SEMINA YA UWEKEZAJI KWA WAWEKEZAJI NA WAFANYABIASHARA JIJINI MBEYA

ZAIDI ya wawekezaji na wafanyabiashara 100 wamehudhuria Semina ya Uwekezaji iliyofanyika leo tarehe 17/2/2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, kwa mafanikio makubwa.

Semina hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya uwekezaji, ambapo washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali, kueleza changamoto wanazokutana nazo katika shughuli zao, pamoja na kujifunza na kujadili kwa kina masuala ya uwekezaji na vivutio vinavyotolewa na Serikali kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA).

Aidha, washiriki walipata ufafanuzi wa kina kuhusu fursa zilizopo mkoani Mbeya na namna bora ya kuzitumia kwa manufaa ya uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.

Semina hiyo ilitolewa na Meneja wa Uhamasishaji Uwekezaji wa TISEZA, Bw. Daudi Riganda, ambaye aliwasilisha mada kuhusu vivutio vya uwekezaji, taratibu za usajili, pamoja na faida za kuwekeza kupitia TISEZA.

Mgeni rasmi katika semina hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, ambaye aliipongeza TISEZA kwa kuendelea kusogeza huduma za uwekezaji karibu na wananchi.

Katika hotuba yake alisema, “Nawashukuru sana TISEZA pamoja na Waziri wa Mipango na Uwekezaji kwa jitihada hizi za kumsaidia Rais kufikia DIRA 2050.

Huu ni mwamko mpya wa sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo na kusonga mbele katika safari ya maendeleo.”

Semina hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, yenye lengo la kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu.