Moshi. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amemwagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Kilimanjaro kuchunguza miradi ambayo fedha zake zimeshatolewa na haijakamilika na kumpa majibu kabla hajaondoka mkoani humo.
Dk Mwigulu ametoa maagizo hayo leo Februari 18, 2026 akiwa katika viwanja vya stendi ya mabasi ya Ndungu, iliyopo Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Amesema ipo miradi ya shule, afya pamoja na barabara ambayo haijakamilika ilhali Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu amehoji ujenzi wa zahanati ya Sujigojanza ambayo Serikali imetoa fedha lakini haijakamilika.
“Hizi fedha zimekuja siku nyingi kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Sujigojanza, ni kwa nini hamjatekeleza mradi huu. Takukuru naomba tufuatilie kabla sijamaliza ziara ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro, nipate majibu,” amesema Waziri Mkuu.
Akijitetea mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Jimson Mhagama amesema kilichokwamisha mradi wa zahanati hiyo ni kutokana na mgogoro uliopo baina ya kijiji na kijiji.
Aidha, amesema baadhi ya miradi haijakamilika kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza, akimuahidi kukamilisha miradi hiyo.