Mwanza. Inaweza ikawa moja ya hukumu za kihistoria baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, kutamka kuwa kifungu cha sheria kinachoruhusu baadhi ya mashahidi wa Jamhuri kutoa ushahidi wao kwa kufichwa kinakiuka Katiba ya Tanzania.
Hukumu hiyo inakuja wakati baadhi ya mashahidi kesi ya uhaini dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, wakitoa ushahidi kwa kificho bila Lissu kuwatambua kwa sura na jina.
Ni mawakili wa upande wa mashitaka pekee ndio wanaowafahamu kwa sura na majina na jopo la majaji wanaoendesha kesi ya Lissu nao wanaoweza kumuona shahidi katika kizimba maalumu, huku Lissu akisikia tu sauti ya shahidi.
Hata hivyo, katika hukumu yao ya shauri la kikatiba lililofunguliwa na wakili Godfrey Mjuni Basasingohe, walioutoa Februari 16,2025 Jijini Mwanza, jopo la majaji watatu limesema kifungu kinachotoa ruksa hiyo kinakiuka Katiba.
Majaji hao wamesema kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinachotoa ulinzi wa kisheria kwa mashahidi hakitoi usawa wa sheria kama ilivyoainishwa chini ya kifungu cha 12(1) na 13(1) cha Katiba ya Tanzania.
Kulingana na majaji hao, Fahamu Mtulya, Kamana Stanley na Wilbert Chuma, wamesema kifungu hicho kinakiuka Katiba kiasi kwamba kinatoa haki za ulinzi kwa shahidi wa mashitaka pekee na kuwanyima haki mashahidi wa upande wa utetezi.
“Ndani ya miezi 12 kuanzia tarehe ya uamuzi huu, kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifanyiwe marekebisho na Bunge la Tanzania ili kuzingatia kanuni ya ulinzi sawa wa sheria, na kushindwa kufanya hivyo, kifungu hicho hakitakuwa na nguvu ya kisheria,” wameeleza majaji hao.
Katika shauri hilo la Kikatiba namba 22482 la 2025, wakili Basasingohe ambaye aliwakilishwa kortini na wakili Elias Hezron, alifungua shauri hilo dhidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).