Airtel yafungua maduka Manne ya kisasa Mkoani Arusha

Arusha.

KAMPUNI ya Airtel Tanzania imefungua
maduka manne mapya ya Smart Shop katika Jiji la Arusha ikiwa ni sehemu ya
juhudi zake za kupanua upatikanaji wa mawasiliano ya kidijitali na huduma za
kifedha.

Maduka hayo yalizinduliwa rasmi Alhamisi
na kaimu mkuu wa wilaya Bi Chausiku Baha ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya
ya Jiji la Arusha, Bw. Joseph Modest Mkude, alisema Serikali inaendelea kuipa
kipaumbele sekta ya mawasiliano kama kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi na
mabadiliko ya kidijitali.

Bi. Chausiku alisema Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejizatiti kuboresha miundombinu ya
mawasiliano na kuharakisha matumizi ya teknolojia za kidijitali ili kuongeza
ufanisi wa utoaji huduma na kusaidia ukuaji wa biashara.

Alitaja takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) zinazoonesha ukuaji endelevu wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya robo ya nne
iliyomalizika Desemba 2025, usajili wa laini za simu za mkononi uliongezeka
kutoka milioni 99.3 hadi milioni 106.9, huku usajili wa intaneti ukiongezeka
kwa asilimia 3.2. Matumizi ya intaneti yaliongezeka kwa asilimia 9.5 katika
kipindi hicho.

Ripoti hiyo pia inaonesha kiwango cha
matumizi ya simu janja (smartphone penetration) kikiwa asilimia 41.82 na upenyo
wa matumizi ya simu kwa ujumla (mobile penetration) ukiwa asilimia 87.11,
ukuaji unaochochewa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji unaoendelea katika
miundombinu ya mtandao, ikiwemo upanuzi wa huduma za intaneti zenye kasi kubwa
kama 5G.

“Ukuaji wa sekta ya mawasiliano
umechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha uwekezaji, kusaidia biashara na
kuboresha maisha ya wananchi,” alisema Bw. Mkude, akiongeza kuwa Arusha
inaendelea kuvutia wawekezaji kutokana na soko lake linalokua na umuhimu wake
wa kimkakati.

Maduka manne mapya ya Airtel Smart Shop
yapo katika maeneo ya Triple A, Morombo, Ngaramotoni na Taasisi ya Uhasibu
Arusha (IAA).

Maduka hayo yanatoa huduma mbalimbali
ikiwemo mawasiliano ya simu na intaneti, malipo ya kidijitali kupitia Airtel
Money, usajili wa laini za simu pamoja na huduma kwa wateja.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi
wa Uzoefu wa Wateja wa Airtel Tanzania, Bi. Adriana Lyamba, alisema maduka hayo
ni sehemu ya mkakati wa kampuni kuwasogezea wateja huduma kupitia vituo vya
kisasa vya kidijitali.

Alisema Smart Shop hizo zisizotumia
karatasi (paperless) zimeundwa kuongeza ufanisi wa huduma, kupunguza muda wa
kusubiri na kuchangia uhifadhi wa mazingira.

“Smart Shop hizi ni za kidijitali
kikamilifu, hazitumii karatasi, na zimeundwa kutoa huduma kwa haraka, kwa
ufanisi zaidi na kwa kuzingatia mazingira. Hii inaakisi dhamira yetu chini ya
kaulimbiu ya ‘Airtel Kila Kona’ kuhakikisha kila Mtanzania anapata mawasiliano
ya kuaminika na huduma za kifedha za kidijitali,” alisema.

Bi. Lyamba aliongeza kuwa kila duka
linatarajiwa kusaidia zaidi ya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo 400
katika maeneo yanayolizunguka kwa kuwawezesha kupata mawasiliano na huduma za
malipo ya kidijitali kwa urahisi, pamoja na kuchangia ajira hususan kwa vijana.

Airtel Tanzania imeendelea pia kuwekeza
katika miundombinu ya mtandao mkoani Arusha, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa
minara ya mawasiliano ili kuongeza wigo wa huduma na kuboresha ubora wa
mtandao