Wosia, usimamizi wa mirathi vichocheo migogoro ya familia

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kuzinduliwa kwa Kliniki ya Sheria katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, zaidi ya migogoro 60 imesikilizwa huku masuala ya mirathi na ardhi yakiongoza kwa malalamiko.

Katika kliniki hiyo iliyozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari changamoto za mirathi zinaendelea kupasua familia nyingi kutokana na ukosefu wa elimu ya kisheria na uzembe wa kufuata taratibu.

Akizungumza na Mwananchi, leo Jumanne, Februari 17, 2026, Musa Mnima (86) ni miongoni mwa wananchi waliojitokeza katika kliniki hiyo iliyoandaliwa kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za kisheria

“Nimekuja hapa kwa sababu kuna uonevu umetokea katika familia yetu, familia yetu ilimkabidhi mmoja wa ndugu jukumu la kusimamia mali za marehemu kwa niaba ya warithi wote hata hivyo, mambo yalibadilika.

“Tulimuachia mali azitunze, lakini akazimiliki yeye mwenyewe yakiwemo mashamba, sisi familia hatujapata chochote, zaidi ya Sh130 milioni zilitumika bila warithi wengine kushirikishwa, jambo lililosababisha uchungu mkubwa kwa familia,” amesema Mnima.

Mnima amesema yeye ndiye msimamizi wa mirathi lakini waliamua kumpa mdogo wao wa mwisho kusimamia na kuziendeleza mali za wazazi wao kwa kuwa waliopo ni wazee hawawezi hata kutembea.

Musa Mnima mkazi wa Kivule amekitokeza katika viwanja vya Mnazimmoja jijini Dar es Salaam kwenye kliniki ya sheria iliyopo chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupata msaada wa kisheria.



Amesema lengo la kufika eneo hilo ni kurejesha usawa na haki kwa familia nzima na si ugomvi. Wengi wao hawana uwezo wa kwenda huku na kule kufuata haki, matumaini yake yakielekeza kwenye kupata haki kabla muda haujamtupa mkono.

Mnima ni mfano wa wananchi wengi waliojitokeza na kutegemea Kliniki ya Sheria kupata msaada wa kisheria na kuhakikisha haki inatendeka ndani ya familia zao.

Akizungumza  na Mwananchi, Wakili Mwandamizi wa Serikali na Mratibu wa Kliniki ya Sheria ya Taifa kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Silinde Gumada, amesema changamoto za mirathi zinaendelea kuipasua familia nyingi kutokana na ukosefu wa elimu ya kisheria na uzembe wa kufuata taratibu.

Gumada amesema katika siku ya kwanza pekee, kliniki hiyo iliwasikiliza wananchi 2,243, ilipokea na kusikiliza migogoro 63, mingi ikihusu ardhi na mirathi.

“Dar es Salaam ina sura tofauti ya migogoro ya ardhi ukilinganisha na mikoa mingine tuliyopita. Hapa unakuta mgogoro wa jengo la ghorofa au nyumba ya urithi, lakini ndani yake kuna mgogoro wa mirathi,” amesema Gumada.

Amesema baadhi ya kesi zinahusisha ndugu kugombania mali ya mzazi aliyefariki, huku wengine wakijitokeza na nyaraka zenye utata, zikiwamo hati mbili kwa eneo moja.

“Unakuta eneo lina hati mbili, kila upande unadai umiliki halali, hii ni changamoto kubwa sana hapa Dar es Salaam,” amesema.

Sababu zinazoibua migogoro ya mirathi

Akizungumzia mirathi, Gumada amesema zipo sababu kadhaa zinazoibua migogoro, akizitaja baadhi kuwa ni kutoandikwa wosia

Amesema Watanzania wengi hawaandiki wosia wakiwa hai, jambo linalosababisha mvutano mkali baada ya kifo.Kuandika wosia mapema hupunguza migogoro kwa kuwa kila mrithi anafahamu haki yake.

“Anapofariki, kila mmoja anaanza kubeba anachotaka, familia zinavurugika, na hata watu wa nje wanaingia kuchochea migogoro ili wanunue mali kwa bei ya chini,” amesema.

Pia, amesema kutoweka wazi mali na madeni ni changamoto nyingine ambayo watu hawaweki wazi mali wanazomiliki au madeni wanayodaiwa na wanayodai.


“Mirathi haihusu mali tu, bali pia madeni ukiwa hai ni vyema kuyaweka wazi kwa familia au kuyaandika kwenye wosia. Vinginevyo, wadai wanaweza kujitokeza baadaye na kusababisha sintofahamu,” amesema.

Kutokusajili mali kisheria

Gumada amesema watu wengi humiliki magari, nyumba au viwanja bila kusajili kwa majina yao halali.

“Unakuta mtu amenunua gari lakini hakufanya mabadiliko ya majina anapofariki gari bado linasomeka kwa jina la mtu mwingine. Hapo ndipo mgogoro unaanzia kwa kukosekana kwa ushahidi kama kweli hiyo mali ni ya marehemu,” amesema Gumada.

Amesema hata kwa nyumba au ardhi, baadhi hununua lakini hawafanyi uhamisho rasmi wa umiliki, hali inayoweka mazingira ya migogoro mikubwa ya kisheria.

Sababu nyingine amesema kutoifungua mirathi kwa wakati kwa mujibu wa sheria inapaswa kufunguliwa ndani ya siku 30 na isizidi miezi 12 baada ya kifo cha marehemu.

Amesema baada ya hapo kesi husikilizwa ndani ya siku 90.

Pia, amesema msimamizi wa mirathi aliyepitishwa na mahakama hudumu miezi sita na anatakiwa kugawa mali kwa wahusika ndani ya miezi minne endapo hakutakuwa na migogoro, kisha anatakiwa kupeleka taarifa mahakamani kwa ajili ya rekodi ya hukumu.

Gumada amesema baadhi ya familia huchukua miaka mingi kabla ya kufungua mirathi, na wanapofika mahakamani hukuta muda umepita au pingamizi linawekwa kuwa wamechelewa.

“Mtu anafariki leo, lakini mirathi inafunguliwa baada ya miaka 10 au 12. Hapo tayari mali nyingine zimeharibika au zimeuzwa hii inaleta migogoro mipya,” amesema.

Jambo lingine amesema kuteuliwa kwa msimamizi asiye mwaminifu na kuamua kujinufaisha mwenyewe na kusahau kuwa ni msimamizi tu na si mmiliki wa mali.

Ametoa wito kuhusu umuhimu wa kuandika wosia, kusajili mali kisheria, kuweka wazi madeni na kufungua mirathi kwa wakati ili kulinda amani ya familia.