Unguja. Wakati mahitaji ya mchele ikiwa ni tani 153,000 kwa mwaka, Zanzibar inazalisha tani 40,391.97 za mpunga na kufanya upatikanaji wa tani 26,000 za mchele sawa na asilimia 17 za mahitaji.
Kiwango hicho kinaifanya Zanzibar iwe na upungufu wa tani 127,608.03 za mchele kwa mwaka.
Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Mifugo, Dk Salum Soud Hamed amesema upungufu huo hufidiwa kwa biashara ya mchele kutoka nje ya Zanzibar.
Dk Soud alikuwa akijibu swali la msingi leo Jumanne, Februari 17, 2026, barazani lililoulizwa na mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayoub akitaka kujua kuna tathmini gani imefanyika kutambua kiwango cha uzalishaji wa ndani wa mchele na kile kinachohitajika kuagiziwa nje.
“Tathmini ya kutambua kiwango cha uzalishaji wa ndani wa mchele imefanyika mwaka 2024/25 ambapo jumla ya tani 40,391.97 za mpunga huzalishwa Zanzibar kwa mwaka na kupatikana tani 26,000 za mchele,” amesema Dk Soud na kuongeza.
“Mahitaji yetu ya mchele ni tani 153,000 kwa mwaka, kukiwa na pengo la tani 127,608.03 za mchele kwa mwaka, ambalo hufidiwa kwa biashara ya mchele kutoka nje ya Zanzibar,” amesema Dk Soud
Hata hivyo, amesema jitihada mbalimbali zinaendelea kufanywa ambapo Serikali imeanza kutekeleza mkakati wa kuongeza chakula kwa kutoa kipaumbele ya kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde ya mpunga.
Amesema kuna jumla ya hekta 8,521 ambazo zimetengwa kwa ajili ya umwagiliaji katika mabonde sita kwa Unguja na Pemba, hatua ambayo wanaamini katika utekelezaji wake utasaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
Kadhalika, amesema Serikali inajenga maghala mawili ya kuhifadhi mchele yenye uwezo wa kuhifadhi tani 60,000 ambapo yatasaidia kuhifadhi mpunga hivyo ikitokea kuna upungufu itakuwa ipo tayari kutoa chakula hicho kwa ajili ya wananchi.
“Kwa hiyo tutakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 80,000 za mpunga Serikali itakuwa ikitoa mchele huo pale inapotokea kuna uhaba wa mkubwa,” amesema
Pia mwakilishi huyo alitaka kujua kuhusu utekelezaji wa agizo la Serikali la kuimarishwa kilimo cha mpunga ili Zanzibar ipunguze uagiziaji wa mchele.
Naibu Waziri amesema utekelezaji wa agizo la Serikali la kuimarishwa kilimo cha mpunga limetekelezwa kwa asilimia 100 kupitia mradi uliokamilika mwaka 2025, ambapo jumla ya skimu sita mpya za umwagiliaji zimejengwa miundombinu ya kisasa ikiwemo visima 39. Mabwawa matatu yenye kiwango cha zege yenye urefu wa kilomita 82.17 na mitaro ya kutolea maji ya kilomita 72.47 na barabara za kuingilia mashambani zenye urefu wa kilomita 85.43.
Mwaka 2011, Baraza la Mapinduzi lilitoa waraka maalumu kuhusu kuimarishwa kilimo cha mpunga Zanzibar na kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula na kuwekewa bajeti yake. Miaka mingi imepita hakujafanyika tathmini kutambua hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa agizo hilo la Serikali.