Kero, vituko Kihongosi anapohitimisha ziara Tabora

Tabora. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amehitimisha ziara ya siku tatu mkoani Tabora huku kero na vituko vikiibuka katika mikutano aliyoifanya kwenye wilaya za Igunga na Nzega.

Katika mikutano yake hiyo iliyoanza Februari 15, wananchi wamelalamikia ubovu wa barabara, miundombinu ya elimu, uvamizi wa wanyama pori, changamoto ya maji, mikopo ya asilimia 10 na madaraja ambapo majibu papo hapo yalitolewa huku malalamiko mengine yakiahidiwa kufanyiwa kazi kwa hatua zaidi.

Ziara hiyo ya awamu ya pili ya Kihongosi lenye lengo la kukagua uhai wa chama hicho na miradi ya maendeleo, ilianzia wilayani Igunga ambapo alizungumza na kupokea kero kwa wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Gulioni, Nkinga wilayani humo.

Katika mkutano huo, mkazi wa Kata ya Mwamala, Lusinde Masunga alisema wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na ukosefu wa zahanati pamoja na huduma za vivuko, licha ya kuwapo mito miwili inayokatiza katika kijiji hicho.

“Wananchi tunaangaika na wanyama pori wanaoharibu mazao yetu. Pia barabara za Kata ya Mwamala ni mbovu. Tunaomba Serikali itusaidie kwa sababu kero hizi zinatuumiza sana,” anasema Masunga.

Mbali na hayo, George Maige aliibua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika baadhi ya kata, akiiomba ipatiwe utatuzi, huku Emmanuel Michael, akiiomba Serikali kujenga upya Shule ya Msingi Charles Kabeho, ambayo madarasa yake ni chakavu na baadhi ya kuta zimetoboka na kuhatarisha usalama wa wanafunzi na walimu.

Wananchi wa Wilaya ya Nzega mkoani Tabora wakiwa kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa Stand ya Zamani Wilaya ya Nzega.



Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) Igunga Solomon Hamis alijibu changamoto ya barabara akisema inafahamika na ipo kwenye mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, ikiwemo ujenzi wa madaraja.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Lucia Kafumu, alisema Mwamala tayari kuna zahanati iliyojengwa na katika Kijiji cha Ngunga kuna boma la zahanati lililojengwa kwa nguvu za wananchi ambalo halijakamilika, akiahidi kuliangalia suala hilo katika mwaka ujao wa fedha.

Kuhusu uvamizi wa tembo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga, Joseph Mafuru, alikiri uwepo wa tatizo hilo, hasa katika kata ambazo wanyama hao hupita mara kwa mara na kuwa wanashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kutatua kero hiyo.

Baada ya majibu hayo, Kihongosi aliutaka uongozi wa halmashauri kuweka mikakati ya haraka, ikiwemo kutumia mapato ya ndani kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo, ili wananchi waanze kupata huduma.

Pia aliwahidi wananchi wa Igunga kuwasiliana na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuangalia namna ya kutatua kero hiyo kwenye baadhi ya maeneo, mbali na mradi wa Sh2 bilioni utakaonufaisha wananchi 32,000.

Katika hatua nyingine baadhi wanachama na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa stendi ya zamani Nzega walijikuta wakiangua kicheko kwa nyakati tofauti wakati wakisikiliza kero zilizokuwa zikiwasilishwa.

Moja ya kero hizo, ni pale Zena Mohamed, mkazi wa Nzega alipowaeleza Kihongosi na Hussein Bashe, mbunge wa Nzega Mjini kuwa hana nyumba ya kuishi na ana watoto sita.

Licha ya wananchi kuangua kicheko, Kihongosi alimtaka Mohamed kueleza asaidiwe nini, ndipo alipojibu kuwa “nahitaji kiwanja na chakula, wewe na Bashe ndio mnisaidie maana nina watoto,” maelezo hayo yalisababisha umati uliofurika kuangua kicheko Zaidi.

Baada ya maelezo hayo Bashe alipewa kipaza sauti na kueleza: “Namfahamu mama yangu na najua matatizo yake, nitamuomba aende kwa mkurugenzi, mimi nitalipa kiwanja, kisha tutampelekea tofali. Tutamjengea nyumba angalau ya vyumba viwili au vitatu,” alisema Bashe.

Alipotaka Zena akafuata Simon Simon aliyedai kupewa uniti chache 25 badala ya 74 kama ilivyokuwa wenzake baada ya kununua umeme, akisema anadai zilizobaki.

“Uniti nilizonazo ni 25 nilifika hadi ofisi ya Tanesco wakaniambia wataniongezea, nilipiga simu makao makuu wakiambia nimuone mkurugenzi, nimeangaika karibu miaka minne nasumbuka, nataka uniti zangu,” anasema Simon.

Baada ya malalamiko hayo, Kihongosi alimwita mmoja wa viongozi Tanesco wilayani humo, ambaye aliahidi kulifanyia kazi.

Kabla ya hajamaliza, Kihongosi aliuliza uniti anazodai Simon zina thamani gani akajibu Sh7, 000 kwa kuwa anatumia mfumo wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) na alitakiwa asajiliwe kwenye matumizi madogo.

Baada ya majibu hayo Kihongosi aliagiza Simon akabidhiwe Sh10,000 ili akazinunue uniti anazozidai, jambo lililoibua kicheko na shangwe kwa wananchi waliohudhuria mkutano wake.

Katika ya ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha alisema kuna kijana mmoja alitaka kuitumia ziara hiyo kama fursa ya kuwatapeli viongozi wa Serikali wa mkoa na CCM wilayani Nzega.

“Jana (Jumapili) baada kukupokea kuna mtu mmoja alisema ametumwa na katibu mwenezi na yupo katika msafara wako, alimpigia katibu wa chama wilayani Nzega akimtaka kuandaa Sh400,000 kwa ajili ya mafuta ya gari lililopo kwa mwenezi na afanye haraka.


“Katibu wa chama akamfikishia mkuu wa wilaya (Naitapwaki Tukai) ambaye alimwambia mtu huyo, kama gari hilo lina shida, basi amwonyesha kituo cha mafuta ili kuweka nishati hiyo. Akajibu nyie hamkijui chama, wewe mkuu wa wilaya na mwenezi ama zangu ama zenu na mkeka haujatoka.”

Kwa mujibu wa Chacha baada ya vitisho hiyo, Tukai alimfikisha suala hilo kwa mkuu mkoa ambaye alimtaka mtu huyo ambaye hakutajwa jina akachukue fedha hizo kwake. Hata hivyo baada ya kugundulika alikimbia, lakini vyombo vya dola vitamkamata.