Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amemuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (RC), Beno Malisa na Mkuu wa Wilaya ya Chunya (DC), Rehema Medusa, kuhakikisha kabla hajaanza ziara mkoani humo wawe wamepatia ufumbuzi kesi ya madai ya Mzee Philip Mbelwa ambaye hukumu ilishaamuliwa na Mahakama.
Mbelwa ambaye amelalamika mbele ya Waziri Mkuu, akisema licha ya mahakama kumpa ushindi kwenye kesi yake ya madai aliyosota nayo kwa miaka 13 imekuwa ngumu kutekelezwa na amekuwa akizungushwa.
Kilio cha mzee huyo kimeibuka leo Jumanne, Februari 17, 2026 wilayani Lushoto, Mkoa wa Tanga ambapo waziri mkuu anafanya ziara ya kikazi na kuzindua jengo la hewa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
Katika maagizo yake, Dk Mwigulu amemuelekeza mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya kutekeleza hukumu hiyo.
“Hivi ni vyombo vyetu vya sheria lazima tuviheshimu, kama chombo cha sheria ikisema huyu anastahili hatupaswi kuwa na mtu anaitwa mbabe anashikilia haki ya mtu mwingine,” amesema.
Amesema kabla ya kufika mkoani Mbeya, akute mzee yule amepatiwa haki yake.
“Nitaanza kufuatilia, haya ndio mambo yanayoudhi watu kujitokeza na kujiona wao ni jeuri zaidi, wababe kwenye jambo ambalo hukumu ya mahakama chombo chetu cha imeshahukumu, haiwezekani mzee huyo adhulumiwe eneo lake,” amesema.
Katika maagizo yake, Waziri Mkuu amemuelekeza mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya kutekeleza hukumu hiyo.
Mzee huyo mkazi wa Tanga amesema alikuwa na kesi ya madai kwa miaka 13 na baada ya hukumu kutoka na kutakiwa kupewa haki yake ya ardhi hapati ushirikiano wowote ndani ya vyombo vya Serikali.
“Nikiomba msaada polisi inakuwa tatizo, hakimu Wilaya ya Chunya analijua hilo,” amesema.
Mbali na tukio hilo mwananchi mwingine Mussa Ramadhani, mkazi wa kijiji cha Bombo aliwasilisha kero yake kwa kusema kuwa Hospitali ya Lushoto ina changamoto ya utoaji huduma za afya licha ya uwepo wa majengo mazuri.
“Mtoto mdogo amelazwa hapa, mwenye mtoto anapewa karatasi akanunue dawa na mimi sio kwamba nazungumza tu, mjukuu wangu alilazwa jengo la mama na mtoto akawekewa mashine ya kupumulia nikapewa karatasi ya kwenda kununua dawa,” amesema.
Mzee huyo amesema baada ya kutafuta dawa bila mafanikio alimpigia simu mwanaye aliyepo Tanga amnunulie na kumtuma kwa basi na alipopata alipeleka kwa daktari.
Akijibu changamoto hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Japhet Simeo amesema baada ya kufungua jengo la mama na mtoto walianzisha huduma ya watoto mahututi na hiyo ni moja ya huduma ngeni katika sekta ya afya ngazi ya msingi.
Amesema huduma hiyo hupatikana katika hospitali za rufaa za mikoa na kikanda hivyo kulikuwa kuna baadhi ya huduma za dawa zinazowasaidia watoto kupumua vizuri na tatizo hilo la dawa limefanyiwa kazi.
Baada ya majibu hayo, Dk Mwigulu amekiri kukutana na changamoto kama hiyo wilaya ya Kilindi akimtaka Waziri wa Afya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kukaa na kutafutia utatuzi changamoto ya namna hiyo kote nchini.
“Wakati mzee anaelezea yasingekuja majibu ya kuridhisha ningejua ni zile biashara tulizokomesha,kila dawa inakosekana hospitali za umma lakini zinapatikana duka binafsi, Rais Samia amechukua hatua kubwa sana ndani ya sekta ya afya,”amesema.