Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amemuhoji shahidi wa tisa wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili kuhusu kifungu kilichomuongoza kujionya na kujiandikia maelezo yaliyomfanya kuwa shahidi katika kesi hiyo.
Lissu amemweka shahidi huyo katika kibano hicho wakati akimhoji maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wake alioutoa mahakamani pamoja na maelezo yake aliyojiandikia mwenyewe, akimpitisha katika Mwongozo wa Utendaji wa Jeshi la Polisi (PGO).
Askari anapokuwa ametekeleza jukumu lake kama vile upelelezi/uchunguzi, ukamataji au upekuzi huandika maelezo ya alivyotekeleza jukumu hilo ambayo yanamfanya kustahili kuwasilishwa mahalamani kama kielelezo cha ushahidi na yeye mwenyewe kuwa shahidi.
Katika kutekeleza majukumu hayo askari polisi huongozwa na sheria mbalimbali hususan zinazohusiana na jinai kama Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), pamoja na PGO ambayo ndio mwongozo wa Jeshi la Polisi, kwa askari klatika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusu kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inasikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Shahidi huyo huyo wa tisa wa Jamhuri PS 18544 ASP Geofrey Aggrey (47), mkazi wa Arusha, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, kikosi cha Ant robbery ametoa ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude.
Pamoja na mambo mengine ameieleza mahakama walivyopata taarifa za vijana kuhamasishana kuzuia Uchaguzi Mkuu 2025 na kwamba walipowahoji walisema walikuwa wanamuunga mkono Lissu katika kauli yake ya “No reforms no election’ yaani bila mabadiliko hakuna uchaguzi.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake huo shahidi huyo amehojiwa maswali ya Dodoso na Lissu, pamoja na mambo mengine kuhusiana na utekelezaji wa majukumu yake pamoja na matumizi ya PGO. Sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo:
Lissu: Unaifahamu Police General Order (PGO)?
Lissu: Waeleze majaji kama ni sahihi au siyo sahihi askari Polisi wanatakiwa wawe ni watu wenye weledi katika kazi zao.
Lissu: Waeleze majaji kama ni kweli au si kweli, kwa mujibu wa PGO, Polisi wanatakiwa kuwa waaminifu na wasiwe na upendeleo, wasiwe mafisadi.
Lissu: Sasa narudi kwenye PGO, uliandika maelezo yako Aprili 18, 2025 ni kweli au si kweli?
Lissu: Waheshimiwa majaji, naomba shahidi apewe maelezo yake ayasome (ambayo tayari yalishapokewa kuwa kielelezo cha 8 cha upande wa utetezi (D8).
Lissu: Nani aliyekupa onyo wakati unaandika hayo maelezo (anauliza Lissu baada ya shahidi kupewa na kuyasoma maelezo hayo).
Shahidi: Hakuna aliyenipa onyo
Lissu: Nani aliyekushuhudia?
Shahidi: Hakuna aliyeshuhudia
Kisha Lissu amemuuliza shahidi huyo kuhusiana na maelezo mbalimbali aliyoyatoa shahidi kizimbani ambayo hayapo katika maelezo yake aliyoyaandika.
Lissu: Kama ni muhimu, waeleze majaji kama yapo katika maelezo yako ya onyo
Shahidi: Huwezi kuandika kila kitu
Lissu: Wewe ni mpelelezi mzoefu wa miaka 15, ni kweli?
Lissu: Kama huo uzoefu wa miaka 15 ya uzoefu wako wa upelelezi, uliandika kwenye maelezo yako ya onyo.
Shahidi: Siwezi kuandika kila kitu kwenye maelezo ya onyo.
Lissu: Shahidi umetueleza umefanya kazi maeneo ya Oysterbay, Geita na Arusha, umeeleza hayo maeneo uliyofanyika kazi kwa sababu unataka majaji wajue ulifanya kazi maeneo hayo.
Lissu: Tutakesha hapa ukijifanya mjuaji.
Lissu: Kwenye maelezo yako ya onyo, haya maeneo umeyaandika?
Shahidi: Nimesema siwezi kuandika kila kitu
Lissu: Ulivyowahoji watuhumiwa wale baada ya kuwakamata, walikueleza wanaunga mkono kauli ya mwenyekiti Tundu Lissu, kuwa watakinukisha, ni kweli au si kweli?
Lissu: Sasa waeleze majaji kama hayo maelezo yapo kwenye maelezo yako ya onyo.
Shahidi: Siwezi kuandika kila kitu.
Lissu: Ieleze mahakama kati ya utofauti wa maelezo aliyaondika Polisi na maelezo aliyoyatoa mahakamani.
Shahidi: Siwezi kuandika kila kitu katika maelezo yangu ya onyo, ndio maana naeleza na kutoa ufafanuzi.
Lissu: Sasa shahidi turudi kwenye PGO.
Lissu: Naomba uthibitishe tena wewe ASP Geofrey Mtufye, kama unayafahamu masharti ya PGO.
Shahidi: Nafahamu lakini…
Lissu: Shahidi sijaanza hata kukuuliza umeshaanza ulalamishi (amesema Lissu huku akicheka)
Shahidi: Hapana, ila hiyo PGO ni pana.
Lissu: Makosa ni matendo yaliyofafanuliwa na sheria, sawa sawa? Upelelezi wa Polisi lazima ujikite katika nguvu ya uchunguzi.
Lissu: Sasa waeleze majaji kuzuia uchaguzi mkuu usifanyike ni kosa kwa mjibu wa sheria gani?
Lissu: Kama PGO inasema upelelezi wenu uzingatie sheria zilizopo sasa ulienda kukamata watu kwa sababu gani?
Shahidi: Kwa sababu walikuwa wanafanya kosa la kula njama
Lissu: Nani aliyekwambia ujiandikie maelezo mwenyewe?
Lissu: Nani alikwambia utajishuhudia mwenyewe?
Lissu: Nani alikwambia ujionye mwenyewe baada ya kuandika maelezo yako?
Lissu: PGO namba 236, imeweka utaratibu wa kuandika maelezo.
Lissu: Sasa ni kifungu gani kinakupa mamlaka wewe kujiandikia maelezo yako Polisi?
Lissu: Hukumbuki au hufahamu?
Lissu: Waeleze majaji, kama kifungu cha 10(3b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kama unaruhusiwa kuandika maelezo yako na kujikanya wewe?
Shahidi: Kuna sheria inaniruhusu, ila nimekisahau.
Lissu: Ni kweli au si kweli maelezo yako yanaweza kuandikwa na askari mwingine?
Shahidi: Yanaweza kuandikwa na mwingine au na mimi
Lissu: Ni kweli au si kweli kwamba askari anayekuandikia maelezo ndiye anayekupa onyo la kusema ukweli?
Lissu: Kuzuia uchaguzi mkuu ni kosa gani?
Lissu: Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, hakuna kosa la namna hiyo.
Shahidi: Mimi najua ni kosa.
Lissu: Kwa sheria gani? Ya Kingai (Ramadhani Kingai Mkurugenzi wa Upelelezi – DCI) na Wambura (Camillius Wambura, Mkuu wa Jeshi la Polisi – IGP) ?
Shahidi: Nimesema sikumbuki
Lissu: Unafahamu kwa nini mimi nashtakiwa kwa kosa la uhaini? Waeleze majaji
Shahidi: Nafahamu ni kauli uliyotoa kuwa utazuia uchaguzi Mkuu
Kesi inaendelea kesho Jumatano