 13 badala ya 18 aliyohukumiwa.

Ndani ya hiyo miezi 13, ukiacha miezi mitatu na nusu ya kwanza, Epstein alitoka kwenda kazini kwake kila siku kwa saa 12. Dereva binafsi wa Epstein ndiye aliyekuwa anamwendesha mhalifu huyo kila siku kutoka kwenye jengo alilowekwa kama mfungwa kwenda ofisini na kurudi kizuizini. Maofisa waliokuwa wanamlinda, Epstein aliwalipa fedha kwa jina la posho ya kufanya kazi zaidi ya muda wa kawaida (overtime).

Kingine, Epstein alilipa gereza dola 128,000 (Sh334 milioni) kwa ofisi ya gereza, ikielezwa zilikuwa za kufidia gharama za ziada kipindi chake akiwa ameshikiliwa kizuizini. Ndani ya kizuizi hicho, Epstein alifungiwa televisheni kubwa, hivyo kuzidi kuyafanya maisha ya jela kwake yawe kama alikuwa uraiani. Aliweza kutoka kwenda kazini kwa saa 12; vilevile aliporejea kizuizini, alipata huduma zilizokaribiana na zile alizozipata nyumbani kwake.

Lawama kubwa ni kwa Acosta. Pamoja na makosa yote aliyoyafanya kumpa ulaini Epstein, lakini Rais Donald Trump aliposhinda urais muhula wa kwanza, alimteua kuwa Waziri wa Ajira. Watu wengi walilaani uamuzi wa Trump kumpa Acosta nafasi hiyo nyeti kulingana na rekodi zake za nyuma. Zingatia, Trump alikuwa rafiki wa karibu wa Epstein. Naye yumo kwenye orodha ya mafaili ya Epstein.

Septemba 2025, Acosta alihojiwa Baraza la Wawakilishi (HoR) kupitia Kamati ya Uangalizi na Usimamizi wa Serikali. HoR walitaka kujua uhusiano uliokuwepo baina ya waziri huyo wa zamani na Epstein, na kwa nini alimpa dili la makubaliano yenye upendeleo. Acosta alijitetea kwamba mashitaka dhidi ya Epstein yalikuwa hayana nguvu ya kumtia hatiani. Acosta alidai kuwa waathirika wengi waliogopa kujitokeza kutoa ushahidi.

Acosta aliwaeleza wawakilishi kwamba waathirika wengine walikuwa na historia mbaya za nyuma, kwa hiyo walihofia kuumbuliwa na mawakili wa upande wa utetezi. Aliendelea kusema kuwa mawakili wa utetezi wangekuwa imara dhidi ya waathirika. Acosta alisisitiza kuwa kesi dhidi ya Epstein ilikuwa upuuzi ambao usingeweza kushawishi hukumu mahakamani.

Kutokana na maelezo hayo, wajumbe wa kamati walimuuliza Acosta ni kwa nini sasa Epstein na mawakili wake walisaini makubaliano ya kwenda jela, ikiwa mashitaka yalikuwa “upuuzi”, na hakukuwa na ushahidi wenye nguvu? Acosta akajibu: “Yalikuwa maoni ya timu ya waendesha mashitaka wa Serikali kuwa kumweka jela bilionea kungetuma alama yenye nguvu kwa jamii kwamba hili halikubaliki, lile siyo sawa, lile haliwezi kutokea.”

Acosta aliendelea kwa kusema kuwa makubaliano ya kutoendelea na mashitaka yaliifanya dunia itambue kilichokuwa kinaendelea. “Iwe dunia ilisikiliza au la, tunaweza kuiweka upande mmoja, lakini inaipa dunia taarifa kwamba alikuwa mhalifu, na mhalifu wa ngono,” alisema Acosta, ambaye baadaye alidai sababu kubwa ya kumpa Epstein dili la kutoendelea na mashitaka ni kwa sababu waathirika wengi waligoma kutoa ushirikiano.

“Juu ya kila kitu, mashitaka yalikuwa upuuzi, na sisi tulichokuwa tunataka ni Epstein kwenda jela,” alisisitiza mkuu huyo wa mashitaka wa zamani wa Jimbo la Florida.

Juni 18, 2010, meneja wa zamani wa kasri la Epstein lililoko Palm Beach, Alfredo Rodriguez, alihukumiwa miezi 18 jela. Makosa ya Alfredo yalikuwa kutokwenda polisi; badala yake akaanza kutaka kuuza jarida lenye matukio aliyorekodi alipokuwa anafanya kazi nyumbani kwa Epstein.