Mbeya. Mtu mmoja anayedaiwa kuwa mwanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE) kampasi ya Mbeya, Tido Kadaga amekutwa amefariki dunia kwenye dimbwi la maji katika mtaa wa Maili tano, Kata ya Iganzo Jijini Mbeya.
Tukio hilo limetokeo leo Februari 17,2016 baada ya baadhi ya mashuhuda na wasamiria wema kuripoti taarifa hiyo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufuatia kuona mwili huo ukielea juu ya dimbwi la maji ambapo askari wa jeshi hilo walifika eneo la tukio na kuuopoa mwili huo na kuupeleka Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya kwa uchunguzi zaidi.
Akithibitisha tukio hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Zimamoto Mkoa wa Mbeya, Malumbo Ngata amesema saa 8 mchana walipokea wito wa uwepo wa mtu anayeelea kwenye dimbwi katika Mtaa wa Maili tano Kata ya Iganzo jijini Mbeya, ambapo walifika na kukuta mwili huo ukielea.
Amesema baada ya kutoa mwili amebainika kuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Biashara (CBE) Kampasi ya Mbeya aliyetambuliwa kwa jina la Tido Kadaga (20), ambapo mwili umepelekwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Bado hatujajua chanzo chake tunaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kubaini sababu, mwili tumeupeleka Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya kwa ajili ya uchunguzi zaidi.”
“Tunawashukuru wasamaria wema waliotufahamisha uwapo wa tukio hili, lakini wananchi wachukue tahadhari hasa kipindi hiki cha mvua hapa Mbeya, tuwaangalie watoto na wazee, wasipime kwa macho madimbwi yaliyojaa maji kama hakuna ulazima wasijaribu kuvuka,” amesema Kamanda huyo.
Ameongeza kuwa kwa sasa Jeshi hilo lina vyombo vya uokozi vya kisasa na huduma ni saa 24 akiomba jamii inapokutana na kukutwa na. “Likitokea janga lolote piga namba 114 ili kupata msaada wa haraka na bila gharama.”
Alipotafutwa Mkuu wa Chuo cha Biashara (CBE) Kampasi ya Mbeya, Dk Beny Mwenda kuhusiana na tukio hilo amesema wanasubiri taarifa rasmi za Jeshi la Polisi kisha kulitolea ufafanuzi.
“Tutalizungumza kesho, kwa sasa tunasubiri taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi, tusubiri,”amesema kwa kifupi Dk Mwenda alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu.