Watumishi na wataalamu wa Sekta ya Afya nchini wametakiwa kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia kanuni, maadili na misingi ya taaluma zao ikiwemo lugha za staha kwa wagonjwa kama ilivyo kiapo cha kila mtaalamu wa sekta hiyo.
Wito huo, umetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe Februari 16, 2026 wakati wa ziara yake ya Hospitali ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara akiongozana na wadau wa Taasisi ya Kimataifa ya ‘Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation’ (EGPAF).
“Wote hapa tumefundishwa na kuhitimu mafunzo vizuri, majengo kama haya mazuri yamejengwa na Serikali na kusimikwa vifaa tiba vya kisasa, kazi tuliyobaki nayo ni kuwahakikishia wananchi ubora wa huduma” amesema Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe amesema kazi nzuri ikifanyika wanaotakiwa kusema ni wananchi wanaohudumiwa, “wakisema tunafanya vizuri, basi tunafanya vizuri lakini wakisema hatufanyi vizuri tupokee kwa moyo mkunjufu na tukafanyie kazi mapungufu yetu kisha tunarudi kuboresha, lengo ni mwananchi apate huduma iliyo bora,” amesema Dkt. Magembe
“Tuendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaondelea kufanyika katika Sekta ya Afya, najua majengo bado hayajaisha lakini angalau majengo yote ya huduma muhimu yapo na Serikali itaendelea kumalizia majengo yaliyobaki kwa ajili ya kulaza wagonjwa,” amesema Dkt. Magembe.
Pia, Dkt. Magembe amesema Halmashauri ya Babati mkoani Manyara imepokea jumla ya watumishi wapya Tisini na Tisa (99) ambao kati yao wapo waliopelekwa Wilaya ya Babati ikiwa ni katika hatua za kupunguza changamoto ya watumishi katika Sekta ya Afya nchini.
“La mwisho nataka niwasisitizie juu ya kutunza vifaa tiba vilivyonunuliwa na Serikali pamoja na wadau wengine ili viendelee kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi ikiwa ndio lengo la Serikali,” amesisitiza Dkt. Magembe


.jpeg)



