LICHA ya kushindwa kutinga robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, bingwa wa kihistoria nchini, Yanga imeendelea kupaa Afrika katika viwango vya ubora kwa klabu za soka ikishika nafasi ya 10, huku watani zao, Simba ikiporomoka kwa nafasi tatu.
Hata hivyo, chati hiyo imewaibua wadau kadhaa waliotoa mtazamo juu ya orodha hiyo mpya na namna vigogo wa Simba na Yanga wanachotakiwa kufanya ili kuzidi kuipeperusha bendera ya Tanzania katika anga la kimataifa baada ya msimu huu kuyumba na kutoingia robo fainali.
Katika orodha hiyo mpya klabu za Azam FC na Singida Black Stars zilizotinga makundi ya Kombe la Shiri-kisho na kukwama kwenda robo zimechomoza kwa mara mara ya kwanza, matajiri wa Jiji la Dar es Sa-laam wakiwa nafasi ya 38 nyuma ya Singida iliyo 37 na alama tano vilevile.
Yanga imechupa kwa nafasi mbili hadi kuingia 10 bora kwani awali ilikuwa ya 12 kabla ya kuanza kwa msimu huu wa mashindano ambayo yapo robo fainali na droo yake ikifanyika jana huko Cairo, Misri.
Kwa mujibu wa chati mpya iliyotolewa na CAF, Yanga ipo nafasi ya 10 kutokana na pointi 35 ilizokusanya kwa ushiriki wa michuano ya shirikisho hilo katika misimu mitano iliyopita.
Wakati Yanga ikiwa na pointi 35, Simba ipo nafasi ya nane kutokana na pointi zake 38 ambazo ime-kusanya katika kipindi hicho.
Katika kipindi cha misimu minne iliyopita, Simba imefika hatua ya fainali mara moja huku mara mbili ro-bo fainali na hatua ya makundi mara moja.
Orodha hiyo ya klabu bora Afrika inaongozwa na Al Ahly yenye pointi 66, Mamelodi Sundowns (58), Esperance de Tunis (53), RS Berkane (52), Pyramids FC (48), Al Hilal (39), Zamalek (39), Simba (38), USM Alger (37) na Yanga ikikamilisha 10 Bora ikiwa na pointi 35.
Kocha wa Pamba Jiji, Francis Baraza amewapongeza wachezaji wa timu zote akiweka wazi kuwa wamepambana sana wangekuwa na wakati mzuri wakuongezewa ufundi wangefika mbali, viongozi wameona wapi tatizo lilipo walifanyie kazi kabla ya nafasi nyingine.
“Timu zetu kutokufanikiwa kufanya vizuri kwanza kwa upande wangu binafsi ni zimekuwa na panda shuka zimekuwa na msururu wa kubadilisha makocha na wachezaji maanake kila mwalimu anakuja na mbinu zake na wachezaji inawachukua muda ili waeze kuingia kwenye mifumo ya mwalimu pamoja na wachezaji wenyewe kuzoeana wenyewe kwa wenyewe ila timu zote kwa upande wangu bado zipo imara,” alisema kocha huyo raia wa Kenya na kuongeza:
“Kwa mfano Simba imefanya mabadiliko makubwa kwa kuingiza wachezaji wengi wa kigeni na wengi wameondoka hilo pia ni tatizo kisha wamebadilisha walimu hiyo pia inachangia pakubwa kushindwa kufanya vizuri wanabadilika muda tayari ushawatupa mkono.”
Kwa upande wa Yanga, Baraza alisema timu haipo vibaya ila changamoto iliyo waangusha ni mabadiliko ya benchi la ufundi na ongezeko la wachezaji wachache.
“Yanga wachezaji wengi ni walewale lakini mabadiliko ya benchi la ufundi ya mara kwa mara yamekuwa yakiwachanganya wachezaji kwani kila kocha anakuja na mbinu tofauti tayari inamchanganya mchezaji jambo jema ni mipango kufanywa mapema wasiwachanganye wachezaji kilichotokea ni funzo kwa viongozi wajue muda sahihi wakuingiza maingizo mapya kwa wakati.”
Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Salim Mbonde alisema sababu ya Simba kushindwa kufanya vizuri ni mabadiliko ya mara kwa mara yamekuwa benchi la ufundi huku akimtaja Fadlu Davids kuwa uongozi ulifanya makosa kumruhusu aondoke kwani tayari alishaojenga timu.
“Simba imetoka kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho ikiwa tayari na kocha ambaye ametengeneza timu haikutakiwa kumuachia ili iendelee kufanya vizuri kwani tayari wachezaji walikuwa wameten-geneza muunganiko, kitendo cha kocha kuondoka timu imevunjika na kusajiliwa mpya. Hii ndio changamoto ya wao kushindwa kuendeleza ubora,” alisema Mbonde na kuongeza:
“Hivyo hivyo kwa upande wa Yanga licha ya ubora waliouonyesha makosa machache waliyoyafanya kwenye mechi mbili nyumbani yamewagharimu kushindwa kutinga hatua ya robo fainali walikuwa bora na wameonyesha ushindani ndio maana wamesonga kwenye nafasi ya kumi wakiendelea kupunguza makosa wana nafasi ya kufika tano bora Afrika.”