Dar es Salaam. Wakati Baraza la Mawaziri nchini Zimbabwe likipitisha rasimu ya marekebisho ya katiba yanayoweza kufungua njia ya Rais Emmerson Mnangagwa kubaki madarakani hadi mwaka 2030, wengi wanajiuliza kama taifa hilo linarejea katika kivuli cha historia yake historia iliyotawaliwa na Robert Mugabe.
Zimbabwe ilipojinyakulia uhuru mwaka 1980, Mugabe aliingia madarakani kama shujaa wa mapambano dhidi ya utawala wa wazungu, akiwa kiongozi wa chama cha ZANU-PF.
Aliahidi maridhiano, elimu kwa wote na usawa wa kiuchumi na miiaka yake ya mwanzo ilionekana kuleta matumaini, ambapo huduma za jamii kama elimu na afya zilipanuka, na taifa lilionekana kuwa mfano wa mafanikio barani Afrika.
Hata hivyo, kadri miaka ilivyosonga, taswira hiyo ilianza kubadilika. Operesheni za kijeshi dhidi ya wapinzani katika eneo la Matabeleland katika miaka ya 1980 zilionesha uso wa kwanza wa utawala mkali chini ya Serikali ya wazawa.
Baadaye, kuanzia mwaka 2000, sera ya mageuzi ya ardhi ilipochukua mkondo wa haraka na wa mabavu, uchumi wa taifa hilo ulianza kuyumba.
Mashamba makubwa ya wazungu yalitaifishwa kwa kasi, uzalishaji wa kilimo ukaporomoka, na Zimbabwe iliyokuwa ghala la nafaka kusini mwa Afrika ikageuka kuwa muagizaji wa chakula kutoka nje.
Uchumi uliingia katika mporomoko wa kihistoria, mfumuko wa bei ukafikia viwango visivyo na mfano duniani, na dola ya Zimbabwe ikapoteza sana thamani yake.
Mataifa ya Magharibi, yakiongozwa na Marekani na Umoja wa Ulaya, yaliweka vikwazo vya kiuchumi na vya usafiri dhidi ya viongozi wa serikali wakidai ukiukwaji wa haki za binadamu na kuvurugwa kwa demokrasia.
Serikali ya Mugabe ilijibu kwa kauli ya kujihami, ikiitaja hali hiyo kama adhabu ya kisiasa kwa sera yake ya kurejesha ardhi kwa Waafrika.
Uhusiano wa Mnangagwa na Mugabe
Katika kipindi hicho, Mnangagwa alikuwa mhimili muhimu wa utawala akishika nyadhifa nyeti kama waziri wa usalama wa taifa, waziri wa ulinzi na makamu wa rais, ambapo kwa wengi alionekana kama mrithi wa ndani wa mfumo wa uongozi wa ZANU-PF.
Uhusiano wake na Mugabe ulikuwa wa karibu lakini wa tahadhari kwani alikuwa mpiganaji wa msituni wakati wa vita ya ukombozi na akajijengea sifa ya kuwa mwana mikakati asiyeogopa maamuzi magumu.
Mwaka 2017, mpasuko ndani ya ZANU-PF ulipozidi, hasa baada ya Mugabe kuanza kumuandaa mkewe Grace kama mrithi, jeshi liliingilia kati kwa kile kilichoitwa “operesheni ya kulinda heshima ya Rais Mugabe.”
Mnangagwa, aliyekuwa amefukuzwa nafasi ya makamu wa rais, alirejea kutoka uhamishoni na kuapishwa kuwa rais baada ya Mugabe kujiuzulu kwa shinikizo la kijeshi.
Hata hivyo, matukio hayo yalielezwa kama marekebisho ya ndani ya chama, si mapinduzi ya kijeshi, lakini yalibeba uzito wa mabadiliko makubwa ya kisiasa huku jeshi likihusika moja kwa moja kumdhibiti Robert Mugabe.
Mwanzoni, akianza utawala wake, Mnangagwa alijitambulisha kwa sura mpya ya Zimbabwe, akijaribu kufungua vikwazo alivyovikuta kwa Taifa hilo dhidi ya mataifa ya nje.
Alijaribu kuvutia wawekezaji, kurekebisha uhusiano na jumuiya ya kimataifa na kuimarisha demokrasia.
Vyombo vya habari vya kimataifa kama BBC na Deutsche Welle nchini humo viliripoti taarifa za matumaini hayo, vikieleza kuwa wananchi wengi walikuwa na matarajio ya zama mpya zisizo na hofu ya ukandamizaji.
Lakini baada ya miaka kadhaa kupita, picha ilianza kufanana na ile ya zamani hasa katika uchaguzi wa 2018 na baadaye wa 2023 ambao ulitawaliwa na tuhuma za dosari na ukandamizaji wa upinzani.
Wanaharakati na wanasiasa wa upinzani walikamatwa au kuzuiwa kufanya mikutano huku Sheria mpya zilionekana kuongeza udhibiti dhidi ya asasi za kiraia na vyombo vya habari.
Ingawa hali ya uchumi ilionesha nafuu kwa kiasi fulani, mfumuko wa bei na uhaba wa fedha uliendelea kuwatesa wananchi wa Taifa hilo.
Katika hatua ambayo imezua mjadala mpana katika siasa za Taifa hilo, pendekezo la marekebisho ya katiba yanayoweza kusogeza mbele ukomo wa urais hadi 2030 limewagawa wanasiasa na wanaharakati nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Zimbabwe na kimataifa, Baraza la Mawaziri limepitisha muswada unaolenga kurekebisha vipengele vinavyohusu muda wa urais na mpangilio wa uchaguzi.
Wafuasi wa hatua hiyo wanasema inalenga kuleta uthabiti wa kisiasa na kuruhusu utekelezaji wa ajenda za maendeleo kwa muda mrefu bila misukosuko ya kampeni za mara kwa mara.
Wakosoaji, hata hivyo, wanaona ishara ya kuondolewa kwa nguzo ya msingi ya demokrasia, ukomo wa madaraka na kuendeleza tawala za muda mrefu kwa marais.
Hofu kuu inaonekana kutokana na historia yenyewe kwani Mugabe alitawala kwa karibu miaka 37, akibadili katiba na sheria mara kadhaa ili kuimarisha mamlaka yake.
Wakati huo, taasisi za dola mahakama, bunge na vyombo vya ulinzi zilionekana kuwa karibu mno na chama tawala hali iliyompa urahisi Mugabe kutimiza matakwa yake.
Leo, wakosoaji wanahofia kuwa Zimbabwe inaweza kuingia katika mzunguko mwingine wa utawala mrefu usio na ushindani wa kweli huku Rais Mnangagwa na wafuasi wake wakikanusha madai ya kutaka kubomoa demokrasia, wakisisitiza kuwa mchakato wa marekebisho unafuata taratibu za kisheria na utapitia bunge kama inavyotakiwa.
Hata hivyo, kwa kuwa ZANU-PF ina ushawishi mkubwa bungeni kwa wingi wa viti, hivyo wapinzani wanaona uwezekano mdogo wa muswada huo kuzuiwa isipokuwa kama kutatokea shinikizo kubwa la umma au la kimataifa.
Swali linaloibuka ni kama Zimbabwe imejifunza kutokana na historia yake au la kwani Taifa hilo limepitia vipindi vya matumaini makubwa na maumivu makali ya kiuchumi.
Aidha, limeona jinsi utawala wa muda mrefu unavyoweza kubadilika kutoka harakati ya ukombozi hadi mfumo wa kulinda maslahi ya wachache.
Sasa, likiwa katika mwaka wa zaidi ya arobaini tangu uhuru, linakabiliwa na mtihani mwingine wa msingi huku mwelekeo wa kisiasa ukiashiria mvutano wa pande mbili.
Kivuli cha Mugabe, aliyewahi kuonekana kama baba wa taifa kisha kuwa mfano wa utawala usio na kikomo, kinaning’inia juu ya Harare.
Ndani ya kivuli hicho, Mnangagwa anajikuta akipimwa si kwa ahadi alizotoa mwaka 2017 alipoingia madarakanikwamara ya kwanza, bali kwa hatua anazochukua leo.
Zimbabwe, kama ilivyokuwa kabla, iko katika njia panda kati ya urithi wa mapambano ya uhuru na changamoto ya kulinda uhuru huo dhidi ya vita vya madaraka.
Wachambuzi watahadharisha
Wachambuzi wa siasa wanaizingumzia hatua hiyo kwa tahadhari na misingi ya kisheria, wakionesha kuwa anachokifanya Mnangagwa hakifanani sana na alichokifanya mtangulizi wake Robert Mugabe, huku wakionya kuwa mchakato huo unaonesha namna viongozi wa mataifa ya Afrika wanavyojaribu kuonesha nia kusalia madarakani muda mrefu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alipozungumza na Mwananchi kuhusu hili amesema si Mnangagwa peke yake anayejaribu kubaduli sheria ili kurefusha muda wa Urais, akisema ipo mifano ya viongozi wengi waliofanya hivyo.
“Madaraka huwa matamu sana, na hii si kwa Mnangagwa tu, wapo viongozi wengi sana tunawaona wanapoingia madarakani wanatamani kusogeza mbele muda wao wa utawala,” anasema.
Anasema kuwa wapo viongozi ambao hufanya hivyo kwa matakwa yao huku wengine hushawishiwa na wafuasi wao na kuchochewa kuingia kwenye mfumo huo.
“Hata hapa kwetu wapo marais wetu waliowahi kushawishiwa na wafuasi wao kukaa muda mrefu madarakani akiwemo Mwalimu Nyerere, hata hivyo hawakukubaliana na ushwishi huo. Tungependa kuwaona watawala wakiridhika na mihula ambayo wamepewa kikatiba ili kuepusha machafuko kwenye nchi zao,” amasisitiza
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo, anasema suala la Mnangagwa ni tofauti na mtangulizi wake Robert Mugabe katika misingi ya kisheria, akibainisha kuwa Robert Mugabe alitawala muda mrefu kwa udhaifu wa kisheria huku Mnangagwa akitumia mifumo rasmi ya kisheria kubadili sheria ya ukomo wa urais.
“Suala la Mnangagwa linapaswa kutazamwa rofauti kwakuwa yeye anafuata utaratibu wa kisheria wa kubadili sheria tena kwa kupitia bungeni kwa wawakilishi wa wananchi, ikiwa watapitisha basi wananchi wa ZImbabwe watakuwa wamepitisha,” anasema.
Dk Masabo anasema kuwa Baraza la Mawaziri kupitisha muswada ni hatua ya kawaida kwani miswada mingi huanzia kwenye baraza la mawaziri kabla ya kufikishwa bungeni.
“Kuhusu hatma yake madarakani kuwa ataondolewa na jeshi au atadumu madarakani hilo ni suala jingine, lakini ikiwa anabadili sheria ili aendelee madarakani hilo siyo tatizo kwakuwa anafuata mfumo sahihi wa mabadiliko ya sheria kama ilivyo kwa sheria zingine zinazobadilishwa kupitia bungeni,” amesema.