BAADA ya kukwama kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba inaanza upya msako wa tiketi ya kushiriki michuano ya CAF kwa msimu ujao, itakaposhuka usiku wa leo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kucheza dhidi ya Greenland ya Kagera.
Mechi hiyo ni kati ya 32 za hatua ya 64 Bora zinazoanza kwa ajili kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo msimu huu iliwakilishwa na Azam FC na Singida Black Stars zilizoishia makundi la Simba na Yanga zilizokuwa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho, itakayopigwa leo saa 1:00 usiku, Simba inaingia ikihitaji kuendeleza furaha ya mashabiki wa timu hiyo, baada ya mwenendo mbaya michuano ya CAF.
Simba iliyochukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho FA mara nne tangu michuano hiyo ilipoanza ikifahamika kwa jina la (FAT) mwaka 1967, inakabiliwa na ukame wa kutolichukua taji hilo toka mara ya mwisho kikosi hicho kilipolitwaa msimu wa 2020-2021.
Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kukutana na Greenland iliyopo Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL), huku mechi nyingine, itashuhudiwa maafande wa Transit Camp inayoshika nafasi ya nne katika Ligi ya Championship msimu huu na pointi 36, ikiwa kwenye Uwanja wa Filbert Bayi, Kibaha, Pwani kucheza na Chama la Wana kutokea Mkoa wa Njombe.
Mbeya City iliyo nafasi ya 12 na pointi 13 katika Ligi Kuu msimu huu, itakuwa nyumbani kuikaribisha Biashara United ya Mara inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, huku KMC ikiikaribisha Bandari Tanzania ya Mtwara kwenye Uwanja wa KMC Complex.
‘Walima Zabibu’ wa Dodoma Jiji itakuwa Kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kucheza na Kilimanjaro Wonders ya mkoani Kilimanjaro, huku Fountain Gate ikiwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuikaribisha Mapinduzi FC kutoka Mwanza.
Kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, kutapigwa ‘Derby’ ya mkoani humo, ambapo wenyeji TRA United itaikaribisha Rhino Rangers, inayoshiriki Ligi Daraja la Pili msimu huu, ikitazamiwa pambano litakalovuta hisia zaidi.
Coastal Union, inayoshika nafasi ya 10 na pointi 15, baada ya sare ya bao 1-1 mbele ya maafande wa JKT Tanzania katika Ligi Kuu Bara mechi ya mwisho, itaikaribisha Nyumbu ya Pwani, iliyopo Daraja la Pili.
Bingwa wa michuano hiyo uwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo kwa misimu minne mfululizo, taji hilo limechukuliwa na Yanga, ambayo ndio vinara baada ya kulichukua mara tisa tangu mwaka 1967.