Arusha. Mahakama ya Rufaa imebatilisha adhabu ya kunyongwa hadi kufa waliyokuwa wamehukumiwa watu watatu baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya Geofrey Manionga, baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kuwa ushahidi haukutosha kuthibitisha hatia ya warufani bila shaka yoyote.
Walioachiwa huru katika rufaa hiyo namba 268/2024 ni Yohana Mwambenjele, Andrea John na Rogers Mwakingili, ambao Aprili 4, 2014, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya iliwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kuwakuta na hatia.
Ildaiwa kuwa Mei 21, 2020, walimuua Geofrey huko Uyole, mkoani Mbeya, na mwili wake ulipatikana Mei 23 mwaka huo ukiwa kando ya barabara ya Mbeya–Iringa, katika eneo la St. Agrey, huku ukiwa na jeraha kichwani, lililodaiwa kusababisha kifo hicho.
Hukumu iliyowaachia huru warufani hao ilitolewa Februari 16, 2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo, ambao ni Rehema Kerefu, Lucia Kairo na Dk Deo Nangela na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Jaji Nangela amesema baada ya kusikiliza hoja za pande zote, kupitia mwenendo, wamebaini kuwa kesi ya upande wa mashtaka ilitegemea ushahidi wa kimazingira, ambao haukukamilika kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Amesema katika kesi zinazotegemea ushahidi wa kimazingira pekee, upande wa mashtaka lazima uanzishe mlolongo wa hali kamili kiasi cha kuondoa msingi wowote wa shaka na kuhakikisha hatia ya mshtakiwa inathibitishwa bila shaka yoyote.
Amesema mahakama ilibaini kuwa ushahidi wa shahidi wa nne pamoja na maelezo ya onyo ya mrufani wa kwanza (yaliyorekodiwa na shahidi huyo wa nne) hayakuzingatia sheria, kwani hayakufuata taratibu zilizopo chini ya kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hivyo kuyaondoa kwenye mwenendo wa rufaa hiyo.
Amesema ushahidi muhimu, ikiwemo simu ya mkononi ya marehemu (kielelezo cha pili), hauna mashahidi waliokuwa na uwezo wa kuthibitisha jinsi kielelezo hicho kilivyopatikana kutoka kwa Emmanuel Masasi au Gift Sanga, aliyedai kuuziwa simu hiyo.
“Kutokuwaita mashahidi hawa waliokuwa na taarifa muhimu kumeathiri mlolongo wa ushahidi, na kuacha pengo la msingi linalodhoofisha kesi ya upande wa mashtaka.”
Baada ya kuchambua ushahidi wote na hoja za pande zote, majaji walihitimisha kuwa baada ya kuondoa ushahidi wa shahidi wa nne na maelezo ya onyo ya mrufani wa kwanza, ushahidi uliobaki haukutosha kuthibitisha hatia bila shaka yoyote.
Majaji walihitimisha kwa kueleza kuwa rufaa inakubaliwa, hukumu ya Mahakama Kuu inafutwa, na kuamuru warufani waachiliwe huru isipokuwa kama wameshikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.
Shahidi wa tatu, ambaye ni ndugu wa marehemu, alimweleza shahidi wa sita kuwa mara ya mwisho ndugu yao kuonekana ilikuwa Mei 21, 2020, na mahali mwili ulikutwa, begi lake dogo lililokuwa na mali zake binafsi, ikiwemo simu, halikukutwa eneo hilo.
Ushahidi wa mashtaka ulieleza kuwa simu ya marehemu ilipatikana baada ya kuwasiliana na watoa huduma, ambapo kupitia namba ya utambulisho wa simu (IMEI), simu hiyo ilionekana ikifanya kazi, ambako alikamatwa na kueleza kuwa aliinunua kwa mtu mwingine.
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, baada ya kutathmini ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani, iligundua kuwa upande wa mashtaka ulikuwa umethibitisha kesi yake bila shaka yoyote na kuwahukumu warufani adhabu hiyo.
Kutokana na kutoridhishwa na hukumu hiyo, warufani hao walikata rufaa wakiwa na sababu mbili, ambazo ni upande wa mashtaka kuwaita mashahidi muhimu na kushindwa kuthibitisha kesi hiyo bila shaka yoyote.
Katika rufaa hiyo, upande wa mjibu rufaa (Jamhuri) uliunga mkono rufaa hiyo na kueleza kuwa shahidi wa nne hakuwa miongoni mwa mashahidi ambao taarifa zao zilisomwa kwa warufani katika hatua ya kuwasilishwa.
Aidha, alieleza kuwa ingawa notisi ya shahidi wa ziada inaonekana kuwa katika faili la awali la mahakama, si sehemu ya rekodi ya kesi ya mahakama hiyo, na kueleza kuwa shahidi huyo ndiye aliyerekodi maelezo hayo ya onyo ya mrufani wa kwanza na ndiyo ulikuwa msingi wa kesi ya mashtaka.
Walieleza kuwa bila kufuata ipasavyo Kifungu cha 308 cha CPA kuhusu kuitwa kwa shahidi wa ziada, ushahidi wa shahidi wa nne unatiliwa shaka, na kuhitimisha kuwa kielelezo (maelezo ya onyo ya mrufani wa kwanza) yatakapoondolewa kwenye rekodi ya rufaa hiyo, hakuna ushahidi mwingine wowote unaoweza kuthibitisha hatia.