Tumuombee Rais, tuliombee Taifa | Mwananchi

Kauli ya Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, kuwaomba viongozi wa dini kumuombea Rais, Samia Suluhu Hassan, imeibua tafakari pana kuhusu nafasi ya maombi katika uongozi wa nchi.

Hoja hii si ya kiimani pekee; ni hoja ya kitaifa inayogusa dhana ya uwajibikaji, ulinzi wa taasisi ya urais na mshikamano wa Watanzania.

Kwanza, tuangalie kilichosemwa. Makamu wa Rais aliwaomba viongozi wa dini waendelee kumuombea Rais kwa ajili ya afya njema na maisha marefu, ili aweze kuendelea kuliongoza taifa kwa uthabiti.

Pia aliomba aombewe ili apate busara na hekima katika maamuzi ya kila siku, hasa katika kipindi ambacho dunia na nchi zinakabiliwa na changamoto za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kumuombea apate wasaidizi waaminifu, wakweli na wenye mapenzi mema na taifa. Vilevile, alihimiza maombi ya ulinzi dhidi ya watu wabaya, wachonganishi na mafisadi, akisisitiza hata usalama wa Ikulu dhidi ya nia ovu. Kwa maneno yake, kumtikisa Rais ni kuitikisa nchi.

Je, kauli hii ina maana gani?

Kwanza, inaonesha utambuzi kwamba uongozi ni mzigo mzito unaobebwa na mwanadamu mwenye mapungufu ya kibinadamu. Rais, kama kiongozi mkuu wa nchi, hukabiliwa na maamuzi magumu yanayogusa maisha ya mamilioni ya watu.

Katika mazingira hayo, wito wa maombi unaweza kutafsiriwa kama ishara ya kutambua mipaka ya kibinadamu na hitaji la msaada wa kiroho na kimaadili.

Pili, msisitizo wa kupata wasaidizi waaminifu unaashiria ukweli kwamba mafanikio ya Rais hayategemei juhudi zake binafsi pekee. Mfumo mzima wa uongozi unaomzunguka una nafasi kubwa katika kuamua ubora wa maamuzi na utekelezaji wake.

Endapo kuna upungufu katika uadilifu au uwajibikaji wa baadhi ya wasaidizi, athari zake hujionesha moja kwa moja katika taswira na utendaji wa serikali. Hivyo, maombi kwa ajili ya wasaidizi waaminifu ni maombi kwa ajili ya utawala bora.

Tatu, hoja ya kumuombea ulinzi dhidi ya watu wabaya inaakisi tahadhari juu ya uwepo wa hila, fitina na tamaa za madaraka ambazo zinaweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Historia ya mataifa mengi inaonesha kuwa misukosuko mikubwa mara nyingi huanzia ndani ya mifumo ya uongozi. Hivyo, kauli ya kuombea; “kufungwa kwa mageti ya Ikulu” ni lugha ya tahadhari kuhusu hatari zinazoweza kuathiri taasisi ya urais.

Hata hivyo, swali la msingi ni hili: Je, kumuombea Rais ni jukumu la viongozi wa dini pekee? Kwa mtazamo mpana wa kitaifa, jibu ni hapana. Rais ni kiongozi wa Watanzania wote bila kujali dini, kabila au itikadi.

Ikiwa tunatambua kuwa ustawi wa taifa unahusiana na utulivu wa kiongozi wake mkuu, basi ni busara kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yake kushiriki kwa namna yake katika kuombea au kuutakia mema uongozi wa nchi.

Wimbo wa Taifa unaanza kwa dua ya kuwaombea viongozi. Huu ni ushahidi kwamba katika utamaduni wetu, maombi kwa ajili ya viongozi si jambo la kundi fulani bali ni sehemu ya utambulisho wa taifa.

Maombi hayo hayapaswi kubaki kwenye maneno ya wimbo au ibada rasmi pekee; yanaweza kuakisiwa pia katika matendo, kama kuheshimu sheria, kulinda amani na kukemea uovu.

Kwa upande mwingine, maombi hayapaswi kuwa mbadala wa uwajibikaji. Kumuombea kiongozi hakumaanishi kufumbia macho mapungufu au kukwepa kukosoa kwa hoja. Badala yake, ni njia ya kuonesha kuwa tunatamani uongozi bora, wenye hekima na maadili.

Taifa linalojali mustakabali wake hujenga utamaduni wa kuombeana na kukosoana kwa staha kwa lengo la kujenga, si kubomoa.

Kwa hiyo, kauli ya Makamu wa Rais ni mwaliko wa kutafakari zaidi ya masuala ya kiimani. Ni mwaliko wa kujenga mshikamano wa kitaifa unaotambua kuwa taasisi ya urais ni mhimili wa utulivu wa nchi.

Tunapomuombea Rais kwa namna yetu binafsi au kupitia taasisi za dini, tunaombea pia amani, maendeleo na mustakabali wa Tanzania. Kwa waliopitia misukosuko ya nyakati mbalimbali za uongozi, tunajua kuwa utulivu wa kiongozi wa nchi huathiri kwa kiasi kikubwa utulivu wa taifa.

Hivyo, kumuombea Rais asiwe jukumu la viongozi wa dini pekee. Liwe jukumu la kila Mtanzania mzalendo, kwa sababu tunapoliombea taifa kupitia kiongozi wake, tunawekeza katika kesho ya nchi yetu.