Dar es Salaam. Wakati Watanzania wengi bado wanategemea tiba asili, Tanzania inapiga hatua kubwa katika ajenda yake ya utalii wa tiba, huku nchi jirani zikianza kuelekeza wagonjwa wao hapa nchini kwa ajili ya kupata matibabu ya kibingwa.
Juni 2025, Wizara ya Afya iliieleza Bunge kuwa maboresho ya miundombinu ya hospitali, upanuzi wa huduma za kibingwa na kuimarika kwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi yamechangia kupunguza safari za wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi, huku pia yakivutia wagonjwa kutoka mataifa mengine.
Mbali na taasisi za Serikali kama Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), hospitali kadhaa za binafsi, ikiwemo Aga Khan, pia zimekuwa zikipokea wagonjwa wa kimataifa.
Takwimu rasmi zinaonesha kuwa utalii wa tiba nchini unaendelea kukua. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, idadi ya wagonjwa wa kimataifa iliongezeka kutoka 5,705 mwaka 2021 hadi 12,180 kufikia Machi 2025.
Kitabu cha bajeti cha wizara kwa mwaka wa fedha 2025/26 kinaonesha kuwa wagonjwa hao wanatoka katika nchi za Comoro, Malawi, Burundi, Zambia, Rwanda, Afrika Kusini, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan, Uganda, Zimbabwe, Ethiopia, Somalia, Kenya, Misri na Mauritius.
Hata hivyo, pamoja na kupanuka kwa huduma za kisasa na kuvutia wagonjwa wa kigeni, uhalisia unaojitokeza katika mitaa yenye pilikapilika na makazi yenye msongamano wa watu jijini Dar es Salaam ni kwamba tiba za jadi bado ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku.
Kwa wakazi wengi, uamuzi wa kuchagua tiba hauchochewi tu na gharama au urahisi wa upatikanaji, bali pia na imani za kitamaduni, ushawishi wa familia na ushuhuda wa mafanikio miongoni mwa ndugu na jamaa.
Sababu hizi zinaendelea kufanya tiba za mitishamba kuwa chaguo linalopendelewa, licha ya kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za kisasa za afya.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Ukaguzi wa Utendaji kuhusu Udhibiti wa Tiba za Asili na Mbadala ya mwaka 2024, iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), tiba za jadi bado zinahudumia kati ya asilimia 60 hadi 80 ya Watanzania kwa mahitaji yao ya msingi ya afya.
Jijini Dar es Salaam, utegemezi huo mara nyingi huimarishwa na mila na desturi za kifamilia zinazorithishwa kizazi hadi kizazi.
Joyce Mnema (47), mkazi wa Kariakoo, amesema imani yake kwa tiba za mitishamba ilianzia nyumbani.
“Nilianza kuziamini kwa sababu mama na shangazi zangu walikuwa wanazitumia mara kwa mara. Nilipokuwa na tatizo la bawasiri, hospitalini sikupata nafuu. Nilijaribu dawa za mitishamba na nikapona kabisa,” amesema. “Nilipoona wao wamepona, nami nikapata ujasiri wa kujaribu.”
Uzoefu wa kitamaduni pia una mchango mkubwa. Wakazi wengi wamesema waganga wa jadi hushughulikia si tu dalili za mwili, bali pia masuala ya kihisia na kijamii.
“Mganga wa jadi hatibu mwili tu,” amesema Fatuma Haji (44), mwenyeji wa Iringa anayeishi Tabata. “Wanasikiliza, wanashauri na hata kutoa mwongozo wa kiroho. Hospitali haziwezi kutoa muda na uangalizi wa aina hiyo. Namwamini mganga kwa sababu ananijua mimi na familia yangu, na anatibu kwa namna inayonifanya nihisi nimekamilika.”
Ushawishi wa kifamilia unaendelea kuathiri uamuzi wa kiafya, hasa kwa vijana.
Yusuf Mchomvu (23), mjasiriamali wa Tabata, amesema alianza kutumia tiba za mitishamba baada ya kuona mafanikio kwa ndugu yake.
“Kaka yangu alinisisitiza na hata kunipeleka kwa mganga mwenyewe. Baada ya kumuona amepona, nami nikaanza kuamini,” amesema. “Ukishuhudia matokeo ndani ya familia, ni rahisi kuamini.”
Wakazi wengine walitoa ushuhuda kama huo. Rehema Kitama (38), wa Gongo la Mboto, amesema alikulia katika matumizi ya chai za mitishamba kwa magonjwa madogo.
“Mama yangu alikuwa akinielekeza nijaribu mitishamba kwa homa au maumivu ya tumbo. Nilimwamini kwa sababu alizitumia kwa miongo mingi,” amesema. “Hata hospitali zilipokuwepo, nilichagua tiba ambazo familia yangu ilikuwa imefanikiwa kutumia.”
Gharama na urahisi wa upatikanaji pia huimarisha imani hii. Halima Omari, mkazi wa Kigamboni, amesema changamoto za kifedha zilimfanya ampeleke mwanawe kwa mganga wa jadi.
“Mwanangu alipougua sikuwa na uwezo wa kulipia gharama za hospitali. Mganga aliruhusu malipo kwa awamu,” amesema. “Dada yangu alimpendekeza, na nilimwamini kwa uzoefu wake.”
Uhaba wa huduma pia ni sababu. Waganga wengi wa jadi wanafanya kazi ndani ya jamii, mara nyingi hutoka majumbani au katika vibanda vidogo vinavyojulikana na wakazi.
“Kwa magonjwa madogo kama maumivu ya tumbo, sihitaji kusafiri mbali,” amesema Nyasanje Rosobya, wa Kigamboni. “Mganga yupo hapa mtaani. Mara nyingi ni kama ndugu, na hilo hujenga imani.”
Hata hivyo, pamoja na faida hizo, sekta hiyo ina hatari zake.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Ukaguzi wa Utendaji ya mwaka 2025 ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), watu wasiopungua 16 walifariki dunia kati ya mwaka 2020 na Septemba 2024 kutokana na vitendo hatarishi vya tiba za jadi, ikiwemo ramli chonganishi na matambiko yanayohusisha viungo vya binadamu. Vifo vingine saba mwaka 2023 vilihusishwa na dawa zisizosajiliwa.
Ripoti hiyo pia ilibainisha changamoto za uhifadhi usio salama, ukosefu wa usafi na kutokuwepo kwa kumbukumbu za wagonjwa.
Wataalamu wa afya wamesema hali hiyo inaakisi wanayokutana nayo hospitalini.
“Tunachokiona Dar es Salaam ni mchanganyiko wa urithi wa kitamaduni na ushawishi wa jamii,” amesema Daktari Aurelia Sabato, wa Sinza Palestina. “Imani inaporithishwa ndani ya familia, huwa si rahisi kuhojiwa.”
Mtafiti wa afya ya umma, Dk Aaron Kimaro, amesema ushuhuda wa kupona kwa ndugu una nguvu kubwa katika kuunda tabia za kiafya.
Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dk Emmanuel Nyankunga amesema wagonjwa wengi hufika na madhara yanayodhaniwa kusababishwa na dawa za mitishamba.
“Tunaona wagonjwa wenye maumivu ya tumbo, matatizo ya ini au muwasho wa ngozi,” amesema. “Bila kumbukumbu ya dawa alizotumia mgonjwa, matibabu huwa changamoto.”
Katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), watafiti wamesisitiza umuhimu wa tafiti za kisayansi kuthibitisha usalama na ufanisi wa dawa za asili.
Dk Benson Mugaka, wa Taasisi ya Tiba za Asili, amesema usalama lazima uwe kipaumbele.
“Dawa si madai tu ya kuponya. Lazima zipimwe kisayansi ili kuthibitisha usalama na athari zake kwa viungo muhimu vya mwili,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk Winifrida Kidima, amesema Serikali inaendelea kusimamia na kudhibiti sekta hiyo kwa mujibu wa sheria, huku ikitambua umuhimu wake wa kitamaduni.
“Sheria inataka dawa zote za asili zisajiliwe. Tunaendelea kukuza, kusimamia na kufuatilia sekta hii ili kulinda afya ya umma,” amesema. “Lakini ushawishi wa familia na jamii katika kujenga imani ni jambo lisiloweza kupuuzwa.”
Wakati Tanzania ikiendelea kujijenga kama kitovu cha huduma za kibingwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, utegemezi unaoendelea kwa tiba za jadi unaonesha taswira changamano ya sekta ya afya iliyojengwa juu ya maendeleo ya kisasa, urithi wa kitamaduni na mizania nyeti kati ya imani na hatari.