Tanga. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesitisha leseni 43 za uchimbaji wa madini ya Bauxite zilizotolewa katika eneo la makazi ya wananchi wa Kijiji cha Magamba, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ambazo zilikuwa zinasubiri kujadiliwa na kupitishwa kwa ajili ya kuanza shughuli za uchimbaji.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumanne, Februari 17, 2026 wakati akisikiliza na kujibu kero za wananchi ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Tanga.
Akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua mtambo wa kuzalisha hewa tiba (oksijeni) katika Wilaya ya Lushoto, Dk Mwigulu amehoji sababu za kutolewa kwa leseni hizo katika eneo la makazi bila kujiridhisha kikamilifu na athari za kimazingira, akisisitiza kuwa madini ni rasilimali muhimu lakini hayapaswi kuchimbwa katika maeneo ya makazi ya watu.
Amesema baadhi ya kemikali zinazotumika katika shughuli za uchimbaji zinaweza kusababisha madhara kwa afya ya jamii, hivyo tahadhari ni lazima ichukuliwe.
Ameelekeza kuwa leseni zote 43 zilizopo kwenye makazi ya wananchi zisitishwe mara moja, isipokuwa zile ambazo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) limejiridhisha nazo baada ya tathmini ya athari za mazingira.
“Hizi leseni zote 43 zilizopo kwenye makazi ya watu zisiendelee. Tusisaini kinyemela na kuweka wananchi kwenye hatari ya kiafya. Nataka kuona taarifa ya Nemc, zipi wamejiridhisha nazo ziko salama ziendelee, lakini hizi nyingine hakuna,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, amesisitiza kuwa iwapo mpango wa kuchimba madini katika eneo hilo utaonekana ni lazima katika eneo hilo, basi wananchi wahusika wapewe fidia stahiki na kuhamishiwa maeneo mengine salama.
Akizungumza katika mkutano huo, mkazi wa Magamba, Asha Mohamed amesema eneo hilo liliwahi kupigwa marufuku kwa shughuli za uchimbaji kutokana na athari za kimazingira na kushangazwa kusikia kuwa kuna leseni 43 zinazotarajiwa kujadiliwa ili kuruhusiwa kuanza uchimbaji baada ya tathmini ya mazingira.
Ameeleza kuwa kijiji hicho ni chanzo muhimu cha maji yanayotumika Lushoto na maeneo ya jirani, hivyo kuruhusu tena uchimbaji kunaweza kuhatarisha upatikanaji wa maji. Pia, amedai kuwa hapo awali kulikuwa na ongezeko la wagonjwa wa kifua kikuu (TB) lililodaiwa kuchangiwa na vumbi kutoka kwenye shughuli za uchimbaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Magamba amesema alipoingia madarakani mwaka 2019 alikuta nyaraka za kusitisha uchimbaji wa madini katika eneo hilo. Amesema kuwepo kwa leseni nyingine 43 zinazodaiwa kusubiri hatua za mwisho kumezua hofu na maswali miongoni mwa wananchi kuhusu uhalali wake.
Kaimu Ofisa Madini Mkoa wa Tanga, Jackson Shirima amemuambia Waziri Mkuu kwamba mgogoro wa awali ilikuwa kati ya wananchi na Kampuni ya Banyambo ambayo ina leseni nne za uchimbaji.
Mgogoro huo ulitokana na madai kuwa shughuli za uchimbaji zilikuwa na athari za kimazingira, na maelekezo ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, yalitaka tathmini ya athari za mazingira ifanyike kabla ya kuendelea na uchimbaji.
Kuhusu leseni 43 zilizotolewa, ofisa huyo amesema kwa mujibu wa Sheria ya Madini, hata kama leseni imetolewa, uchimbaji hauwezi kuanza bila kufanyika kwa tathmini ya athari za mazingira na mamlaka husika kujiridhisha kuwa hakuna madhara kwa jamii na mazingira.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu yuko katika ziara ya kikazi mkoani Tanga akizindua miradi ya maendeleo, kuweka mawe ya msingi na kusikiliza kero za wananchi pamoja na kuzitafutia ufumbuzi.