Wakati Kituo cha Michezo cha Jakaya Mrisho Kikwete kikiadhimisha miaka 10 tangu kianzishwe, baadhi ya makocha wamesema zaidi ya wachezaji bora 35 wametokea hapo.
Kituo hicho kilifunguliwa Desemba 2015 na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Kocha mkongwe wa kituo hicho, Bahati Mgunda, alisema wachezaji bora wa kikapu wanaocheza ligi mbalimbali za nchini wamepita hapo akiwataja miongoni mwao kuwa ni Ally Faraji, Marwa Muhangachi (Dar City), Omary Ndulla, Baraka Sabibi (JKT), Victory Michael, Fotius Ngaiza (Vijana ‘City Bulls’) na Rahim Ramadhan (KIUT).
Wengine ni Angel Tumsifu anayekipiga nchini Marekani, Tumaini Ndossi (Tausi Royals), Noela Uwendameno (Jeshi Stars) na Jesca Ngisaise (JKT).
Rahim aliyejifunza kikapu katika kituo hicho alisema mchezaji aliyepitia hapo wamekuwa wakitumainiwa katika timu wanazocheza kutokana na ubora wa mafunzo waliyoyapata.
Alisema: “Faida niliyopata katika kituo hicho timu mbalimbali zimekuwa zikinihitaji kuzichezea katika ligi za kikapu. Jambo ambalo ni faida na neema kwangu.”
Katika sherehe za maadhimisho hayo ilifanyika michezo mbalimbali ya soka, mpira wa magongo na kikapu.
Kwa upande wa kikapu, timu ya wavulana ya Temeke na Ukonga Queens zilitwaa ubingwa, ambapo ushindi Temeke ulitokana na kuifunga Dream Chase kwa pointi 20-17, huku Ukonga Queens ikiifunga St Mary kwa pointi 32-12.
Kwa upande wa mchezo uliowahusisha wachezaji watatu uwanjani (3×3) wavulana, timu ya Dream Chase iliifunga St Mary kwa pointi 22-2, na ule wa wheelchair Malilo iliifunga Machela kwa pointi 28-18.
Katika soka, kocha wa mchezo huo, Abdul Mpunga aliwataja baadhi ya wachezaji waliopitia kituoni hapo ambao wengi wanacheza Ligi Kuu Bara na miongoni mwao ni Omary Chibadi (KMC), Saidi Nashon (Mbeya City), Michael Mwilu (Prisons), Hija Shamte (Mbeya City), Asharf Khalidi (KMC) na Haris Nelson (Fountain Gate).