Dar es Salaam. Hatua mpya ya mapinduzi ya kidijitali katika sekta ya uvuvi imepigwa kufuatia kuzinduliwa kwa soko la samaki la mtandaoni.
Soko hili linalofahamika kama TanFishMarket limelenga kuunganisha wadau wa mnyororo wa thamani wa samaki na kuongeza tija, uwazi na kipato kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika.
Jukwaa hilo la kidijitali limeundwa na timu ya wataalamu wa Chuo Kikuu Kikuu cha Dar es Salaam chini ya Ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliani (CoiCT) ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa FISH4ACP ulio chini ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Akizungumza leo Jumatano, Februari 18, 2026, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema jukwaa hilo ni taswira ya matokeo ya taasisi za elimu ya juu, washirika wa maendeleo na Serikali zinaposhirikiana kwa lengo moja la kuleta maendeleo yenye tija kwa jamii.
Amesema kwa ushirikiano huo umedhihirisha dhamira ya pamoja ya kutumia ubunifu na teknolojia kubadilisha sekta ya uvuvi nchini.
Profesa Anangisye amesema jukwaa hilo linaendana kikamilifu na vipaumbele vya kitaifa kwa kuchochea ukuaji jumuishi wa uchumi, kuimarisha mifumo ya usalama wa chakula, kukuza uchumi wa kidijitali na kuendeleza uchumi wa buluu.
“Kwa kuunganisha wazalishaji, wasindikaji na wanunuzi katika mfumo mmoja wa kidijitali, tunapunguza mianya ya upotevu, tunaongeza uwazi wa bei na tunarahisisha upatikanaji wa masoko.
“TanFishMarket ni mfano wa utafiti wenye matokeo halisi kwa jamii. Maarifa yanayozalishwa chuoni sasa yanageuzwa kuwa fursa za kiuchumi kwa wananchi, hususan wavuvi na wafanyabiashara wa samaki,” amesema.
Amesema taasisi hiyo itaendelea kutoa ubora wa utafiti, ubunifu wa kidijitali na mafunzo kwa jamii ili kuhakikisha mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi unakuwa wenye ufanisi, shirikishi na himilivu.
“Uzinduzi wa leo si mwisho, bali ni mwanzo wa safari pana zaidi ya kuleta athari chanya kwa jamii, chuo chetu kipo kwa ajili ya jamii hivyo tutaendelea kutumia maarifa kufanya yale yanayoweza kubadilisha maisha ya wanajamii,” amesema Profesa Anangisye.
Naye Mratibu wa mradi huo ambaye ni Mhadhiri wa Tehama CoICT, Dk Eva Shayo amesema kupitia jukwaa hilo wauzaji wanaweza kufungua akaunti, kupakia bidhaa, kuweka na kusimamia bei, kufuatilia akiba na kuwasiliana moja kwa moja na wanunuzi.
Mfumo unaunganisha njia za malipo, uratibu wa usafirishaji na zana za ufuatiliaji kwa taasisi husika, kuimarisha uwazi wa bei na uratibu wa ugavi na mahitaji, ukitarajiwa pia kupunguza upotevu wa mazao ya samaki baada ya kuvuliwa, hususan pale unapounganishwa na uwekezaji katika miundombinu ya uchakataji na maghala ya baridi.
Mwakilishi wa FAO Tanzania, Dk Tipo Nyabenyi amesema mabadiliko ya kidijitali si anasa tena bali ni hitaji la lazima katika kukuza ushindani wa sekta ya uvuvi.
Amesema kwa muda mrefu wadau katika mnyororo wa thamani wa Ziwa Tanganyika wamekabiliwa na changamoto za kuyumba kwa bei, utegemezi kwa madalali, miundombinu hafifu ya baridi, gharama kubwa za usafirishaji na ukosefu wa taarifa sahihi za soko.
“Vikwazo hivi vimepunguza faida na kuwanyima wavuvi na wafanyabiashara uwezo wa kunufaika kikamilifu na kazi yao. Jukwaa hili linakwenda kushughulikia changamoto hizi kwa kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi wa ndani, kikanda na hata kimataifa,” amesema Dk Nyabendi.
Amesema matokeo ya awamu ya majaribio yameonesha mafanikio makubwa ambapo zaidi ya wanajamii 200 wamepatiwa mafunzo ya kutumia mfumo huo.
Kati yao, asilimia 62 ni wanawake na asilimia 48 ni vijana, jambo linalotajwa kuwa ishara ya ujumuishaji na fursa mpya za kiuchumi.
Dk Nyabenyi amesema awamu itakayofuata, itaweka mkazo katika kuongeza idadi ya wauzaji na wanunuzi watakaosajiliwa, kuimarisha huduma za kiufundi na upangishaji wa mfumo, pamoja na kuboresha vipengele vya mfumo kulingana na maoni ya watumiaji.