Timbwili laibuka CUF, Polisi yaingilia kati

Timbwili jipya limeibuka Makao Makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), Buguruni jijini Dar es Salaam baada ya wanachama wake kugawanyika katika pande mbili, wapo wanaoutambua uongozi uliopo na wengine wanaoukataa.

Chanzo cha mgawanyiko huo ni barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyobatilisha uchaguzi uliofanyika mwaka 2024, uliomweka Profesa Ibrahim Lipumba katika nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho pamoja na wenzake watano.

Inadaiwa, kwa mujibu wa uamuzi huo, Profesa Lipumba na wenzake hawakupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa, hivyo ushindi wao ukatajwa kuwa batili na uchaguzi huo ulipaswa kurudiwa.

Baadhi ya makada, wanachama, Polisi wakiwa kwenye ofisi za CUF.



Leo Jumanne, Februari 17, 2026, uongozi wa chama hicho uliitisha mkutano na vyombo vya habari. Hata hivyo, wakati Naibu Katibu Mkuu-Bara, Magdalena Sakaya, akizungumza, wanachama wasiotambua uongozi huo walifika na kuanza mkutano wao wa vyombo vya habari, nje ya ukumbi aliokuwa akifanya mkutano jambo lililozua taharuki na gumzo miongoni mwa waliohudhuria.

Hali hiyo ilisababisha mikutano yote kuvurugika baada ya Jeshi la Polisi kuingilia kati ili kudhibiti vurugu zilizoanza kujitokeza, huku kila upande ukimpinga mwenzake.

Endelea kufuatilia Mwananchi