Njombe yachukua hatua kudhibiti homa ya nguruwe

Njombe. Wafanyabiashara wa nguruwe katika halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani hapa wametakiwa kuchukua tahadhari katika kununua wanyama hao nje ya mkoa huo, ili kukabiliana na ugonjwa wa homa ya nguruwe ambao umeripotiwa mkoani Mbeya.

Onyo hilo limetolewa leo Februari 17, 2026 na Ofisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Samora Mgaya wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema wafanyabiashara wa nguruwe mkoani humo wanatakiwa kuhakikisha wanachukua tahadhari hiyo kutokana na ugonjwa huo hatari.

Amesema katika mji wa Makambako bado hakuna taarifa za kuwepo kwa ugonjwa huo lakini wafanyabiashara wasinunue wanyama hao nje ya mji wa Makambako ili kuepusha kueneza ugonjwa wa homa ya nguruwe.

Amesema wafugaji wa nguruwe waache kulisha mabaki ya vyakula kwani inaweza kusababisha wanyama hao kula vyakula vyenye viashiria vya magonjwa na hatimaye kupata ugonjwa huo wa home ya nguruwe.

“Mfugaji akiona nguruwe ameanza kubadilika rangi kwenye masiko na chini ya tumbo na anashindwa kula, aripoti kwa maofisa mifugo ili aweze kusaidiwa,” amesema Mgaya.

Amewataka wafanyabiashara wa nguruwe ndani ya halmashauri hiyo wazingatie tahadhari hiyo na yeyote atakayekiuka maagizo hayo, atachukuliwa hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa Wafugaji na Wafanyabiashara wa Nguruwe katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, Yurick Msaki amesema maelekezo yaliyotolewa na halmashauri hiyo wameyapokea na kuahidi kufanyia kazi ili kudhibiti ugonjwa huo kuingia Makambako.

Amesema endapo wafanyabiashara watapuuza agizo lililotolea na Serikali, itasababisha biashara ya nyama ya nguruwe kusitishwa kwa muda, hivyo kushindwa kuingiza kipato.

“Kwetu ugonjwa haupo lakini tunachukua tahadhari watu wasiende Mbeya kuchukua mifugo wakaleta hapa na kusababisha kuenea,” amesema Msaki.

Baadhi ya wananchi mkoani Njombe wamepongeza hatua hyo yenye lengo la kusaidia kupunguza magonjwa ya mifugo.

“Ni hatua nzuri halmashauri kutoa tahadhari kwa wafanyabiashara kutonunua nguruwe kutoka nje ya mkoa, hii itasaidia kupunguza magonjwa,” amesema mkazi wa Njombe, Petro Mwalongo.