Matumaini kwa waandishi, wachapishaji vitabu

Dar es Salaam. Ahadi ya Serikali ya kuchapisha vitabu vya washindi wa Tuzo ya Taifa ya Uandishi Bunifu ya Julius Nyerere imeanza kutekelezwa, hatua inayotajwa kuwa ya kihistoria katika kuhuisha sekta ya fasihi na uchapishaji nchini.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), imeanza kuchapisha na kusambaza vitabu vya washindi wa tuzo hiyo katika shule na maktaba za umma, kwa lengo la kukuza utamaduni wa kusoma na kuthamini kazi za ubunifu za Watanzania.

Hatua hiyo imepokelewa vyema na waandishi, wachapaji pamoja na wadau wa elimu wakisema inafungua ukurasa mpya wa matumaini kwa tasnia ya vitabu iliyokuwa ikikabiliwa na changamoto za soko na ukosefu wa motisha.

Mohamed Omari Juma ambaye ni mwandishi wa kitabu cha ‘Ngoma ya Muwele’ amesema hatua hiyo inawapa uhakika wa wasomaji na kuwahamasisha waandishi chipukizi kuingia katika tasnia kwa kuamini kuwa kazi bora zitatambuliwa na kuungwa mkono.

“Kuona kitabu changu kikiingia maktaba za shule ni faraja kubwa. Inanifanya nijue kuwa sauti yangu inawafikia maelfu ya wanafunzi,” amesema Juma.

Kwa upande wake Tune Shaban Salim mwandishi aliyeandika kitabu cha Maziwa ya Kuku amesema hatua hiyo imempa ujasiri wa kuendelea kuandika kazi zinazolenga malezi na maadili ya watoto.

“Watoto wetu wanahitaji hadithi zinazowafundisha kwa lugha rahisi na inayogusa maisha yao. Serikali inapochapisha kazi hizi, inatusaidia kuwafikia watoto wengi zaidi na kujenga kizazi chenye maadili,” amesema.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa vitabu hivyo, Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali iliona kuna haja ya kuweka mkono ili kuzuia anguko la sekta ya uchapaji na uandishi wa vitabu.

Wageni mbalimbali waliohudhuria shughuli ya uzinduzi wa vitabu vya tuzo ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu.



Amesema hatua hiyo inalenga kuchochea uandishi wa vitabu nchini tasnia ambayo katika miaka ya karibuni inaonekana kushuka.

“Ukweli ni kwamba uchapishaji umeshuka na hii ni kwa sababu uandishi nao haufanyiki, sasa tukaona kuna haja ya kuchochea uandishi na tumeona matunda yake kupitia hizi tuzo waandishi wengi wa kazi bunifu za fasihi wamekuwa wakionesha uwezo wao.

“Sasa wanaofanya vizuri zaidi lazima tuwape motisha ili kuhamasisha wengine, tunahitaji waandishi wetu waandike vitu ambavyo vinawezesha watoto wetu kupandikizwa kuhusu uzalendo na umuhimu wake, ndiyo maana tunasisitiza kuwa na waandishi wa ndani,” amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk Aneth Komba amesema kazi kubwa imefanyika katika kuhakikisha vitabu hivyo vinachapwa  na kusambazwa katika shule na maktaba zote nchini kwa nakala nane hadi 10 ya kila kitabu kwa shule.

Amesema hilo limewezekana kutokana na utayari wa Serikali kutenga fedha kwa ajili hiyo ambapo mwaka  2024/25, zilitengwa Sh1 bilioni kwa ajili ya vitabu na kati ya hizo Sh400 milioni zilitengwa kwa ajili ya kuchapa na kusambaza vitabu vya washindi wa kwanza wa tuzo hii katika kila fani. 

“Fedha hizi zimetumika kuchapa jumla ya nakala 142,000 ambazo zitasambazwa katika shule zote kwa uwiano wa kati ya vitabu 10 na vinane kwa shule. Aidha, vitabu hivi vimeshapatiwa ithibati ya Kamishina wa Elimu inayoruhusu kutumika katika shule zetu,” amesema Dk Aneth.

Mhadhiri wa fasihi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benard Shio amesema vitabu hivyo vinasaidia kuimarisha utambulisho wa Taifa kwa kuwa vinazungumzia maisha, historia na changamoto halisi za jamii ya Kitanzania.

Amesema upatikanaji wa vitabu hivyo katika maktaba za umma utasaidia pia kuamsha ari ya usomaji miongoni mwa vijana, jambo linaloelezwa kuwa limepungua kutokana na ushindani wa teknolojia na mitandao ya kijamii.

“Tunapoweka vitabu vya waandishi wetu shuleni, tunawajenga watoto wetu kwa hadithi zinazoakisi mazingira yao. Hii ni uwekezaji wa moja kwa moja katika fikra za kizazi kijacho,” amesema Dk Shio.