Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameishauri Serikali kurejesha utaratibu wa kutoa vibali vya watu wanaotakiwa kutumia vilevi ili kudhibiti matumizi holela kama inavyoonekana kwa sasa kisiwani humo.
Hayo yameelezwa leo Jumanne, Februari 17, 2025 wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika mkutano wa 11 wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani, Unguja Zanzibar.
Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman amesema Serikali haioni umuhimu wa kuweka utaratibu wa kutoa vibali maalumu kwa wanaotaka kunywa, ili kuepusha athari zinazoweza kutokea ikiwamo vilevi kutumika holela na hata kwa vijana wadogo.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Idrissa Mustafa Kitwana amesema kwa kuwa baraza ndilo lenye jukumu la kutunga sheria basi wakiona linafaa wanaweza kulipeleka ili kuhakikisha jambo hilo linatekelezwa.
Katika swali la msingi, Dk Mohamed amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la uingizaji wa kilevi kinachojulikana kama Double Kick kwa siku za karibuni Zanzibar, kinyume na sheria ya vileo namba 9 ya mwaka 2020.
Amesema kilevi hicho kina zaidi ya asilimia 43 ya alcohol, jambo linalosababisha athari kubwa kwa vijana wanaokitumia akitaka kujua kiwango kipi Serikali inalitambua tatizo hili la uingizwaji wa kilevi hicho.
Amesema uingizwaji kiholela wa Double Kick pamoja na kuuzwa kwake katika maduka ya kawaida hapa Zanzibar hususan wakati wa usiku, unakubalika vipi kwa mujibu wa Sheria ya Vileo Namba 9 ya mwaka 2020.
Akijibu swali hilo, Waziri Kitwana amekiri kweli Serikali inatambua karibuni kumekuwa na uingizwaji wa vileo aina ya double kick, ambavyo, huingizwa nchini na baadhi ya wafanyabiashara waliopewa vibali kisheria kama wanavyoingiza vingine.
“Hata hivyo, tulichogundua tatizo halipo kwenye uingizwaji, bali linaanzia kwenye usambazaji na uuzaji, ambapo baadhi ya wafanyabiashara walioruhusiwa kisheria huwapatia vijana vileo hivyo vya double kick kuuza katika maeneo yasiyo rasmi,” amesema Waziri Kitwana na kuongeza.
“Kwa mfano, kuuza kwenye maduka ya kawaida ya mitaani jambo ambalo, Serikali imeliona na sasa imeanza kuchukua hatua ya kupambana nalo kupitia Bodi ya ushauri na udhibiti wa vileo, kwa kufanya operesheni mbalimbali na kuchukua hatua kwa wale wanaofanya biashara hiyo kinyume na sheria na kanuni za vileo,” amesema.
Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Azza Januari Joseph ameshauri ili kukabiliana na changamoto hiyo ni vyema Serikali ikaongeza bei ya bidhaa hizo.
Hata hivyo amesema kuongeza bei hakuwezi kuwa suluhisho ya matumizi ya kinywaji hicho badala yake ipo haja kushirikiana na jamii kutoa elimu kwa vijana ambao ndio wanaonekana kuwa watumiaji wakubwa.
Amesema kuna madai kwamba vijana wanatumia kinywaji hicho wakichanganya na kinywaji cha energy kwa madai ya kuongeza nguvu za kiume.
Sheria ya udhibiti wa vileo nambari 9 ya Mwaka 2020, ndiyo inayosimamia masuala ya uingizaji, usambazaji, uhifadhi na uuzaji wa vileo Zanzibar.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, mwingizaji, msambazaji na muuzaji wa vileo ni lazima awe amepata leseni ya uuzaji, usambazaji au kibali cha kuingiza vileo nchini kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 25 (1) cha sheria hiyo.