Lyimo: Mirungi itakuwa historia Same

Kilimanjaro. Jumla ya kilogramu 299.8 za dawa za kulevya aina ya mirungi zimekamatwa katika operesheni iliyofanyika kwa siku sita wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Mbali na kukamatwa kwa kiasi hicho cha mirungi operesheni hiyo imefanikisha kukamatwa kwa watu saba wanaotuhumiwa kuhusika na dawa hizo za kulevya sambamba na kuteketeza ekari 203 za mashamba ya mirungi.

Ekari hizo za mashamba zilizoteketezwa ni pungufu ikilinganishwa na ekari 376 zilizoharibiwa mwaka 2024 na ekari 550 zilizoteketezwa katika operesheni iliyofanyika mwaka 2023.

Akizungumza na Mwananchi, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo amesema ushirikiano ambao mamlaka hiyo inaupata kutoka kwa wananchi, kilimo cha mirungi kinakwenda kukomeshwa Same.

Amesema kwa muda mrefu kilimo cha mirungi kilikuwa kimeshika kasi wilayani humo lakini kadiri operesheni hizo zinavyofanyika, ndivyo wananchi wanavyoachana nacho na kugeukia kilimo cha mazao mengine.

“Wananchi wametupa ushirikiano mkubwa tumefika katika maeneo ambayo yalikuwa hayafikiki, huko kote tumeteketeza mashamba ya mirungi, tuliporudi tena safari hii tumekuta wanalima mazao kama vitunguu, karoti, migomba na kahawa.

“Nikiangalia hali ilivyokuwa mwaka 2023 na 2024 wakati zile operesheni na tulichokikuta safari hii naweza kusema mwaka huu tunaenda kutokomeza kabisa kilimo cha mirungi kule Same,” amesema na kuongeza

“Serikali imefikisha huduma muhimu ikiwemo umeme na maji safi pamoja na miradi ya kilimo na ufugaji. Wananchi wengi wameanza kujishughulisha na mazao mbadala kama vile vitunguu, viazi, kabeji, parachichi na kahawa,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Amesema hapo awali kilimo cha mirungi kiliathiri hata elimu kwenye vijiji hivyo kwani wanafunzi walikuwa hawaendi shuleni na badala yake walifanya kazi kwenye mashamba hayo kwa ujira wa Sh10,000.

Lyimo amesema mamlaka itaendelea kushirikiana na viongozi wa vijiji, kata, wilaya na mkoa pamoja na wadau wengine kutoa elimu na kutekeleza operesheni endelevu ili kuhakikisha tatizo la mirungi linadhibitiwa kikamilifu katika mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Mhero, Hamad Waziri Hamad, amesema operesheni hiyo itakuwa msaada mkubwa katika kijiji hicho kwa sababu itasaidia vijana wengi kuachana na kilimo na matumizi ya mirungi, kwani madhara yalikuwa mengi kwa vijana ikiwemo vitendo vya uhalifu na kuhatarisha usalama wa wakazi wa maeneo hayo.

Mkazi wa eneo hilo, Chome Kisenge amekiri kuwa hali imebadilika kwa sasa na wanakijiji wengi wamezigeukia fursa zinazopatikana kwenye kilimo cha mazao mbalimbali na kuachana na kilimo haramu cha mirungi.

“Naishukuru serikali kwa kuweka mfumo mzuri, tunapata ruzuku ya pembejeo na hata tukilima katika eneo dogo tumekuwa tukipata faida. Hivyo hakuna sababu za kufanya kilimo haramu” amesema Kisenge.