BAADA ya timu 32 zikiwamo nne za Tanzania kuchujwa katika hatua ya makundi, leo Jumanne inachezeshwa droo ya kupanga mechi za robo fainali za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, huku timu za Afrika Kaskazini maarufu kama ‘Waarabu’ wakitawala kila noma.
Ukanda huo wa Afrika Kaskazini umeingiza jumla ya timu 11 kati a 16 zilizopo hatua hiyo kwa michuano hiyo, tano zikiwa Ligi ya Mabingwa na sita zikiwa Shirikisho, japo droo ya leo inayofanyika makao makuu ya Shirikisho la Soka la Misri (EFA), jijini Cairo, huenda ikazipunguza kwani asilimia kubwa zitafanya zikutane zenyewe kwa zenyewe.
Katika Ligi ya Mabingwa ‘waarabu’ sita waliopo huko ni watetezi wa taji, Pyramids na Al Ahly za Misri, AS FAR Rabat na RS Berkane za Morocco na Esperance ya Tunisia, huku ukanda wa CECAFA ukiingiza moja Al Hilal ya Sudan kama ilivyo kanda ya COSAFA yenye Mamelodi Sundowns na WAFU ikiingiza Stade Malien ya Mali.
Kwa Kombe la Shirikisho timu sita zilizotinga robo ni Olympique de Safi n Wydad AC za Morocco, Al Masri na Zamalek za Misri pamoja na USM Alger na CR Belouizdad za Algeria, huku Otoho d’Oo ya Congo Brazzaville na As Maniema ya DR Congo zikipenya kutoka Kanda ya Kati.
Kwa mujibu wa ratiba ya CAF, droo ya Kombe la Shirikisho itaanza saa 8:00 mchana kwa saa za Afrika Mashariki, ikifuatiwa na droo ya Ligi ya Mabingwa saa 9:00 alasiri.
Droo hizo zitaamua ratiba ya mechi za robo fainali pamoja na njia ya kuelekea fainali katika mashindano yote mawili.
Katika droo hiyo, vinara wa makundi kila mashindano, watakuwa upande mmoja na walioshika nafasi ya pili upande wao. Vinara wa makundi wataanzia ugenini na kumalizia nyumbani katika mechi za robo fainali zitazochezwa Machi 15 na 22, upande wa Kombe la Shirikisho wakati Ligi ya Mabingwa ikiwa kati ya Machi 13 na 14, marudiano kati ya Machi 20 na 21.
Timu kutoka kundi moja haziwezi kukutana robo fainali, huku timu kutoka nchi moja zinaweza kukutana.
Katika droo za nusu fainali, hakutakuwa na upangaji, na timu kutoka kundi moja au chama kimoja zinaweza kupangwa dhidi ya kila mmoja. Kwa kuwa droo za robo fainali na nusu fainali zitafanyika pamoja kabla ya robo fainali kuchezwa.
Mechi za nusu fainali Kombe la Shirikisho ni Aprili 12 na 19, 2026, kisha fainali itachezwa nyumbani na ugenini Mei 9 na Mei 16 mwaka hu.
Kwa Ligi ya Mabingwa, nusu fainali itachezwa kati ya Aprili 10 na 11, marudiano kati ya Aprili 17 na 18, huku fainali ya kwanza ni Mei 15 na marudiano Mei 24 mwaka huu.
Klabu nne zimethibitisha nafasi katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2025–2026, baada ya kukamilika kwa hatua ya makundi juzi Jumapili.
Katika kila kundi, kulikuwa na timu nne zilizocheza mechi sita kila moja, huku timu mbili za juu zikifuzu kwenda hatua ya mtoano.
Baada ya kumalizika kwa mechi za mwisho za makundi, vigogo kadhaa wa soka la Afrika wamekata tiketi ya kuingia nane bora, huku Stade Malien ikiandika historia kwa kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia yake.
Mabingwa watetezi wa michuano hii, Pyramids FC wameongoza Kundi A kwa pointi 16 baada ya kushinda mechi tano na sare moja. Timu hiyo ya Misri imefunga mabao 14 na kuruhusu mawili pekee.
RS Berkane ya Morocco iliyobeba Kombe la Shirikisho msimu uliopita, imemaliza nafasi ya pili kwa pointi 10, ikiizidi Power Dynamos ya Zambia. Rivers United ya Nigeria ilishika mkia wa kundi hilo kwa pointi moja.
Kwa upande mwingine, mabingwa wa kihistoria wa Misri na michuano hii, Al Ahly wameongoza Kundi B kwa pointi 10 baada ya kucheza mechi sita bila kupoteza (ushindi mara mbili na sare nne). Klabu hiyo ya Cairo imeruhusu mabao matatu pekee, huku ikifunga manane.
FAR Rabat, imemaliza ya pili kwa pointi tisa, ikiizidi kidogo Yanga (8), huku JS Kabylie ikiwa mkiani na pointi tatu.
Al Hilal Omdurman ya Sudan imemaliza kileleni mwa Kundi C kwa pointi 11 baada ya ushindi muhimu katika mechi ya mwisho. Imefunga mabao tisa na kuruhusu saba.
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini imeshika nafasi ya pili kwa pointi tisa, ikiipiku MC Alger iliyomaliza na pointi saba huku Saint-Éloi Lupopo ikiwa na tano.
Stade Malien ya Mali imeibuka kinara wa Kundi D kwa pointi 11, ikiruhusu mabao mawili tu katika mechi sita. Ulinzi wao thabiti ulikuwa silaha yao kubwa katika kundi lililokuwa na ushindani mkali.
Esperance ya Tunisia imechukua nafasi ya pili kwa pointi tisa, ikiizidi Petro Atlético ya Angola (6) na Simba ya Tanzania (5).
Klabu za Misri, Zamalek na Al Masry, ni miongoni mwa timu zilizofuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2025–2026.
Katika Kundi A, USM Alger iliongoza msimamo kwa pointi 14 baada ya kumaliza hatua ya makundi bila kupoteza mchezo, ikishinda mechi nne na kutoa sare mbili. Timu hiyo ya Algeria ilifungwa mabao manne pekee katika michezo sita, huku ikifunga tisa.
Olympique de Safi ya Morocco ilimaliza nafasi ya pili kwa pointi 13, ikiwa imepoteza mchezo mmoja tu katika hatua ya makundi. Timu zote mbili zilikuwa tayari zimehakikisha kufuzu kabla ya mechi ya mwisho.
WAA 05
Mabingwa wa Morocco, Wydad AC, wamemaliza kileleni mwa Kundi B kwa pointi 15 baada ya kushinda mechi tano kati ya sita, wakishinda tano mfululizo mwanzoni mwa hatua ya makundi.
Maniema Union ya DR Congo imeshika nafasi ya pili kwa pointi 12, ikiwa mbele kwa pointi tatu dhidi ya Azam (9). Azam na Nairobi United (0) zimeaga mashindano baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu na nne.
Kutoka Algeria, CR Belouizdad imefuzu kutoka Kundi C kwa pointi 15, ikishinda mechi tano kati ya sita. Timu hiyo imeonyesha makali ya ushambuliaji kwa kufunga mabao tisa na kuruhusu manne pekee.
AS Otoho ya Congo imeshika nafasi ya pili kwa pointi tisa, ikiizidi Singida Black Stars na Stellenbosch katika msimamo zilizomaliza na pointi tano kila moja.
Kundi D lilitoa ushindani mkali zaidi katika hatua ya makundi. Zamalek imemaliza kileleni kwa pointi 11 baada ya kuifunga Kaizer Chiefs mabao 2-1 katika mechi ya mwisho.
Al Masry imeshika nafasi ya pili kwa pointi 10 kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Zesco United.
Matokeo hayo yalikuwa ya uamuzi katika kundi ambalo timu tatu zilikuwa zikitofautiana kwa pointi moja tu kuelekea raundi ya mwisho. Kaizer Chiefs imekosa kufuzu licha ya kumaliza na pointi 10 pia, ikizidiwa kwa tofauti ya mabao.