Kondoa. Matumizi ya kuni na mkaa katika minada na masoko ya samaki nchini yametajwa kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira na afya za wananchi.
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba ametoa kauli hiyo leo Jumanne Februari 17, 2026 wakati akizindua mradi wa nishati safi ya kupikia kwa taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100.
Uzinduzi huo umefanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa ambapo ameelekeza wasimamizi wa minada kote nchini, kuhakikisha uchomaji nyama na samaki kwa kutumia kuni na mkaa unakomeshwa.
Amesema pamoja na mapambano makubwa yanayoendelea katika ulinzi wa misitu, bado eneo hilo halijatupiwa jicho lakini ni hatari kwenye suala la uharibifu.
“Tanzania Bara tuna minada 13,763 na masoko ya samaki 1,229 ambao wote wanatumia kuni na magogo kwa kiasi kikubwa, hapa tusipoangalia kazi yetu itakuwa bure,” amesema Makamba.
Amefafanua kuwa lengo la Serikali la kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo 2034 ni kubwa ambalo linahitaji mkakati wa pamoja ili kulifikia.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) Balozi Jacob Kingu amesema mradi huo unalenga kuzifikia taasisi 453 kwa gharama ya Sh25.8 bilioni.
Balozi Kingu amesema hadi sasa wameshazifikia shule 52 na chuo kimoja cha Veta katika awamu ya kwanza lakini wanalenga kuzifikia taasisi 400 zilizobaki katika awamu ya pili.
Awali, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Jones Olotu amesema mapokeo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na mazuri ambapo kambi 22 ya jeshi zimeanza kutumia mfumo huo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kondoa, Flora Nussu amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 870 ambao wamefungiwa jiko lenye uwezo wa tani moja lakini wanaweza kupikia kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu.
Naibu wa Nishati Salome Makamba (mwenye) mavazi meupe akiangalia chakula cha wanafunzi kilichopigwa kwa jiko la Nishati safi
Nussu amesema muda mwingi ulikuwa unapotea kwenye upishi ambao mara kadhaa kuni na mkaa vilikuwa vikiwasumbua lakini sasa hawatapata adha hiyo.